25.8 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali: Dira 2050 kushirikisha makundi yote ya jamii

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Serikali imeeleza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 imezingatia ushirikishwaji wa makundi yote ya jamii kwa lengo la kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kushiriki kwa kutoa maoni yake katika kuandaa mipango ya nchi kwa miaka 25 ijayo.

Hayo yamebainishwa leo Desemba 12, 2023 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo kupitia mjadala wa kitaifa unaozungumzia miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara na Mkutano wa Kwanza wa Kitaifa wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, mjadala ulioendeshwa kwa njia ya mtandao na kurushwa mbashara kupitia kituo cha televisheni cha EATV pamoja na  mitandao mbalimbali ya kijamii.

“Tarehe 9 Desemba tumefanya Mkutano wa Dira ambao tulihakikisha makundi yote ya jamii yanaalikwa na kuhudhuria mkutano ule, vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa hapa nchini vilialikwa na kushiriki kama ambavyo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekua akisisitiza kila Mtanzania kushiriki”, amesema Prof. Mkumbo.

Amefafanua kuwa Timu ya Uandishi wa Dira ni ya kitaalamu inayohusisha makundi yote na inatazamiwa kuibua vipaumbele, sambamba na kuzingatia maeneo muhimu mfano maadili ambayo Mhe. Rais Samia ameelekeza yazingatiwe katika Dira 2050.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk. Tausi Kida amesema kuwa Mkutano wa Kwanza wa Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 utakusanya maoni ya kila Mtanzania na hivyo ushiriki wa Watanzania ni  muhimu katika  machakato huo.

“Katika zoezi la kukusanya maoni kutakuwa na ushirikishwaji wa kina wa makundi mbalimbali na katika ngazi mbalimbali za kitaifa. Cha muhimu hapa ni Watanzania kutoa maoni ya Tanzania wanayoitaka,” ameeleza Dk. Kida.

Aidha, Dk. Kida ameongeza kuwa: “Kama nchi tunatakiwa kuwa na malengo, mfano katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na  Jumuiya ya Afrika Mashariki  (EAC)  kuna  malengo  na kuna ajenda nyingine za kidunia mfano 2030 na sisi kama nchi tuangalie Dira yetu na hii ajenda yetu lazima tuifungamanishe kwa kuangalia ngazi za kikanda na kimataifa,” amesema.

Naye, Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru amesema kuwa Timu ya Uandishi wa Dira itakuwa na kazi ya kuchakata maoni yatakayotolewa na kila Mtanzania kwa lengo la kutengeneza Dira ya Taifa ya Maendeleo. Sambamba na kutaja njia zitakazotumika kutoa maoni kuwa ni majadiliano, mahojiano, makongamano, mijadala ya kitaalamu katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

“Kinachotengenezwa ni Dira kwa miaka 25 ijayo, tutumie fursa hii kutoa maoni yetu, kwa njia ya simu kwa kutuma ujumbe wa maandishi na tovuti. Napenda kusisitiza hatutengenezi jarida ni Dira ambayo lazima tushirikiane kufanyakazi kwa pamoja kuitekeleza katika maeneo yote mfano huduma, uzalishaji na ufundi,” amesema Mafuru.

Mjadala wa Kitaifa unaozungumzia miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara na Mkutano wa Kwanza wa Kitaifa wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, umehudhuriwa  na kuchangiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Saada Mkuya, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mahmoud, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, Mhe. Joseph Selasin na Mwenyekiti wa Baraza la Diaspora Duniani, Norman Jasson.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles