24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Samaki waadimika, kuongezeka 2030

MWANDISHI WETU

UVUVI ni mojawapo yasekta za uchumi inayochangia maendeleo ya nchi kwa kuuza samaki ndani na nje ya Tanzania. Hivyo, husaidia kupata fedha za kigeni kuboresha uchumi.

Maendeleo katika sekta hii si mazuri kama inavyotakiwa, hii inatokana na ukosefu wa vifaa vya kisasa vinavyotakiwa kutumika, pia kutofanyika kwa utafiti wa kutosha ili kuona na kujua maeneo yenye samaki wa kutosha. Hali hii kwa namna moja au nyingine hurudisha nyuma maendeleo ya uvuvi nchini.

Pia asilimia kubwa ya wavuvi nchini hawana elimu ya kutosha kuhusu masuala ya uvuvi, hali inayosababisha wafanye uvuvi haramu, jambo linalopoteza uhai wa samaki na viumbehai wengine wa baharini. Uvuvi huo haramu ndio sababu kuu ya kupungua kwa samaki katika bahari na maziwa nchini.

Sasa basi, ili kuboresha sekta hii, wavuvi wanapaswa kufuata njia bora zasizoharibu mazingira.

UVUVI HARAMU

Hapa nchini iliwahi kufanyika operesheni ya kutokomeza uvuvi wa kutumia mabomu katika ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi, ambao ulisababisha madhara kwa watu wengi.

Miaka minne iliyopita, uvuvi huo ulikuwa umeshamiri katika ukanda huo baada ya baadhi ya wavuvi kuamua kutumia vilipuzi baharini kinyume na taratibu ili kupata samaki wengi na kujiongezea kipato. 

Jambo ambalo wengi walikuwa hawalifahamu ni kwamba mbali na vitendo hivyo kuathiri afya na mazingira, madhara yake yameendelea kuitafuna sekta ya uvuvi na nyingine zinazotegemea mazao ya bahari kama utalii na biashara, huku baadhi ya wavuvi wakipata ulemavu.

Hata hivyo, pamoja na Serikali kudhibiti uvuvi haramu, kiwango cha upatikanaji wa samaki bado hakijaimarika kama ilivyokuwa huko nyuma, jambo linalochangia bei ya samaki kuwa juu kutokana na kuadimika sokoni na wafanyabiashara wanahaha kutafuta wateja. 

Baadhi ya wavuvi wanataja sababu ya kuhadimika kwa samaki ni uvuvi wa kutumia mabomu unaofanywa na baadhi yao.

Mmoja wa wavuvi nchini, Rahim Bakary, anasema kuwa wapo baadhi ya samaki ambao ni adimu kuwapata.  

Anataja samaki aina ya Bunusi ambao hupenda kukaa sehemu iliyotulia kwamba hukimbia pindi wavuvi wanapovua kwa kutumia mabomu.

Bakary ambaye anajishughulisha na shughuli za uvuvi kwa miaka kumi sasa, anataja samaki wengine ambao huadimika unapofanyika uvuvi haramu kuwa ni jodari, change, kolekole na vibua.

Uhaba samaki umesababisha biashara ya samaki kutofanya vyema ikizingatiwa wengi wanaokaa ukanda wa Pwani hutegemea sekta hiyo kama moja ya njia ya kujiingizia kipato.

Baadhi ya wachuuzi wanasema kuwa huwalazimu kununua samaki wanaovuliwa kutoka nje ya nchi wakiwamo vibua, lengo likiwa ni kumudu mahitaji. 

Kutokana na ukosefu wa samaki uliochochewa na kuharibiwa kwa mazalia ya viumbe hao, wale wanaopatikana huuzwa kwa bei ya juu kwa jumla na rejareja.

Uhaba wa samaki si tu unawatesa wavuvi na walaji nyumbani, bali pia mama lishe ambao ili kupata faida kidogo huwalazimu kumkata samaki katika vipande vidogo tofauti na kipindi ambacho hupatikana kwa wingi.

HUTISHIA SOKO LA SAMAKI

Chama cha Uhifadhi Wanyamapori Duniani (WCS) kinaeleza kuwa uvuvi wa mabomu hutishia soko la samaki nchini, utalii wa kuogolea, pia ni hatari kwa usalama wa Taifa.

Wataalamu wa viumbe wa baharini wanaeleza kuwa uhaba wa samaki wakati mwingine huwa hauhusiani na msimu wa hali ya hewa baharini, bali matumizi ya mabomu yaliyokuwapo huko nyuma na kuathiri matumbawe ambayo ni muhimu katika kuongeza mazalia ya samaki.

Baada ya mabomu kupigwa, matumbawe hayo huharibika na baadhi ya viumbe bahari ambao husalimika katika kadhia hiyo kama samaki hulikimbia eneo hilo na kwenda mbali zaidi ambapo si rahisi kwa mvuvi mwenye vifaa duni kuwavua. 

Viumbe vingi vya baharini hutegemea matumbawe kwa sababu wanapata chakula na hifadhi. Pia, ‘mangrove’ (miombo) ambayo ni chakula kwa samaki huweza kuharibika kwa sababu ya mabomu yanayopigwa.

Ili matumbawe hayo kurudi katika hali yake ya kawaida na kuzalisha samaki kwa wingi, huchukua muda mrefu na kuacha wavuvi wakilia na ukame na walaji wa samaki wakihaha kupata kitoweo hicho katika afya ya mwanadamu.

Wavuvi wanasema uvuvi wa mabomu huwa unapunguza kasi ya watalii ambao hupenda kupiga mbizi baharini ili kuangalia viumbe baharini.

Aidha, tafiti zinaonesha kwamba mwamba wa matumbawe, ambao samaki hupenda kuwapo kwa sababu ya chakula na mazalia, huchukua takriban miaka 100 ili kufikia urefu wa nchi moja.

Sasa basi, yakiharibika madhara yake huwa ni makubwa mno.  Kwa hiyo, kurudishia yale maeneo ambayo yamepigwa na mabomu katika hali yake ya awali huchukua muda mrefu.

Wataalamu wanasema wakati mwingine huwa ni kama haiwezekani na hasa kama ni maeneo yenye miamba ya matumbawe.

Mmoja wa wavuvi wa Kigamboni, ambaye hakutaka kutaja jina lake gazetini, anasema uvuvi wa mabomu umepunguza kasi ya watalii waliokuwa wakitembelea Kigamboni na kupiga mbizi ili kuangalia viumbe baharini.

“Zamani walikuwa wanakuja watalii wengi hapa kuja ‘kudive’ (kuzamia) kuangalia samaki chini ya bahari lakini walifukuzwa na mabomu. Watalii wengi wamesitisha kwa kweli si kama zamani,” anasema. 

Mbali na kuathiri viumbe bahari na mazingira, mabomu yanayotumika kuvulia yameathiri hadi wavuvi wenyewe na wengine kufariki.

SAMAKI HUPOTEA

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema theluthi ya bahari duniani inakakabiliwa na athari za uvuvi uliopitiliza, huku mahitaji ya samaki yakisalia kuwa juu wakati wote.

Hali hiyo husababisha kutoweka kwa samaki, ambao ni chanzo kikubwa cha protini kwa mamilioni ya binadamu duniani kote. 

Ripoti hiyo iliyochapishwa Julai mwaka jana na shirika na Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Chakula (FAO), ilisema uvuvi huo ni mbaya hususani katika mataifa yanayoendelea, ambako idadi kubwa ya watu tayari wanapambana kuhakikisha wanapata chakula cha kutosha chenye virutubisho.

Mkurugenzi wa kitengo kinachojihusisha na uvuvi na ufugaji wa samaki kwenye shirika hilo, Manuel Barange, alisema kuna shinikizo kubwa linalokabili rasilimali za bahari, na hivyo kuna haja kubwa pia kwa serikali kujitoa kuboresha mazingira ya uvuvi kwenye nchi zao.  

Katika ripoti hiyo, ilisema kuna wasiwasi katika siku za usoni, Afrika itaanza kuingiza samaki kutoka nje, na kwamba upungufu wa samaki huenda ukasababisha bidhaa hiyo kupanda bei, na hivyo kuathiri zaidi watu masikini.

Aidha, Afrika ilikuwa na uwezo mkubwa katika eneo la ufugaji wa samaki, lakini ilihitaji kusaidiwa kifedha, malisho na usambazaji wa samaki hao.

Ripoti hiyo ilisema sekta hiyo ya ufugaji wa samaki ambayo umeendelea kukua kwa haraka zaidi katika kipindi cha miaka 40, kwa kiasi kikubwa imewezesha upatikanaji zaidi wa samaki.

WAADIMIKA KIGOMA

Takwimu zinaonesha kuwa uvuvi huwanufaisha zaidi ya watu milioni nne hapa nchini, huku wakazi wa Mkoa wa Kigoma wakiutegemea zaidi katika kuendesha maisha yao.

Hivi sasa hali ni mbaya mkoani humo kutokana na uhaba wa samaki katika Ziwa Tanganyika, huku baadhi ya wavuvi wakiamini kuachwa kwa mila na desturi ni moja ya sababu inayochangia uhaba huo.

Miezi kadhaa iliyopita, wavuvi walikuwa wakipata zaidi ya ndoo 20 za samaki, lakini kwa sasa mambo ni tofauti.

Wavuvi wengine wameamua kuachana na kazi hii na kuingia kwenye kilimo huku baadhi yao wakisema kuzipa kisogo mila na desturi kumechangia hali hiyo ziwani.

Akihojiwa na BBC, Dunia Rashid ambaye ni mvuvi katika eneo hilo anasema: “Tunaweza kuchukua mwaka mzima kuvua dagaa na samaki wakubwa.”

Anasema wazee wa kimila wanasema asiyesikia la mkuu huvunjika guu, wananyooshea vidole teknolojia kama chanzo cha vijana wengi kuachana na mila na desturi, ambazo huamini ndio njia pekee ya mafanikio.

“Machifu walikuwa wanafanya matambiko, wanaomba dua kwa MwenyeziMngu kutumia mambo ya asili, na kweli MwenyeziMngu alikuwa anatoa jibu. Mboga zilikuwa zinavulika na kupatikana,” anasema Muhsini Mmbanga.

Katika mkusanyiko ulio mfano wa kanisa ila si kanisani, mvuvi mwingine katika eneo hilo, Moshi Haruna, anawaelemisha wavuvi wenzake kuhusu kuamini kwamba mila ndio husababisha kushindwa kupata mavuno ya samaki.

“Wale wanaoendekeza mila, wanaamini kwamba bila ya mila hawawezi kupata. Ila sisi ambao hatuamini mila tunaamini, Mungu anatoa kulingana na vile anaona awalisheje binadamu.

“Kwa wa mila wanakula, na sisi ambao hatuamini mila tunakula na tunaishi,” anaeleza Haruna.

Mamlaka za serikali zinazoshughulikia uvuvi katika Ziwa Tanganyika, zinasema uhaba wa samaki kwa msimu huu si jambo la kiimani.

Ofisa wa Uvuvi Kigoma, Edimund Kajuni, aliimbia BBC kuwa: “Kwa uhalisia ni kwamba katika Ziwa Tanganyika tuna misimu mitatu ya uvuvi.

“Kuna kipindi ambacho ni msimu mbaya, ambao ndio tuliopo hivi sasa, unaoanza Mei hadi Julai.”

Imani potofu, dhana duni za uvuvi ni moja ya sababu zinazotajwa kurudisha nyuma sekta ya uvuvi nchini.

Baadhi wanaona jitihada zaidi zinahitajika kuifanya sekta hii iweze kuinufaisha jamii na kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa.

WAGEUKIA UFUGAJI WA SAMAKI

Katika wakati ambapo uvuvi baharini ukiendelea kupungua, mataifa mengi zaidi hivi sasa yanageukia sekta ya ufugaji wa samaki.

Nchini Algeria, serikali imeendelea kuwahimiza wakulima kuzalisha samaki ili kuongeza kipato na kuimarisha uzalishaji jumla wa rasilimali hiyo.

Hata hivyo, wakosoaji wanasema hatua hiyo inaweza kuchangia uharibifu wa mazingira, ingawa suluhisho la wasiwasi huo ni kuwa na kanuni mwafaka, sheria na ufuatiliaji, lakini pia udhibiti kwenye shughuli za uvuvi.

Ripoti hiyo inaonesha asilimia 33.1 ya samaki walivuliwa bila kuzingatia taratibu mwaka 2015, ikiwa imeongezeka kutoka asilimia 31.4 ya mwaka 2013, na asilimia 10 mwaka 1974.

Ulaji wa samaki nao umeendelea kuwa juu kwa kilo 20.2 kwa mtu mmoja kutoka kilo 9 za mwaka 1961, lakini kukitarajiwa ongezeko zaidi, katika wakati ambapo wengi wanachagua kula samaki kutokana na matatizo ya kiafya.

Hata hivyo, kuna haja ya kutafutwa suluhu itakayowezesha kuitengeneza mifupa ya samaki pamoja na vichwa kuwa vyakula vyenye virutubisho, kwa kuwa sehemu hizo zina virutubisho vingi, badala ya kutegemea minofu ya samaki pekee.

Lakini, upande mwingine wa ripoti hiyo ulisema, kunatarajiwa ongezeko la uzalishaji wa samaki kwa asilimia 18 ifikapo mwaka 2030 na kufikia tani milioni 201. Hata hivyo, shirika hilo la FAO lilitoa wito kwa mamlaka husika kusimamia vyema  sekta ya uvuvi, ikiwa ni pamoja na kupunguza takataka na kukabiliana na uchafuzi wa bahari na mabadiliko ya hali ya hewa, ambavyo kwa pamoja huathiri bahari na uzalishaji wa samaki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles