29.6 C
Dar es Salaam
Saturday, May 21, 2022

Rungwe na joto la kampeni

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

MGOMBEA urais wa  Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Hashim Rungwe ameahidi kuwa iwapo atachaguliwa kuwa Rais, serikali yake itafuta utaratibu wa wananchi kupeleka chakula hospitali.

Rungwe ambaye pia ni Mweyekiti wa Chama hicho aliyasema hayo jana Manzese jijini Dar es Salaam wakati akinadi sera zake kwa mamia ya wakazi waliojitokeza kwenye viwanja hivyo.

Hata hivyo wakati Rungwe ambaye aliwasili viwanjani hapo  saa 9:50 akiwa kwenye gari aina ya Range Rover Vogue lenye namba za usajili T 452 DFX pamoja na magari mengine mawili, wakati akijiandaa kuanza kumwaga sera zake ghafla jenereta lilishiwa mafuta na hivyo kulazimika kusubiri kwa dakika 5 ili kuongeza mafuta ambapo alitoa Sh 10,000.

Hata hivyo, bado pepo mbaya ziliendelea kuvuma kwa mgombea huyo kufuatia matangazo yake kukosa utulivu uliotarajiwa kwa wakati huo.

Hatua hiyo iliwalazimu mafundi mitambo wa Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC) kuingialia kati kwa kumsaidia maiki nyingine. 

Na hapo sasa safari ya kunadi sera zake ambazo anasema ni bora na zimekuwa zikiibwa na wapinzania wake, ikaanza.

Mgombea huyo ambaye siku za karibuni amepata umaarufu kwenye mitandao ya kijamii kutokana na sera yake ya kutoa wali na kuku kwenye mikutano yake ya kampeni, alianza kwa kusikitika juu ya mpango wake huo kupigwa marufuku na Taasisi ya Kuzuia na Kupamba ana Rushwa(Takukuru).

Chakula

Rungwe alisema iwapo atachaguliwa mbali na kufuta utaratibu wa kupeleka chakula kwa wagonjwa pia atahakikisha kuwa wanafunzi wanapata chakula shuleni kama ambavyo amekuwa akisisitiza na kuongeza kuwa uwezo wa kufanya hivyo upo.

“Nitahakikisha nafuta utaratibu wa wananchi kupeleka chakula hospitali, kwani ni jambo lisilowezekana wewe una mgonjwa alafu bado unahangaika kupeleka chakula, nitaondoa huu utaratibu.

“Pia shuleni wanafunzi lazima wapate ubwabwa kwani ni jambo linalowezekana, serikali inayo nguvu ya kufanya hivi kwani wakati wa utalawa wa mkoloni huduma hii ilikuwa inapatikana lakini baadaye ikatolewa kwa kisingizio cha kuongezeka kwa watu bila kujihoji kwamba ongezeko hilo lilikuwa linakwenda sambamba na kuongezeka kwa kodi.

“Hivyo hakuna ambacho kingeharibika, hivyo kwangu lazima wananchi wale ili wawe na nguvu ya kufanya kazi ikiwmao kusoma vizuri,” alisema Rungwe.

Atawezaje?

Rungwe alisema kuwa ni rahisi sana kulifanikisha suala hilo la chakula shuleni pamoja na mahospitali kutokana na kuwapo kwa mfuko wa chakula.

“Lazima tutambue kuwa serikali inao mfuko wa chakula, lakini kama hiyo haitoshi chakula hiki kitakuwa kinatoka kwa wakulima wetu ambao watakuwa wanaiuzia serikali kupitia shule hivyo tutakuwa tumetengeneza pia kipato kwa wananchi wetu.

“Kwani enzi za wakoloni na baadaye Julius Nyerere Serikali ilikuwa ikigharamia kila kitu mwanafunzi ulikuwa unaenda na madaftari tu na peni yako, hatujui kwanini utaratibu huu ulipotea, lakini sisi tutaurejesha iwapo mtatuchagua mambo haya tutayafanya ndani ya siku 20 za mwanzo,” alisema Rungwe.

Aliongeza kuwa 

ni ngumu kumpatia mgonjwa dawa bila kuwa na uhakika wa chakula.

Utawala wa Sheria

Rungwe alisema kuwa anataka kuunda serikali ambayo itazingatia utawala wa sheria ambao utazingatia masilahi ya watu ikiwamo kutoa fidia pale panapostahili.

“Tutazingatia utaratibu wa sheria, kuhakiksha kuwa wananchi wanakuwa na haki ndani ya nchi yao, hata pale unapotaka kufanya maendeleo mfano kupitisha barabara lazima uwaondoe watu kwa ustaarabu na kuwalipa fidia zao na siyo kuwatoa kama ‘manyani’,” alisema Rungwe.

Miradi kutokuendelezwa

Aidha, Rungwe alishangazwa na namna ambavyo kumekuwa na miradi mingi ambayo imeshindwa kuendelea hatua ambayo alisema kuwa serikali inapoteza kodi za bure.

“Kuna miradi mingi kama, Dege Beach kule Kigamboni, Mradi wa Morocco na mingine, lakini yote imesimama na hakuna kinachoendelea, kama kuna makosa yalifanyika si wakamateni wahusika kisha muendeleze ili wananchi wanufaike kiuchumi kuliko kuacha yakaliwe na popo, si hasara ile, kuna bandari ya Bagamoyo si hasara hiyo?.

“Kwani hizo ni kodi za wananchi ambazo zinapotea bila majibu kwa kipindi hiki cha miaka mitano, lazima tumalize vitu, ndiyo maana mimi sitaki kulipiza kisasi,” alisema Rungwe.

Bahari kwenda Dodoma(Rungwe Canal)

Aidha, katika hatua nyingine chama hicho kilisema kuwa kitajenga mrefeji wa bahari kutoka Dar es Salaama hadi Dodoma na kwamba hatua hiyo itaimarisha utalii.

“Miongoni mwa jambo tutakalolitekeleza ni pamoja na kujenga mfereji wa bahari kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma itakayofahamika kama Rungwe Canal ambapo tutaanza na kilomita 100. 

“Tunaamini kuwa hii itakuwa ni chanzo cha kuibua fursa za utalii na kutengeneza ajira kwa vijana wetu, kwani kama Misri waliweza kutengeneza sisi tutashindwaje?,” alihoji Rungwe.

Kutumia ‘mabeberu’

Alisema ni lazima wawe wakweli kwamba fedha za kutekeleza mradi huo watategemea misaada kutoka nje.

“Lazima tuseme ukweli fedha za kuanza kutengeneza mradi huu tutategemea mabeberu na lazima tuelewane kwamba hata ukisaidiwa na watu kutoka Kenya hao ni mabeberu tu,” alisema Rungwe.

Mgombea mwenza

Kwa upande wake mgombea mwenza, Mohammed Masoud, alisema iwapo wataingia madarakani watahakikisha kuwa wanajenga daraja kutoka Zanzibar hadi Bagamoyo ili kuondoa adha kwa wananchi ambao hawapendi usafiri wa majini.

Ubwabwa kupigwa marufuku

Aidha, chama hicho kilisema kuwa kinasikitishwa na uamuzi wa Takukuru kuzuia watu kula ubwabwa na kuku kwenye kampeni wakati vyama vingine vikifanya hivyo kwa kuwatumia wasanii.

“Ubwabwa utakuwa palepale ni suala la muda tu, tunaambiwa kuwa hii ni rushwa vipi kwa wale wanaotoa fedha na kuwapatia wasanii? Tumepigwa sana tuko hoi, watu wanahitaji kula wali kuku,” alisema Rungwe.

Chama hicho kinatarajia kuendelea na kampeni huku kikiomba wananchi kukiwezesha zaidi kwa kukichangia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
191,701FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles