Selasini alalamikia kutengwa na wenzake Chadema

0
865
MBUNGE wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema)

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MBUNGE wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), amedai kwamba ametengwa na wabunge wenzake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na viongozi wa juu wa chama hicho.

Amesema hata nafasi ya kuchangia asingeipata kama meza ya Spika isingempa nafasi ya kuchangia.

Kauli hiyo aliitoa jana bungeni wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2020/21.

Alidai kuwa ametengwa na viongozi wa juu na wabunge wenzake wa Chadema na hata kuchangia ilibidi apeleke maombi kwa Katibu wa Bunge, Steven Kagaigai.

Alisema anachangia mjadala wa bajeti ya wizara hiyo akiwa ametengwa na familia ya wabunge wa Chadema.

“Hii ni mara yangu ya kwanza katika Bunge hili kuchangia tangu bajeti zianze kujadiliwa, pia namshukuru Katibu wa Bunge, Mheshimiwa Kagaigai kwa kuwakilisha ombi langu mbele yako.

“Leo (jana) natoa mchango wangu nikiwa nimetengwa na familia ya kisiasa na familia ya group la WhatsApp la wabunge wa chama changu, ambapo pia wapo viongozi wakuu wa chama changu bila ya kupewa taarifa ya kukemewa au hatua hiyo iliyochukuliwa,” alisema Selasini. 

Alisema nafasi ya kuchangia asingeipata kama Katibu wa Bunge asingepeleka kilio chake kwa Spika.

“Mheshimiwa Spika ni dhahiri kwamba  nafasi hii nisingeipata bila kupitia meza yako na bila kufikishwa kwako na Katibu wa Bunge,” alisema Selasini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here