28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

RC Simiyu aagiza kuburuzwa mahakamani kwa vikundi vilivyoshindwa kurejesha mikopo ya Halmashauri

*Ni baada ya kutoweka na zaidi ya Sh milioni 200 tangu mwaka 2013

Na Samwel Mwanga,Maswa

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahya Nawanda amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Simon Berege kuvifikisha mahakamani vikundi vyote vya Wanawake, Vijana na watu Wenyeulemavu vilivyoshindwa kurejesha mikopo kwa wakati waliopewa na Serikali.

Baadhi ya Watumishi wa Serikali na Mashirika ya Umma wilayani Maswa wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahya Nawanda (hayupo picha) katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo.(Picha Na Samwel Mwanga).

Agizo hilo amelitoa leo Agosti 16, 2022 mjini Maswa wakati akizungumza na Watumishi wa Serikali na Mashirika ya Umma katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya hiyo.

Amesema kuna vikundi vilipatiwa mikopo ya fedha kutoka serikalini ili kuviwezesha vikundi hivyo viweze kujikomboa kiuchumi lakini vimeshindwa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.

“Serikali imekuwa ikiziagiza halmashauri zote za wilaya kutoa asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuviwezesha vikundi vya makundi maalum ya Vijana, Wanawake na watu wenye ulemavu lakini wamekuwa wakishindwa kurejesha kwa wakati.

“Hizi fedha ni za serikali ni lazima zirejeshwe ili na wengine waweze kukopa, hivyo nakuagiza Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Maswa kuanzia kesho (Agosti 17) wafikishe wote mahakamani ambao hawajaresha fedha hizi za mikopo na taarifa niipate ifikapo Ijumaa Agosti 19, mwaka huu,” amesema Nawanda.

Amesema fedha hizo ni lazima zirejeshwe kwani ndiyo masharti yake nakwamba hazikutolewa kama sadaka hivyo uongozi wa wilaya hiyo uhakikishe zinapatikana ili na vikundi vingine viweze kunufaika na mikopo hiyo.

Akizungumzia agizo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Berege amesema kuwa kuanzia kesho(Agosti 17, 2022 kwa kushirikiana na Wanasheria wa halmashauri ya wilaya ya Maswa wataanza kuwafikisha mahakamani wadaiwa sugu.

Amesema kuwa kuna vikundi vipatavyo 31 hadi sasa havijaresha mikopo waliyopatiwa ya zaidi ya Sh milioni 200 na mikopo hiyo ni ile iliyotolewa kuanzia mwaka 2013.

“Sisi kuanzia kesho tunaanza kutekeleza agizo la Mkuu wa mkoa, nitashirikiana na wanasheria tulionao katika halmashauri yetu ili waweze kuandaa mashitaka na kuvifikisha vikundi vyote mahakamani ambavyo vimeshindwa kurejesha mikopo ya fedha kwa wakati.

“Tutaanza na wadaiwa wale sugu wa mwaka 2013 hawa wote kufikia kesho ni lazima tuwafikishe mahakamani kwani kwa wadaiwa wote tunadai zaidi ya Sh milioni 200 hizo ni fedha nyingi sana zinapaswa zipatikane ili na wengine tuwakopeshe,” amesema Berege.

Aidha, Berege amewasihi viongozi wa vikundi hivyo watumie muda huu kurejesha fedha hizo bila shiruti kwani wao hawatawafikisha mahakamani wote waliorejesha mikopo yao  kabla ya utekelezaji wa agizo la mkuu wa mkoa wa Simiyu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles