23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

‘Serikali ikiwa na malalamiko, nayo ishitaki’

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

WADAU wa habari nchini, wameeleza kwamba, uundwaji wa Bodi ya Idhibati ya Habari huru, utaweka mazingira ya usawa kati ya Serikali na vyombo vya habari nchini.

Wameeleza kuwa, iwapo bodi hiyo ya kitaaluma haitaingizwa mkono wa Serikali katika uundwaji wake, serikali itapata sehemu ya kwenda kupeleka malalamiko yake pale itakapokwazwa na habari ama mwanahabari.

Nivile Meena, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Katibu Mstaafu wa taasisi hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari leo hii jijini Dar es Salaam, wahariri hao wameeleza kwamba kuundwa kwa chombo hicho, kutakuwa mwarobaini wa malalamiko ya muda mrefu kutoka kwenye vyumba vya habari mbalimbali nchini.

Nivile Meena, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Katibu Mstaafu wa taasisi hiyo amesema, iwapo serikali itaamua kuunda Bodi ya Ithibati ya Habari, basi bodi hiyo itakosa uhuru wa kufanya uamuzi pale malalamiko yatakapoihusu yenyewe (serikali).

Amesema, ili kukwepa hilo na kutenda haki kwa vyombo vyote vya habari nchini, hakuna budi kwa Bodi ya Ithibati ya Habari kuundwa na kusimamiwa na wanataaluma wenyewe ambao ndio wanahabari.

“Bodi ya Ithibati ya Habari ikisimamiwa na serikali, itakosa uhuru wa kuamua. Hiyo, bodi inapaswa kuundwa na Wanataaluma na kazi yake ni ya kitaaluma. Serikali ikiwa na malalamiko nayo inakwenda kulalamika kwenye bodi na wala haipaswi kutoa maelekezo,” ameeleza Meena.

Joseph Kulangwa, Mhariri wa Gazeti la Raia Mwema ameonesha wasiwasi iwapo serikali itasimamia uundwaji wa bodi hiyo akisema “serikali itataka wanaowaandika vizuri tu, ndio wahalalishwe kufanya kazi hiyo.”

Amesema, tasnia mbalimbali nchini zimeunda na kusimamia bodi zao wenyewe bila maelekezo ama kuingiliwa na serikali, amehoji sababu za serikali kupendekeza kuunda bodi hiyo badala ya kuwaacha wanataaluma wa habari kuunda na kusimamia bodi hiyo.

“Tasnia inatakiwa kujidhibiti yenyewe kama wanavyofanya wanasheria na wengine. Serikali ikiwa ndiye mdhibiti wa bodi hiyo, kutakuwa na upendeleo kwa magazeti so called (yanayoitwa) ya umma,” amesema Kulangwa.

Jimmy Charles, Mhariri wa Jarida la Tz & Beyond pia PANAROMA amesema, iwapo serikali itaunda bodi hiyo, itajihakikishia uhuru wa Habari kutuama mikononi mwake.

“Serikali ikiundwa bodii kama inavyoelekezwa na sheria, basi uhuru wa habari utaendelea kutuama kwenye mikononi yake (serikali).

“Ikumbukwe kuwa, kwa sasa serikali ndio mwamuzi wa mwisho kwa maana ya kuwa ndio mlalamikaji, msikilizaji na hakimu kwa wakati mmoja. Na ukitaka kujua hilo, utaona pale tu utakapogusa kile isichopendezwa nacho (serikali).

Jimmy Charles(kushoto), Mhariri wa Jarida la Tz & Beyond pia PANAROMA.

Jimmy amesisitiza kuwa: “Tasnia ya Habari inahitaji bodi huru isiyosimamiwa na Serikali,”.

Mei 31, 2021, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa (kabla tasnia ya Habari kuhamishiwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Tasnia ya Habari) alisema, serikali inaendelea na taratibu za kuanzisha Bodi ya Ithibati itayokuwa na jukumu la kutoa ithibati na vitambulisho kwa wanahabari wenye sifa.

Bashungwa alitoa kauli hiyo wakati akiwasilisha makadiro ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Alisema, Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, inaelekeza kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati, Baraza Huru la Habari pamoja na mfuko wa mafunzo kwa wanahabari.

“Kwa sasa wizara inaendelea na taratibu za kuanzisha bodi hii,” alisema na kuongeza Baraza Huru la Habari litaundwa baada ya Bodi ya Ithibati kuanza kazi.”

Kwa upande wa Jaji Eliezer Feleshi ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), alisema ni vizuri kwa Bodi ya Ithibati ya Habari ikaundwa na kusimamiwa na wanahabari wenyewe.
Jaji Feleshi alitoa maoni hayo Mei 13, 2022 wakati alipokutana na wadau wa Habari ofisini kwake bungeni, jijini Dodoma.

Jaji Eliezer Feleshi,

Wadau hao waliongozwa na Deodatus Balile, Mwenyekiti wa TEF na James Marenga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa MISA – TAN, ambapo walimkabidhi Jaji Feleshi mapendekezo ya mabadiliko ya sheria zinazominya uhuru wa vyombo vya habari nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles