Samatta aandika rekodi tatu mpya

0
1048

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

NAHODHA wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta ameweka rekodi tatu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, licha ya timu yake ya KRC Genk kuzindua kampeni kwa kuchapwa mabao 6-2 na Red Bull Salzburg ya Austria.

Rekodi hizo tatu ni kuwa Mtanzania wa kwanza na kucheza na kufunga bao katika michuano na kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kufunga bao katika mchezo wake wa kwanza wa michuano hiyo.

Genk ilijikuta ikianza kwa kupokea kichapo hicho katika mchezo huo wa kundi E uliochezwa juzi  kwenye Uwanja wa Red Bull Arena  mjini Wals-Siezenheim, Austria.

Katika mchezo huo, Samatta alitupia baodakika ya 52 , huku jingine likiwekwa kimiani na Mcolombia, Jhon  Lucumi dakika ya 40.

Kabla ya Samatta kufunga bao katika michuano hiyo ya Ulaya, Kassim Manara alikuwa anashikilia rekodi ya muda mrefu ya kuwa Mtanzania pekee aliyecheza michuano ya klabu barani Ulaya, iliyokuwa ikijulikana kama Kombe la Washindi akiwa na klabu ya SK Austria Klagenfurt ambayo sasa michuano hiyo inajulikana kama Europa League.

Samatta ambaye msimu uliopita alikuwa Mtanzania wa kwanza kucheza michuano ya UEFA Europa League na kusaidia timu hiyo kutinga hatua ya 32 bora ya michuano hiyo.

Katika michuano hiyo ya Europa, Samatta alifunga mabao tisa katika michezo 12 kuanzia hatua ya kusaka tiketi ya kufuzu, hatua ya makundi na mtoano 32 bora.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26, amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu akifunga mabao matano katika michezo sita aliyoshuka dimbani katika ligi ya Ubelgiji.

Hadi sasa Samatta amefunga mabao sita katika michezo nane aliyoichezea Genk msimu huu katika mashindano yote, mabao matano kwenye ligi na bao jingine kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Samatta alikuwa katika kiwango bora msimu uliopita, akifunga mabao 35 katika michezo 51, mabao 23 kwenye ligi, mabao tisa Europa, mabao matatu kwenye michezo ya play off kusaka ubingwa wa ligi.

Mkali huyo alimaliza nafasi yapili kwenye chati ya ufungaji bora wa ligi hiyo , mabao mawili nyuma ya Hamdi Harbaoui wa Zulte Waregem aliyechukua kiatu cha ufungaji bora.

Kiwango hicho kilimfanya kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wanaokipiga katika Ligi ya nchini Ubelgiji msimu uliopita, tuzo hiyo inajulikana kwa jina maarufu la Ebony Shoe Award.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here