Serikali yapata wabobezi wa kuisuka Dodoma

0
577
waziri-mkuu-kassim-majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa

 

Na SARAH MOSES, DODOMA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Serikali imeunda timu ya wataalamu watakaotoa ushauri wa kuhamia mkoani Dodoma.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana wakati akizungumza na watumishi wa Serikali wa Mkoa wa Dodoma, wazee wa mkoa huo, wafanyabiashara na viongozi mbalimbali katika ukumbi wa Mikutano wa Dodoma (Dodoma Convention Centre).

“Tumeunda timu ya watu 10 ambao ni wataalamu waliobobea katika masuala ya ujenzi wa miji mikuu, hawa wana uzoefu wa kuangalia makao makuu ya nchi yanafananaje. Watakuja Dodoma, wapitie master plan na kisha watapita katika maeneo kadhaa ya mji ili waone hali halisi ikoje ndipo watupe maoni yao.

“Tunataka tusirudie kosa la Dar es Salaam la kulazimika kubomoa makazi ya watu kila inapolazimu kufanya uboreshaji wa miundombinu. Hawa watu watatuambia wapi tunatakiwa tuweke njia nne au sita za magari, wapi tuweke bustani au wapi tujenge nyumba za ghorofa moja, mbili, tatu au zaidi,” alisema Majaliwa.

Kuhusu miundombinu, alisema timu hiyo pia itatakiwa kutoa ushauri juu ya wapi ijengwe njia ya malori tu au mahali gani zinahitajika kujengwa barabara za juu ili kuepusha msongamano katikati ya Dodoma.

Bila kutaja majina ya wajumbe wa timu hiyo, alisema timu hiyo itaongezewa wataalamu kutoka China na Malaysia ambao nchi zao tayari zina uzoefu wa kuhamisha makao makuu ya nchi zao zaidi ya mara moja.

Alitumia fursa hiyo kuwaeleza watumishi juu ya uwepo wa Tume ya Kuboresha Masilahi ya Wafanyakazi ambayo imekuwa ikifanya kazi tangu mwaka jana. “Kuna vikao vimekuwa vinafanyika tangu mwaka jana baina ya Serikali na viongozi wa vyama vya wafanyakazi kwa lengo la kujadili uboreshaji wa masilahi ya wafanyakazi na jambo hili linaendelea vizuri,” alisema Majaliwa.

Kuhusu madeni ya watumishi wa umma, aliwasihi watumishi wawe na imani na Serikali yao kuhusu madeni hayo na kwamba ikimaliza uhakiki unaofanyika hivi sasa, kila mwenye stahiki zake atalipwa.

Katika hatua nyingine, aliutaka uongozi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), ihakikishe inakamilisha upimaji wa viwanja 100,000 kama ilivyojipangia ili watumishi hao na wananchi waweze kupatiwa viwanja haraka iwezekanavyo.

“Nimearifiwa kuwa mna mpango wa kupima viwanja 100,000 kwa ajili ya kuwapatia wananchi na watumishi,” alisema Majaliwa na kuongeza:

“Kamilisheni utaratibu huo haraka ili watumishi wapewe viwanja na waweze kujenga nyumba zao za kuishi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here