29.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia aagiza Wizara, NECTA kutafuta mwarobaini udanganyifu wa mitihani

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital 

Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, amezitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Baraza la Mitihani Tanzania(NECTA), kuweka mkakati wa  kushughulikia  changamoto ya udanganyifu wa mitihani nchini ili wahitimu wafaulu kwa haki.

Maagizo hayo ameyatoa leo  Desemba 16,2023 katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya NECTA, jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa utanganyifu unasababisha kuzalisha watu wasio na tija kwa Taifa.

“Sasa kuna wahitimu mamilioni, tunapowachukua ndani ya ajira ukiwapa kazi ndogo akufanyike hawawezi, unajiuliza huyu kaja na cheti chake, katoka  chuo, kwa hiyo tunazalisha nguvu kazi ambayo haipo ‘productive’ ,haina tija kwa taifa, lazima tujitazame katika utungaji wa mitihani na usahihishaji, kubwa zaidi udhibiti wa mitihani.

Tukitoa mianya ya watoto wetu kufanya mitihani kwa kuijua kabla tutatoa ‘product’ isiyokuwa nzuri, tuzingatie hilo ili tutoe nguvu kazi nzuri itakayotumika vyema katika maeneo mbalimbali,”amesema.

Pia ameiagiza Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ili kufunga mtandao katika vijiji  vyenye umeme kuwawezesha wanafunzi waliopo pembezoni  kujifunza na kufanya mitihani ya masomo ya sayansi kwa njia ya mtandao.

Rais  Dk.Samia amesema serikali itaendelea kupeleka umeme  katika maeneo mbalimbali hasa vijijini kuwawezesha wanafunzi wa sayansi wasiokuwa na walimu wa kutosha kusoma kwa kutumia teknolojia.

“Kutokana na watahiniwa wote kutahiniwa sawa bila  kujali mazingira na changamoto yoyote, serikali itaendelea  kupeleka umeme katika maeneo mbalimbali hasa vijijini kuwawezesha wanafunzi  hasa wa sayansi  ambao hawana walimu wa kutosha ,wasome kwa  kutumia  mfumo wa kimtandao unaotekelezwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF),” amesema.

Amesema  mfumo huo umekuwa na matokeo chanya  kutokana na wanafunzi wanaoutumia kufanya vizuri katika masomo yao.

Rais Dk. Samia amesema mfumo huo umesaidia  kupunguza gharama ya kununua vifaa vya maabara kwa wizara kwani mwanafunzi anaviona katika mtandao na anaweza kufanya mtihani au kusoma  kwa mtandao.

Amesema serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika Tehama  ambao umeimarisha utendaji wa  Baraza  hasa katika matumizi ya teknoliojia  katika usajili wa watahiniwa, uchapaji, usahihishaji wa mitihani na uchakataji wa matokeo.

 “Serikali  tutaendelea kuijengea uwezo NECTA na walimu kuhakikisha ufundishaji , usomeshaji na utahini unafanyika kwa  umahiri mkubwa  kuwawezesha watahiniwa kumudu mahitaji  ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia,” amesema.

Amezitaka a NECTA kutekeleza majukumu yao  kuendana na shabaha ya sera ya elimu hususani  katika upimaji umahiri.

 Amesema serikali itaendelea kuimarisha utendaji wa  Baraza hilo kulingana na mazingira mapya ya kiteknolojia na kushirikiana nalo kufikia malengo ya muda mrefu ya kuweka mitambo ya kisasa ya uchapishaji kadri uwezo utakaporuhusu.

 “Kutokana na  kukua kwa teknolojia siku hadi siku mitambo ya uchapishaji inapoteza ubora wake hivyo ili kuongeza ufanisi  katika Baraza la Mitihani, serikali itaongeza mtambo mmoja kila mwaka  kuliwezesha  baraza kuendelea kuboresha huduma zake  kupitia  teknolojia,” amesema.

 Ameeleza kuwa NECTA imeomba kuongezewa mitambo mitatu na mmoja unagharimu sh. bilioni sita, hivyo ameahidi kuanzia mwaka  wa fedha ujao kuona namna ya kuwapa mtambo mmoja kwa kila mwaka.

Naye Spika wa Bunge, Dk.Tulia Akson amelipongeza baraza hilo kwa kutimiza miaka 50, kwani ni muda muafaka wa kutafakari  lilipotoka, lilipo sasa na linapokwenda.

 Amesema bunge litaendelea kutoa ushirikiano kwa kulisimamia na kulishauri baraza hilo  kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

“Rais Dk.Samia kwa miaka hii 50 tunaomba kuangalia namna ya kuweka mazingira yanayofanana kwa wanafunzi wote kwa sababu wanatahiniwa sawa,” amesema.

Kwa upande wake  Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema ndani ya miaka 50 ya NECTA, wamefanikiwa kudhibiti wizi wa mitihani ukilinganisha na nchi nyingine.

Amesema katika mtihani uliofanyika hivi karibuni  wamebaini majaribio ya wizi lakini hayakufanikiwa kwa sababu yalidhibitiwa mapema kwa kuwa wakali.

“Kwa yoyote atakayejaribu kuiba mitihani hasa kwa mfumo wa taasisi tutamchukulia hatua kali kwa sababu Baraza la Mitihani  liko macho kila kukicha,” amesema.

  Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohomed ametoa pole kwa waathirika wa mafuriko wilayani Hanang, mkoani Manyara ambapo baadhi ya wananchi walipoteza vyeti vyao vya elimu hivyo aliahidi  kuwa Baraza litatoa mbadala.

 Hata hivyo amesema Baraza hilo limejikita kuwekeza zaidi katika Tehama kwa kutoa elimu kwa njia ya mtandaoni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles