25 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

Sababu za kuchelewa mishahara EALA zatajwa


LOVENESS BERNARD-DAR ES SALAAM

UCHELEWESHAJI wa michango ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afika Mashariki (EAC), umetajwa kuwa kikwazo katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za jumuiya hiyo .

Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa Wabunge wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Dk Abdullah Makame katika mkutano na  waandishi wa habari Dar es Salaam jana.

Alisema katika mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki pamoja na mambo mengine pia walijadili suala hilo la ucheleweshaji michango na kusisitiza kuwataka wanachama wote kutimiza wajibu wao kwa wakati.

“Nchi wanachama wa jumuiya hii ni kweli wanachelewesha michango hivyo shughuli nyingi za jumuiya hii zinakwama ikiwamo ulipwaji wa mishahara. Ni Tanzania pekee ambao wanalipa kwa wakati na mwaka unapopinduka huwa hawabaki na deni” alisema DK. Makame.

Wabunge hao wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), walisema wameanza kukutana na wadau mbalimbali kuangalia utekelezaji wa itifaki za jumuiya na kutoa elimu kuhusu utengamano wa jumuiya hiyo.

Dk. Abdullah Makame alisema wamepanga kutembelea Bandari ya Dar es Salaam huku leo wakitarajia kukutana na wadau wa sekta ya usafirishaji pamoja na wanafunzi wa elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Dk. Makame alisema lengo la ziara hiyo ni kuwafahamisha wananchi kuhusu jumuiya yao na kuwahamasisha fursa mbalimbali zinazopatikana miongoni mwa nchi wanachama.

“Tunalenga kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya umma na binafsi kuangalia utekelezaji wa itifaki za jumuiya. Kimsingi tunaangalia utekelezaji wa itifaki ya umoja wa forodha na soko la pamoja,”alisema Dk Makame.

Mbunge, Fancy Nkuhi alisema Watanzania wengi hawana mwamko wa kutumia fursa zinazopatikana katika nchi nyingine, jambo linalowafanya wabaki nyuma katika maendeleo.

Kwa upande wake, Dk. Ngwaru Maghembe alisema Tanzania inasifika kwa kuwa na amani ambayo haipatikani katika nchi nyingine, huku Tanzania ikiwa haina wakimbizi katika mataifa mengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles