23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

RAMBIRAMBI MSIBA WANAFUNZI ARUSHA ZAZUA GUMZO

Na MWANDISHI WETU-ARUSHA

UTATA umeanza kuibuka kuhusu Sh milioni 215 za rambirambi zilizotolewa na zinazoendelea kutolewa kwa familia zilizofiwa ndugu katika ajali ya basi la Shule ya Lucky Vincent, iliyotokea Mei 6, mwaka huu katika eneo la Marera, Rotia Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha na kuua wanafunzi 33, walimu wawili na dereva.

Baadhi ya wananchi kupitia mitandao ya kijamii wamehoji utata huo kwa kuuliza maswali mengi kuhusu matumizi ya fedha hizo zilizolengwa kukabidhiwa wafiwa.

Wananchi hao walihoji baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, kutoa taarifa ya awali ya makusanyo ya fedha hizo zilizokwisha kupokelewa.

Akiwa katika Viwanja vya Sheikh Amri Abeid Mjini Arusha mapema wiki hii wakati wa kuaga miili ya wanafunzi hao, Gambo, aliutangazia umma uliofurika uwanjani hapo kuwa Serikali itagharamia gharama zote za mazishi ya watu hao.

Wakizungumza na MTANZANIA Jumapili jana, baadhi ya watu walidai kauli aliyoitoa Gambo uwanjani siku ya kuaga miili ya marehemu imekuwa tofauti na taarifa ya awali ya fedha za rambirambi aliyoitoa akiwa ofisini kwake juzi.

“Tumemsikiliza vizuri RC Gambo akitoa kwa kifupi mchanganuo wa matumizi ya fedha za rambirambi zilizochangwa kwa familia za wafiwa,” alisema mkazi mmoja wa Arusha aliyeomba kutotajwa jina gazetini na kuongeza:

“Nadhani akikamilisha hesabu atakuwa na majibu sahihi au taarifa kamili. Kuna maswali ya kujiuliza, uwanjani alituambia Serikali itagharamia shughuli zote bila kufafanua ni Serikali Kuu au Serikali ya Mkoa wa Arusha.

“Wadau na wafanyabiashara wa Arusha walitoa fedha na magari yao kusafirisha miili, pia yalikuwapo magari ya Serikali kwa maana ya halmashauri na mashirika ya umma.

“Spika wa Bunge, Job Ndugai, tulimuona akisisitiza kwamba shilingi milioni 100 zilizochangwa na wabunge pamoja na Ofisi ya Bunge ziwafikie walengwa, ikiwamo pia Naibu Spika Baraza la Wawakilishi na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar waliotoa shilingi milioni 10.”

Pia mkazi mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema kuwa, katika taarifa hizo za awali za matumizi ya fedha za rambirambi, hakuna mahali palipoonyesha mchango wa Serikali wa kugharamia shughuli zote kama Gambo alivyoeleza.

Akizungumza na waandishi wa habari, Gambo, alisema zaidi ya Sh milioni 190 zimetumika, ikiwamo Sh 3,850,000 zilizotolewa kwa familia 32.

Alisema gharama nyingine ni pamoja na usafiri wa magari ya kusafirisha miili hiyo kwa maziko yaliyofanyika kwenye mikoa ya Arusha, Iringa, Tanga, Mbeya na Kilimanjaro.

Kutokana na kuibuka kwa utata huo, baadhi ya watu, akiwamo Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, kupitia mitandao ya kijamii, alihoji kuwapo kwa harufu kubwa ya ufisadi na wizi katika michango iliyochangwa kwa ajili ya wafiwa.

Naye Gambo kupitia mitandao ya kijamii alionekana kujibu madai hayo, akisisitiza kuwa taarifa iliyotolewa ilikuwa ni ya awali, hivyo watatoa hesabu kamili.

“Mimi ninawekeza katika uadilifu na uwazi. Utamaduni wa kuchangisha fedha na kutoa taarifa kwa umma ni mgeni. Nimedhamiria kuonyesha njia, hizi ni fedha za umma,” ilisema taarifa yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles