23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI: HAKUNA UHABA WA CHAKULA

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu tathmini ya upatikanaji wa chakula nchini. Kushoto ni Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mathew Mtigimwe
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu tathmini ya upatikanaji wa chakula nchini. Kushoto ni Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mathew Mtigimwe

Na waandishi wetu – dar/dodoma


 

SIKU chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kusema hakuna uhaba wa chakula nchini, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, amepigilia msumari wa mwisho hoja hiyo baada ya kusema Serikali imefanya tathimini nchi nzima na kubaini hakuna uhaba wa chakula.

Pamoja na kauli hiyo, alisema wamebaini kuwapo kwa halmashauri za wilaya 43 ambazo hakuzitaja, zilizovuna chakula chini ya kiwango msimu uliopita.

Dk. Tizeba akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alisema Serikali ina mfumo wa kutathimini hali ya chakula na upatikanaji wake kila eneo nchini.

Alisema watu wanaoeneza taarifa za kuwapo kwa njaa  wana lengo la kuingiza mahindi yasiyo na ubora ili wafanye biashara.

“Serikali inao mfumo wa kutathimini hali ya chakula eneo kwa eneo, mkoa kwa mkoa, wilaya kwa wilaya. Serikali mamlaka yake ipo hadi ngazi ya vitongoji na kwamba tumebaini kwamba hali ya chakula si mbaya.

“Taarifa yetu ya awali ilionyesha kuwa Halmashauri za wilaya 43 zilikuwa zimevuna kwa upungufu na hawakuwa na ziada, lakini maeneo yaliyobaki yalikuwa na mavuno mazuri na kwa ujumla tulikuwa tumevuna na ziada tani zaidi ya milioni tatu.

“Hata ninyi ni mashahidi kwamba chakula kilikuwa kingi na uwezo wa wananchi kutunza chakula ulikuwa mdogo, baadaye wabunge wakapiga kelele kwamba wauze nje ya nchi ili wapate bei nzuri.

“Lakini sisi tulikuwa tunaendana nayo kwa uangalifu sana kwa sababu tulikuwa tuna takwimu zinazoonyesha upatikanaji wa chakula katika nchi zinazotuzunguka ulikuwa chini na zilikuwa zinatarajia kupata chakula kutoka Tanzania. Nchi hizo ukiacha Zambia ni Kenya, Burundi, Kongo, Rwanda, Ethiopia, Msumbiji, Sudan Kusini, Malawi.

“Sasa tujiulize nchi hizo ambazo zina uhaba wa chakula hazikutangaza hatari ya njaa, sasa inakuwaje Tanzania ambayo ilikuwa na mavuno mazuri itangaze?

“Kutokana hilo hatuna mpango wa kugawa chakula bure kwa sababu hakuna uhaba wa chakula,” alisema.

Alisema jambo ambalo linajitokeza hivi sasa ni kupanda kwa bei ya mahindi kuliko miaka mingine.

Dk. Tizeba alisema pamoja na bei hiyo ya mahindi kupanda, lakini kwa upande mwingine bei ya mchele imeshuka na kwamba ipo mikoa ambayo hawajui wapi watauza.

“Mfano mwaka jana gunia la mahindi wastani wake ulikuwa Sh 65,000 mwaka huu ni 85,000 hili ndilo linalojitokeza, bado watu wana akiba ya chakula, tumezunguka nchi nzima, tunazo taarifa na tunafahamu ni wapi kuna upungufu,” alisema.

WAZIRI MKUU

Wakati huo huo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Tanzania hakuna tatizo la njaa na wenye mamlaka ya kutangaza ni Serikali na si mtu mwingine.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma mara baada ya uzinduzi wa safari ya ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, Majaliwa alisema: “Tanzania haina tatizo la chakula, kelele zinazopigwa na baadhi ya vyombo vya habari na taarifa zinazotolewa si sahihi, Serikali ndiyo yenye mamlaka ya kutangaza hali ya chakula na kwa maana hiyo basi bado tuna chakula cha kutosha.” Alisema Serikali itaanza kusambaza kiasi cha tani milioni 1.5 za chakula zilizobaki msimu uliopita katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ili kupunguza kasi ya ongezeko la bei ya vyakula nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles