Sarakasi uchaguzi wa mameya Ubungo, Kinondoni

0
665
Boniface Jacob
Boniface Jacob
Boniface Jacob

Na AGATHA CHARLES – DAR ES SALAAM

UCHAGUZI wa mameya wa manispaa za Ubungo na Kinondoni, Dar es Salaam umeibua sintofahamu kutokana na madai  ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa hawakuwa na taarifa rasmi.

Taarifa zilizosambaa jana katika mitandao mbalimbali ya kijamii, zilieleza kuwa uchaguzi huo unatarajia kufanyika leo. Lakini MTANZANIA Jumapili lilipomtafuta kwa simu mmoja wa wagombea, Boniface Jacob (Ubungo -Chadema) ili kujua alivyojipanga, alisema walipata mwaliko ambao si rasmi, hivyo hafahamu iwapo uchaguzi huo upo au haupo.

Jakob alipotakiwa kufafanua kuhusu mwaliko huo aliouita si rasmi, alisema kawaida inapaswa chama kupatiwa kwanza barua na kuelezwa idadi ya wapigakura wao ili kujua wanachama wao wanakwenda kwenye wilaya ipi.

“Uchaguzi mpaka sasa hivi hatuujui, tumepata mialiko lakini si rasmi, hadi sasa hivi hatujui wapigakura ni kina nani, hivyo siwezi kusema uchaguzi upo au haupo.

“Kawaida chama ndiyo kinapewa kwanza barua kuambiwa idadi ya wapigakura wao na wanachama ambao wanakwenda kwenye wilaya ipi. Hadi ninavyosema sasa hivi diwani mmoja mmoja anaitwa ila chama hakijui. Hadi sasa hivi hatuji ni idadi ya watu wangapi watapiga kura, kwa hiyo huwezi kusema ni uchaguzi, huenda kuna hila nyuma. Kwahiyo siwezi kusema kuna uchaguzi kesho au haupo,” alisema Jacob.

Alipoulizwa kama alipatiwa taarifa rasmi za kuwapo uchaguzi huo akiwa mmoja wa wagombea, alisema alizipata kwa kuelezwa kuwa barua yake imepelekwa ofisi ya kata juzi saa sita usiku.

“Nimeambiwa tu barua imepelekwa ofisi ya kata, ila hakuna mkurugenzi wa manispaa zote mbili anayepiga kwa viongozi wetu wa chama na ndiyo utamaduni ulivyo na ndiyo taratibu zilivyo, huwa kinaanza kikao cha vyama, kinafuata kikao cha uchaguzi. Barua tumepata jana (juzi) usiku saa sita usiku,” alisema Jacob.

Alipotafutwa kwa simu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, John Kayombo, alisema hakuwa na taarifa kuwa uchaguzi huo unafanyika leo.

“Mimi sina taarifa hiyo, ukitaka kujua mambo ya ofisi yangu uje ofisini…sifanyi kazi kwa simu,” alisema Kayombo.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli, alipotafutwa jana kwa simu ili kujua iwapo uchaguzi huo unafanyika pamoja na kutaka ufafanuzi wa malalamiko ya upinzani, alijibu kuwa upo na unafanyika leo kuanzia saa tatu.

“Ni sahihi kuna uchaguzi kesho (leo). Sikiliza, sisi tunapeleka taarifa kwa mujibu wa kanuni, halmashauri hizi zimegawanyika kwa mujibu wa sheria, na si kwamba tumeingia kwenye uchaguzi mpya labda watu wameondoka, wamemaliza muda wao wa utawala wameingia kuomba kura kwa wananchi wapate kurudi kwenye udiwani,” alisema Kagurumjuli.

Alisema halmashauri hizo zimegawanyika, lakini madiwani ni wale wale na tayari walitoka kwenye Baraza la Madiwani wakiwa wameacha maazimio ambayo utekelezaji wake utahusisha pande zote.

“Tumegawanyika halmashauri, madiwani wale wale waliogawanyika katika sehemu mbili na wakati wanagawanyika tayari walitoka kwenye full council (baraza) wakiwa wameacha maazimio , maazimio ambayo ni lazima yatekelezwe kwa pande zote mbili. Yale yanayohusu Manispaa ya Ubungo ni lazima yatekelezwe na madiwani wanaotoka hapa kwenda kule, lakini pia yale maazimio yatakayoihusu Manispaa ya Kinondoni ni lazima yatekelezwe na madiwani waliobaki huku,” alisema Kagurumjuli.

Alisema katika kutekeleza hilo, kuna sheria ambazo zinaongoza kuendesha halmashauri na kwamba mkutano maalumu wenye ajenda ya uchaguzi kwa mujibu wa kanuni unapaswa kuitishwa saa 24 kabla.

“Kwa hiyo ni vikao ambavyo ni endelevu vinavyo-oparate (vinavyofanya kazi) chini ya kanuni za uendeshaji wa halmashauri, kipengele cha pili vifungu namba tano, kanuni ya 11 na 12, ambayo inatoa mandate (kibali) cha kuita mkutano maalumu ndani ya saa 24, sasa ukiangalia jana (juzi) jioni saa 12 hadi saa 1 hadi kesho (leo) maana yake ni saa 36. Na ukichukua hadi saa tatu ambayo ndiyo uchaguzi, ni saa 39. Kwa hiyo kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji halmashauri sie bado tuko vizuri,” alisema Kagurumjuli.

Akizungumzia mwaliko wa vyama, alisema uchaguzi huo si mpya, ni endelevu na kwamba tayari waliwaandikia barua makatibu wa vyama vyote vyenye madiwani ili washiriki kama watazamaji katika uchaguzi huo.

Alisema uchaguzi huo kwa upande wa Manispaa ya Ubungo utafanyika Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya hiyo huku ule wa Kinondoni ukifanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Uchaguzi huo wa kuwapata mameya na manaibu meya wa manispaa hizo mbili ulitokana na Mkurugenzi Kagurumjuli kuvunja Baraza la Madiwani la Manispaa ya Kinondoni kisheria Septemba 16, mwaka huu baada ya serikali kuigawa manispaa hiyo kuwa mbili.

Wakati hayo yakijili Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliitishwa jana ambapo moja ya ajenda zilizozungumziwa ni uchaguzi huo wa kushitukiza.

Akizungumza na gazeti MTANZANIA Jumapili Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema kuwa kikao hicho kilikuwa cha kawaida na kilipangwa kufanyika jana na leo.

Makene alisema kikao cha leo kimesogezwa mbele na wajumbe wote wamegawanywa kufuatilia kwa ukaribu nmwenendo wa uchaguzi huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here