26.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

Serikali Lebanon yashindikana

BEIRUT, LEBANON

WAZIRI Mkuu mteule wa Lebanon Mustapha Adib ameachia ngazi baada ya kushindwa kuunda serikali isiyoegemea upande wowote kisiasa kwa karibu mwezi mzima. Hilo ni pigo kwa mpango wa Ufaransa wa kuumaliza mzozo wa nchi hiyo.

Adib ambaye awali alikuwa balozi wa Lebanon nchini Ujerumani aliteuliwa kuwa waziri mkuu Agosti 31, na kutwishwa jukumu la kuunda serikali baada ya uingiliaji kati wa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Serikali hiyo ingefuata mpango uliopendekezwa na Ufaransa kwa ajili ya kuiondoa Lebanon katika mkwamo wa kisiasa, kwa kupiga vita ubadhirifu na kutekeleza mageuzi ambayo yangevutia msaada wa kimataifa wenye thamani ya mabilioni ya dola, ili kuunusuru uchumi wa Lebanon unaokabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni.

Hali mbaya ya uchumi wa Lebanon ilizidi makali baada ya mripuko mkubwa kwenye bandari ya Beirut wa Agosti 4, 2020, ambao uliharibu kabisa sehemu kubwa ya mji huo mkuu.

Adib ambaye ni Muislamu wa madhehebu ya Sunni kulingana na mfumo wa ugawaji wa madaraka nchini Lebanon, amesema kuondoka kwake hakupaswi kuwa sababu ya kuupa kisogo mpango wa Ufaransa, wala kupuuza nia njema ya Rais Emmanuel Macron.

”Nasisitiza kuwa mpango huu unapaswa kuendelea”, amesema Adib baada ya mazungumzo na rais wa Lebanon, Michel Aoun, na kumtakia kila la heri mtu atakayemrithi, katika ”jukumu pevu” la kuunda serikali.

Mustapha Adib alikuwa akinuia kuunda serikali ya wataalamu katika taifa lake ambalo mfumo wake wa kugawana madaraka unazingatia misingi ya kimadhehebu, kati ya Wakristu na Waislamu wa Kisuni na wa Kishia.

Wanasiasa wa Lebanon walikuwa wameiahidi Ufaransa kuwa wangeipata serikali ya namna hiyo ifikapo katikati ya mwezi wa Septemba. 

Hata hivyo juhudi za Adib zimekumbwa na pingamizi katika kuwateuwa mawaziri, hasa katika kujaza nafasi ya waziri wa fedha, ambaye angekuwa na jukumu la kutunga sera ya kuufufua uchumi wa nchi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alijitolea kujaribu kutafuta suluhisho kwa ajili ya Lebanon

Mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika baina ya Lebanon na Shirika la Fedha Ulimwenguni, IMF kuhusu fungu la uokozi wa uchumi wa nchi hiyo yalisambaratika mwanzoni mwa mwaka huu, na jukumu la kwanza la baraza jipya la mawaziri lingekuwa kuyafufua mazungumzo hayo.

Kizingiti kikubwa katika mchakato wa kuunda baraza jipya la mawaziri kilitokana na msisitizo kutoka makundi mawili ya kishia, Amal na Hezbollah, kwamba waziri wa fedha lazima atoke makundi hayo kama ilivyokuwa siku za nyuma.

Hakukuwepo tamko la mara moja kutoka Ufaransa kuhusiana na kuondoka kwa Waziri Mkuu Mteule Mustapha Adib, na baadhi ya vyanzo vya kisiasa nchini Lebanon vinasema mengi sasa yatategemea msimamo wa Ufaransa, ikiwa itakata tamaa na kujiengua au la.

Waziri mkuu wa zamani wa Lebanon, Msuni Saad al-Hariri, amesema yeyote anayeshangilia kushindwa kwa mpango wa Ufaransa, atakuja kujuta baadaye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,734FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles