24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

Silanga: Miaka 20 wananchi waliteseka, tumefanya mageuzi ndani ya muda mfupi

Na Derick Milton, Itilima

“Nilianza harakati za Siasa mwaka 2007 baada ya vijana wa Mkoa wa Simiyu kuniamini kwa kunipigia kura 664, kati ya kura 668, vijana wanne tu ndiyo walisema sitoshi kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu CCM,”

Ni maneno yake Mbunge wa Itilima mkoani Simiyu, Njalu Silanga (CCM), ambaye pia anatajwa kuwa mbunge namba moja ndani ya mkoa huo kuungwa mkono zaidi na wananchi wote wa jimbo lake hata wale wa kutoka vyama shindani.

Mbunge wa Jimbo la Itilima Mkoani Simiyu Njalu Silanga akizungumza na wananchi wa Jimbo lake la Itilima, wakati wa sherehe za miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika kiwilaya katika kijiji cha Ndoleleji. (Picha na Derick Milton)

Hadi anafikia hatua ya kuwa Mwakilishi wa wananchi wa jimbo hilo kwenye chombo cha kutunga sheria (bunge), Njalu anasema haikuwa kazi rahisi kupambana na vigogo wa siasa kutoka vyama shindani.

Kutoka mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (MNEC) na Mbunge wa Jimbo la Itilima, anasema alisukumwa zaidi na mateso ya wananchi wa jimbo hilo waliyoyapata kwa miaka 20.

Chini ya vigogo wa siasa, John Cheyo (UDP), Dany Makanga (UDP) na wengine wengi wakiwemo, Edward Ng’wani, zaidi ya miaka 20 wananchi waliteseka na miundombinu mibovu ya barabara.

Ukosefu wa huduma za Afya ilikuwa changamoto nyingine iliyowatesa, ukosefu wa maji safi na salama, kukosekana kwa mazingira rafiki ya upatikanaji wa elimu bora kwa wananchi ni moja ya sababu nyingine.

Utekelezaji wa Ilani

Wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa wananchi wa jimbo hilo jana, wakati wa sherehe za miaka 46 ya kuzaliwa kwa chama hicho zilizofanyika katika kijiji cha Nangale kata ya Ndoleleji.

Anasema baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka 2015, kazi yake ya kwanza ilikuwa kuhakikisha anatatua changamoto ya miundombinu ya barabara ambayo ndiyo ilikuwa kilio kikubwa cha wananchi.

“Nikiwa na Madiwani saba kutoka CCM kati ya 22, tulifanya kazi kubwa usiku na mchana ya kuhakikisha jimbo la Itilima linabadilika, wananchi wanaanza kuonja raha ya maendeleo na kupata huduma bora za kijamii,” anasema Njalu.

Miundombinu ya Barabara

Mbunge huyo anasema kuwa kwa kipindi cha miaka saba, Wilaya ya Itilima imefunguka, kila sehemu panapitika kwa nyakati zote tofauti na awali ambapo hakuna gari ilifika kijijini.

Anaeleza kuwa Wilaya hiyo inazo barabara kubwa na muhimu zipatazo 82, ambapo kwa sasa zote zimefunguliwa na zinapitika muda wote na wananchi wanafanya shughuli zao kwa furaha.

“Kila mwaka nimekuwa nikihakikisha tunatapa fedha za kutengeneza barabara zetu, kwa sasa unaweza kuingia na kutoka Wilaya ya Itilima kwa kupitia sehemu yoyote, hakuna kikwazo hata kimoja. Tunamshukuru sana Rais Dk. Samia Suruhu Hassan kwa kuendelea kutuletea fedha nyingi kwenye eneo la miundombinu na katika bajeti ya mwaka huu ametupatia Sh bilioni 2.7 kwa ajili ya barabara tu,” anasema Njalu.

Huduma za Afya

Njalu anasema kuwa wakati anaomba kura kwa wananchi kipaumbele chake cha pili ambacho aliwahidi wananchi ni kuhakikisha wanapata huduma bora za afya na kwa karibu.

Anasema jambo la kwanza kulifanyia kazi baada ya kuchaguliwa, lilikuwa kuhakikisha wilaya hiyo inapata hospitali ya wilaya, jambo ambalo alilifanikisha kwa kiwango kikubwa nasasa in hospitali ya wilaya.

“Wananchi sasa hawafuati huduma wilayani Bariadi, hospitali yetu inafanya kazi na inatoa huduma zote, Rais Dk. Samia ametulileta Sh milioni 500 kwa ajili ya kuboresha hospitali yetu na tunaendelea na maboresho,” anasema.

Anaongeza kuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Dk. Samia ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa zahanati nane na ujenzi wa kituo kingine kimoja cha afya cha Mwanunda na kimekamilika.

Elimu

Anasema kuwa wilaya hiyo ilikuwa nyuma kielimu kutokana na mazingira, huku mwitikio wa wananchi kpeleka watoto shule ukiwa chini, ambapo kwa kushirikiana na wananchi wameweza kujenga shule mpya 16.

“Katika wlimu tunaishukuru serikali imeendelea kuboresha mazingira, tumepokea zaidi ya Sh bilioni 3 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya wanafunzi na walimu kwa kujenga madarasa na nyumba za walimu,” anaeleza Silanga.

Huduma ya maji

Chagamoto kubwa nyingine ambayo wananchi wa jimbo hilo wameteseka nayo kwa muda mrefu ni upatikanaji wa maji safi na salama, ambapo awali walipata maji kwenye madimbwi na mabwawa ya kuchimba wenyewe.

Mbunge huyo akizungumzia suala la huduma ya maji, anaeleza kuwa kwa kiwango kikubwa huduma hiyo imeboreshwa, na wananchi maeneo mengi wameanza kuonja maji safi na salama.

“Pale makao makuu yetu ya Wilaya Lagangabilili, walikuwa hawajawahi kupata maji safi na salama, lakini nilipoingia nilihakikisha tunapata mradi mkubwa wa maji, na sasa wanapata maji kila siku … maji safi na salama. Katika kijiji hiki cha Ndoleleji serikali imeleta kiasi cha zaidi ya Sh milioni 192 kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu cha maji, muda siyo mrefu tutapata maji safi na salama hapa,” anasema.

Anaeeleza kuwa mbali na hilo, kuna mradi mkubwa wa kutoa maji ziwa Victoria, ambapo Jimbo lake limewekwa katika awamu ya kwanza ya mradi huo, hivyo wananchi watarajie kupata maji.

Huduma ya Umeme

Njalu anasema kuwa hadi kufikia April,i mwaka huu, vijiji vyote 102 katika jimbo hilo vitakuwa na umeme, ambapo baada ya hapo wataanza kupeleka umeme kwenye vitongoji.

“Serikali ya Mama Samia, tayari imetutengea kiasi cha Sh bilioni 14 kwa ajili ya kusambaza umeme, ambapo Mkandarasi Sengerema Company Ltd anaendelea na zoezi la kupeleka umeme katika vijiji vyote,” anasema Njalu.

Michezo

Mbunge huyo anasema kuwa suala la michezo halijaachwa nyuma, kwani tangu amechaguliwa alianzisha mashindano ya Njalu Cup, mashindano ya mpira wa miguu ambayo yamekuwa maarufu na kuleta furaha, amani na upendo baina ya wananchi wa jimbo hilo.

Hata hivyo, anasema kuwa kazi bado haijamalizika katika jimbo hilo, kwani baadhi ya maeneo bado yameendelea kuwa na changamoto, ambapo yeye na viongozi wa Wilaya wakiwemo madiwani wataendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha changamoto zote zinatatuliwa.

Anasema kuwa kuendelea kuwa Mbunge kwenye jimbo hilo, atahakikisha anawatumikia wananchi wa jimbo hilo kwa nguvu zote, ikiwa pamoja kuhakikisha anashirikiana nao katika kuleta maendeleo.

“Kazi bado haijaisha, tuliteseka sana miaka 20, lakini sasa tuna miaka 7 tumeanza kuonja matunda, kazi bado haijamalizika, mimi pamoja na viongozi wengine na madiwani, tumesema lazima tuwatumikie,/” anasema Njalu.

Njalu anawataka wananchi hao kutoa ushirikiano kwa serikali na wadau wa maendeleo, ikiwemo kupeleka watoto shule kwani kazi kubwa imefanyika ya kuboresha elimu mashuleni.

“Kwenye wilaya hii, chini yangu, chini yangu, na kwa umri wangu huu, hakuna mwananchi atateseka kama ambavyo mliteseka miaka 20 nyuma, tumejipanga kuhakikisha tunawahudumia,” amesema Njalu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles