31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

RC Kunenge awataka wananchi bonde la mto Rufiji kuchukua tahadhari ya maji

Na Gustafu Haule, Mtanzania Digital 

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amewataka wananchi walioweka makazi na kufanya shughuli za kilimo katika bonde la mto Rufiji kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maji yanayoongezeka katika mto huo.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Machi 14, 2024 kuhusu tahadhari ya bonde la mto Rufiji kujaa maji.

Kunenge ametoa kauli hiyo Machi 14 ,mwaka huu wakati akitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa Habari kuhusu maji yaliyojaa mto Rufiji ambayo yameleta madhara kwa baadhi ya makazi na hata mazao ya wakulima wa Wilaya za Rufiji na Kibiti.

Amesema mto Rufiji umejaa maji kutokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni pamoja na maji yaliyotoka katika Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Julias Nyerere ambalo kwasasa limeanza kuzalisha megawati 235.

Kunenge amesema kutokana na mvua hizo bwawa hilo lilijaa maji kwa kina cha mita za ujazo 183.85 hivyo kufikia maamuzi ya kufungulia baadhi ya mageti ili kupunguza maji hayo ambapo hata hivyo kwasasa yamepungua na kufikia mita za ujazo 183.45.

Amesema kufunguliwa kwa mageti katika bwawa hilo kulisababisha maji kusambaa katika bonde la mto Rufiji na hivyo kuleta mafuriko ambayo yamesababisha kuwepo kwa athari kwa wananchi wanaofanya shughuli za kilimo pembezoni mwa mto huo.

Amesema kabla ya kufunguliwa kwa mageti hayo Serikali ilitoa taarifa kwa wananchi ambao wamepitiwa na bonde hilo kwa njia mbalimbali ikiwemo kutangaza katika Redio ya Rufiji FM, nyumba za ibada na hata kupitia wenyeviti wa vjiji na vitongoji.

Aidha, Kunenge amesema athari mojawapo iliyopatikana ni kuharibiwa kwa mazao baada ya kufunikwa na maji mengi lakini hatahivyo wengine walifanikiwa kuokoa mazao yao kwakuwa waliwai kuondoa mara baada ya kupewa taarifa juu ya kufunguliwa kwa maji hayo .

“Baada ya maji kujaa katika bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere ililazimika baadhi ya mageti kufunguliwa ili kupunguza maji hayo lakini kabla ya kufungua wananchi wote walipewa taarifa na wengine kuondoka na hata kuokoa mazao yao.

“Kufunguliwa kwa mageti hayo kulisababisha maji kusambaa katika mashamba na bonde la mto Rufiji kujaa na kuleta changamoto kwa wakulima ambao mazao yao yalizingirwa na maji na kuharibiwa ikiwemo mahindi, mpunga, maboga na mengine,” amesema Kunenge.

Amesema kuwa tayari vyombo vya uokoaji vimefanyakazi na sasa hali inaendelea vizuri na kusema tahadhari lazima ichukuliwe kwakuwa mvua kubwa zinaendelea kunyesha.

“Tunaendelea kutoa elimu na tahadhari kwa wananchi kuwa waondoke katika maeneo hayo ili kuepusha vifo kwakuwa mvua nyingi zinaendelea kunyesha hivyo kufanya mto Rufiji kuendelea kujaa maji,” amesema Kunenge.

Hata hivyo, Kunenge amesema kuwa kamati ya maafa inaendelea kufanya tathmini katika maeneo yote ili kuweza kujua athari iliyopatikana na kuitolea taarifa kwa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles