25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Safari ya Ikulu-CCM yaanza leo

 WAANDISHI WETU– DAR/ZANZIBAR

HEKEHEKA za kumpata mrithi wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein kuongoza Serikali ya awamu ya nane ya Mapinduzi Zanzibar na ile ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zinaanza leo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hali hiyo, inatotokana na ratiba iliyotolewa wiki iliyopita na CCM ambapo kuanzia leo wanachama wanaotaka kuwania urais wa Zanzibar na ule wa Jamhuri ya Muungano, wamefunguliwa pazia sambamba na kutakiwa kutafuta wadhamini mikoani.

Kwa upande wa urais wa Jamhuri, joto halipandi kwa kasi ndani ya chama hicho, ambapo hadi sasa Rais Dk. John Magufuli anatarajiwa kuchukua fomo ya kukamilisha kipindi chache cha pili cha uongozi licha ya CCM kuwataka na wanachama wenye sifa kujitokeza kufanya hivyo.

Hatua ya CCM kufungua pazia hilo kwa wagombea urais, ilitokana na uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu ya CCM, iliyoketi Juni 10, mwaka huu chini ya Rais Dk. John Magufuli, Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Kikao hicho hicho kiliridhishwa na kiwango cha maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba.

Mwishoni mwa wiki CCM kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole, alitangaza ratiba ya mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho tawala nchini.

Joto la kisiasa kwa upande wa Zanzibar kumekuwa likipanda na kuibuka kwa mijadala kutoka kwa watu wa kada mbalimbali ya nani atamrithi kijiti cha urais Dk. Shein.

Pamoja na hali hiyo, makada kadhaa ambao wamekuwa wakitajwa kwenye mbio hizo wao na wapambe wao wameanza kupigana vikumbo kwa kutumia upepo wa shughuli mbalimbali za kijamii na hata kiserikali katika kutafuta lkuungwa mkono kimyakimya kama hatua ya kutengeza wapigakura wao.

Baadhi ya wahafidhina walioopo CCM sasa wameibuka na hoja kadhaa ikiwamo suala la kutaka mgombea ajaye awe na sifa ya kuijua Zanzibar, ikiwamo kuzaliwa na kujua mila na utamaduni wa visiwa hivyo ambavyo utawala wake ulitokana baada ya kupinduliwa na Sultan.

Marais waliowahi kuiongoza Zanzibar ni pamoja na Sheikh Abeid Amani Karume (1964-1972), Mwinyi Aboud Jumbe (1972-1984), Ali Hassani Mwinyi (1984-1985), Idris Abdul Wakili (1985-1990), Salmin Amour (1990-2000) na Amani Abeid Karume (2000-2010)

Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, alipata wadhifa huo baada ya kutokea mapinduzi yaliyosababisha kupinduliwa kwa Sultani wa mwisho wa Sultan Jamshid bin Abdullah Januari 1964.

Licha ya hali hiyo,Rais Dk. na Makamu wake upande wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, wamekuwa na mazungumzo ya ana kwa ana hivyo kuongeza joto la siasa juu usiri ulioko bana yao kwamba ni nani hasa atakuwa mgombea wa chama hicho kumrithi Dk. Shein Oktoba maka huu.

Hilo linatokana na uamuzi wa viongozi hao wa juu wa CCM kukutana kwa nyakati tofauti ambapo inaelezwa kuwa sehemu kubwa ya mazungumzo yao ni nani atarithi viatu vya Dk. Shein na kuwa Rais wa Zanzibar wa awamu ya nane.

Licha ya hali hiyo, viongozi hao wametajwa kuwa kwenye mikakati kadhaa ya kupata mgombea atakayeshindana na vyama vingine vya upinzani ili chama hicho kikibaki salama bila mpasuko wa makundi hivyo kujihakikishia umoja ambao ni silaha muhimu kwa ushindi katika uchaguzi huo.

Mara kadhaa viongozi hao wa juu, wamekuwa wakikutana na kujadili masuala kadhaa kuhusu hatima ya CCM na majaliwa yake kuelekea Uchaguzi Mkuu, Juni 3, mwaka huu, Rais Dk. agufuli alikutana na Rais Dk. Shein katika kikao cha ndani kilichofanyika Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma

Kikao hicho kilichofanyika Ikulu Chamwino, ilielezwa kuwa kilihudhuriwa na Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bashiru Ally, kuzungumzia masuala ya chama hicho.

Majadiliano hayo yalikuwa yakihusisha viongozi hao yaligusia masuala kadhaa ikiwamo kufanyika kwa Mkutano Mkuu Maalumu ambapo utateua mgombea urais unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi ujao.

“Pia suala la uteuzi wa mgombea urais limebaki kuwa siri nzito kwa viongozi maana kwa sasa wapo ambao wamekuwa wakijihakikishia ni wao. Ingawa hata hivyo lolote linaweza kutokea.

“Tunaamini CCM kwa kuwa ni chama kiongozi nchini na Afrika kitakuja na mgombea bora ambaye atakuja kumaliza siasa za mivutano Zanzibar ikiwamo kuwaunganisha viongozi wote.

“…hata baada ya kikao cha viongozi hao pia ujue hadi kupata mgombea ni mchakato mrefu ndani ya CCM kwani baada ya wanachama kuchukua fomu … ni lazima kura zipite kwa Kamati Kuu Maalumu ya CCM Zanzibar ambayo huwa kama njia, lakini pia mapendekezo hayo yatakwenda Dodoma na kujadiliwa na Kamati Kuu na hatimaye Halmashauri Kuu,” alisema mmoja wa viongozi wa waandamizi wa CCM upande wa Zanzibar.

Hata hivyo, viongozi hao wakuu wawili wa nchi (Rais Magufuli na Shein), walikutana tena jana Juni 10, jijini Dodoma ambapo safari hii wakiwa wawili pasi na kushirikisha viongozi wengine kama ilivyokuwa kwenye kikao cha awali.

Rais Magufuli na mwenzake Shein walikutana kabla ya kufanyika kwa kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, ambako walijadili masuala kadhaa kabla ya kuingia kikaoni.

Hadi sasa yamekuwa yakitajwa makundi kadhaa ya wana CCM ikiwamo wengine kuanza mchakato wa kuendesha kura za maoni kupitia mtandao, kama njia ya ushawishi ya kujua jina la mgombea gani linakubalika kabla ya uteuzi wa mwisho wa chama.

Yapo majina ambayo yamekuwa yakitajwa licha ya CCM kuzuia makada wake wenye nia kuwania kiti hicho kujiepusha na harakati zozote za kujipitishapitisha kwa wanachama kabla ya wakati kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho.

MAKADA WANAOTAJWA 

Miongoni mwa wanaotajwa kuwania urais Zanzibar ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, Balozi Ali Karume, Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni na Waziri wa Viwanda upande wa Zanzibar, Balozi Amina Ali ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 alijitokeza kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika orodha hiyo, yumo pia aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Dk. Khalid Salum Mohamed ambaye aliondolewa kwenye wadhifa huo Machi 3, mwaka huu, baada ya kile kilichoelezwa kukaidi agizo la chama chake la kutoanza kampeni kabla ya wakati.

Mbali na hao, pia wanatajwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Abood, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Issa Haji Ussi Gavu na Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Agosti 26, mwaka jana, Samia alisema hana nia ya kuwania urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

 UBUNGE, UDIWANI UWAKILISHI

Kulingana na ratiba iliyotolewa juzi wanaotaka kugombea ubunge, uwakilishi, udiwani na viti maalumu watachukua na kurejesha fomu Julai 14 hadi 17, mwaka huu.

Wanachofanya makada wengi hivi sasa hasa wale wanaotajwa kutaka kugombea nafasi hizo ni kutafuta ushawishi au ‘kiki’ ya kuwafanya waonekane ili kujitengenezea mtaji wakati wa vikao vya ndani na nje ya CCM. 

Wengine wamekuwa wakiitumia kwa kasi mitandao ya kijamii kujipambanua kwa kueleza yale waliyotekeleza wakati wakiomba kura mwaka 2015.

Wamo pia baadhi ya wabunge wa kuteuliwa na wale wa Viti Maalumu ambao pia ni mawaziri wameonyesha dalili ya kutaka kugombea majimbo mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles