Na MWANDISHI WETU -MWANZA
KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL), imezindua bia mpya inayojulikana kama Pilsner King ambayo ni mwendelezo wa bia ya Pilsner Lager iliyozoeleka na ambayo ipo sokoni kwa kipindi kirefu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bia hiyo jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Masoko wa SBL, Cesear Mloka, alisema bia hiyo mpya ni kama bia imara ambayo itakuwa kipenzi cha wanaume jasiri na wanaojiamini.
Bia ya Pilsner King ina kilevi cha asilimia 7.6 na ndiyo bia imara kuliko zote zinazozalishwa hapa nchini.
“Pilsner King imetengenezwa na mzalishaji bia wa Kitanzania kwa kanuni za kimataifa akitumia malighafi za hapa nchini zenye ubora wa hali ya juu ambazo zimeipa bia hiyo ladha murua. “Hii ni kama zawadi kwa wanaume wa kweli baada ya shughuli nyingi za mchana kutwa,” alisema Mloka.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, bia ya Pilsner imepata jina lake kutoka katika Mji wa Pilsen uliopo Jamuhuri ya Czech ambako bia hiyo ilitengenezwa kwa mara ya kwanza na kuongeza kuwa, bia hiyo ya kipekee na yenye ladha ya aina yake itakuwa ni chaguo sahihi kwa wateja wanaopenda kuwa ‘wanaume wa kweli’.
“Ikiwa na kilevi cha asilimia 7.6 Alc, Pilsner King ambayo kaulimbiu yake ni ‘Kutana na Mfalme, kwa ajili ya Wanaume Imara na Wenye Ujasiri’, imetengenezwa kwa kuzingatia kanuni halisi za utengezaji wa bia ya kwanza ya Pilsner iliyotengenezwa huko Ulaya Mashariki,” alisema Mloka.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela ambaye alisifu kazi kubwa inayofanywa na Kampuni ya SBL kwa kuonyesha njia katika ubunifu wa vinywaji vyenye kileo hapa nchini.
“Napenda kuchukua fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa niaba ya wananchi wa Mwanza kwa Kampuni ya SBL. Uwekezaji wao hapa Mwanza umesaidia upatikanaji wa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja pamoja na fursa za kibiashara kwa wakazi wa jiji hili,” alisema Mongela.
Pamoja na kiwanda cha Mwanza, SBL ina viwanda vingine viwili vya bia, kimoja kipo jijijni Dar es Salaam na kingine kipo Moshi mkoani Kilimanjaro.
SBL inazalisha bia kama vile Pilsner Lager, Tusker Lager, Tusker Lite, Kibo Gold, Guinness Stout and bia inayobeba bendera ya kampuni, Serengeti Premium ambayo imeshinda zaidi ya medali 10 za Kitaifa na Kimataifa.