24.8 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yataja sababu ya kuchelewa mabadiliko ya sheria ya habari

*Yasisitiza kuwa nia yake njema iko palepale kuleta mabadiliko

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Serikali imesema kutokukamilika kwa kwa baadhi ya taratibu ndiyo sababu iliyokwamisha kupeleka mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari bungeni katika Bunge la Novemba mwaka huu.

Hayo yamebainishwa Novemba 9, mwaka huu na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akizungumza na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), jijini Dodoma ambapo amesema serikali ilitarajia kupeleka mapendekeo hayo lakini haikufanya hivyo kwa kuepuka mivutani kutoka kwa wadau wa habari.

Kwenye kikao hicho na CoRI, Waziri Nape alisema serikali ipo tayari kupeleka mapendekezo ya sheria ya habari kwa watunga sheria, baada ya kikao cha wadau wa habari na serikali kitakachofanyika Novemba 22, 2022, jijini Dar es Salaam.

‘‘Serikali tupo tayari kupeleka mabadiliko ya sheria ya habari bungeni baada ya kikao cha mwisho. Baada ya kikao hicho tutakubaliana tuliyokubaliana na ndio yataenda,” amesema Nape.

Nape amefafanua zaidi kuwa haikuwa vyema kupeleka mapendekezo ya sheria ya habari bungeni wakati kuna maeneo wadau wa habari na serikali walikuwa hawajakubaliana.

‘‘Sisi kama serikali hatujakaa kimya, bado tupo vizuri kwenye mchakato huu. Nia ya serikali mpaka sasa bado ni njema.

‘‘Isingefaa kwenda na mabadishano bungeni. Mpaka sasa kuna maeneo ambayo bado hatujakubaliana na kikao hicho cha mwisho ndio kitatoa mwelekeo wa mapendekezo yote.
Kwenye kikao hicho Nape alisema, uhuru uliopo sasa unapaswa kutumika vizuri.

‘‘Sisi kama tupo happy (tunafuraha) na mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari unavyokwenda, lakini pamoja na yote haya, ni vizuri uhuru uliopo tukautumia vizuri,’’ alisema.

Na kwamba, pamoja na mchakato wa mabadiliko ya sheria kuwa njiani kukamilika, serikali inaangalia pia uhalisia wa mabadiliko hayo ya sheria na mazingira ya sasa.

‘‘Hata kama kuna mapitio tunayofanya, lakini lazima tuangalie uhalisia wa nchini,’’ alisema Nape.

Akizungumzia takwa la Rais Samia Suluhu Hassan la kukutana na wanahabari alilolitoa wakati wa Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD), jijini Arusha Nape alisema, wizara ipo mbioni kuandaa mazingira ya Rais Samia kukutana na wanahabari hao.

‘‘Katika Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani Rais aliagiza wizara kutaka kukutana na wanahabari. Tunafanyia kazi hilo,’’ alisema Nape.

Gerson Msigwa, Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), alishauri wanahabari kubaki Pamoja kwenye mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari.

‘‘Tutumie vizuri kipindi hiki ambacho serikali imekuwa tayari kusikiliza. Tubaki Pamoja mpaka mwisho,’’alisema Msigwa.

Upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF), Deodatus Balile ameomba wadau wa habari kushiriki vema katika kikao cha mwisho cha serikali na wadau wa habari kwa kuwa ni muhimu.

‘‘Kama kuna mtu anawazo, alilete kupitia umoja wa haki ya kupata habari ili kwenye kikao hicho tuwe na lugha moja,’’ amesema Balile.

Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dk. Rose Reuben alisema, wadau wa habari wanapaswa kutoa mawazo yao ili ifike mahali wakubaliane katika utungaji wa sheria.

‘‘Tunapaswa kutoa mawazo yetu lakini ili tufike mahali ambapo tunaweza kukubaliani ili kuufanya huu mchakato wa mabadiliko ya sheria uende haraka. Sheria itakapoanza kufanya kazi, tutaanza kuona mabadiliko katika uandishi wa habari ambao ni wakitaaluma,’’ alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), Wakili James Marenga alisema katika kikao cha pili, hakuna jambo litalobaki bila kushughulikiwa.

‘‘Baada ya kikao cha pili kama ambavyo imeelezwa na serikali, tunaamini mabadiliko yatakayopelekwa bungeni yatakidhi matakwa ya wanahabari kwa ajili ya kunufaishi wananchi, serikali na tasnia kwa ujumla,’’ alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles