29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 1, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaitaka OSHA kuwafikia wachimbaji wadogo wa madini

MWANDISHI WETU, GEITA

SERIKALI imeuagiza Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuandaa na kutekeleza programu maalumu ya mafunzo ya Usalama na Afya kwa wachimbaji wadogo katika mikoa yote nchini yenye shughuli za uchimbaji madini.

Agizo hilo lilitolewa jana Septemba 26, na Waziri wa Madini, Doto Biteko, alipotembelea banda la OSHA katika maonesho ya tatu ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika mkoani Geita.

Waziri Biteko alieleza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kupunguza ajali na magonjwa yatokanayo na kazi katika sekta hiyo muhimu katika uchumi wa nchi.

“Serikali inataka kuona wachimbaji hawa wadogo ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wafanye shughuli zao lakini wakiwa na elimu.

“Hivyo, niwatake OSHA muandae programu ambayo itatoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini kwenye mikoa yote yenye madini nchi nzima.

“Lakini pia nimeridhishwa na mafunzo ya usalama na afya kazini ambayo OSHA mmekuwa mkiyatoa kwa baadhi ya makundi ya wachimbaji wadogo niseme tu kwamba Wizara yangu itaendelea kuwapa ushirikiano,” amesema Biteko.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel, amewataka wadau wa sekta ya madini na sekta nyingine za kiuchumi katika mkoa wake kuzingatia misingi ya usalama na afya katika shughuli zao za uzalishaji.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema baada ya maonesho hayo, taasisi yake itaandaa mpango mahsusi wa kutoa mafunzo hayo ya usalama na afya kwa wachimbaji wadogo katika mikoa yote yenye shughuli za uchimbaji madini nchini.

“Tumepokea maelekezo ya serikali ya kuhakikisha kuwa tunatoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo katika mikoa yote yenye madini nchini nasi tutalitekeleza hilo, kwani lengo la OSHA nikuona elimu inafika katika kada zote za wafanyakazi,” amesema Khadija.

Baadhi ya wadau waliotembelea maonesho akiwemo, John Samweli, wameeleza kufurahishwa kwao na mafunzo ambayo wameyapata kutoka OSHA wakati wa maonesho hayo ya tatu ya Teknolojia ya Madini.

OSHA ni taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu yenye wajibu wa kulinda nguvu kazi ya nchi kupitia kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles