23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Magufuli aongoza Watanzania kufanya usafi

Pg 1NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli jana aliwaongoza Watanzania kote nchini kutumia siku ya maadhimisho ya sherehe za Uhuru wa Tanganyika kufanya usafi katika maeneo ya soko la Feri jijini Dar es Salaam.

Akiwahutubia wananchi wakiwamo wavuvi alioshirikiana nao katika kazi ya kufanya usafi, Dk. Magufuli aliwashukuru kwa kujitokeza na kusema kwamba hiyo ni chachu kwa wananchi wengine kujitolea kufanya usafi katika maeneo wanayoishi.

“Ni aibu kwa nchi yetu ya Tanzania kuendelea kuwa na ugonjwa wa kipindupindu katika maeneo mbalimbali wakati wangeweza kuepukana nao kwa kujituma wenyewe katika kufanya usafi, sisi wenyewe katika maeneo yetu.

“Wakati nikifanya usafi pamoja na wavuvi na wananchi nimeelezwa shida zao wanazozipata katika masuala ya uvuvi. Ukweli shida zao ni za msingi na katika kuzingatia ujirani mwema shida zao nitazibeba na nina uhakika sitawangusha,” alisema Dk. Magufuli.

Magufuli aliyeongozana na mkewe, Janet Magufuli katika kazi hiyo, aliongeza kuwa bahati ya kukutana na wananchi hao imemsaidia kutambua namna ambavyo wananchi wa hali ya chini wanavyoonewa na kile alichokiita vikodi vya ajabu ajabu.

“Katika suala la msingi ukimtazama mvuvi mdogo utabaini kwamba zana zake anazotumia ni za hali ya chini lakini anajikuta akiumizwa kwa kupewa masharti mengine ambayo hayana maana ya kulipishwa vijikodi vidogo,” alisema.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli ametoa wito kwa wavuvi wadogo kuunda umoja wa katika dhana ya ‘Umoja ni Nguvu’ na wawachague viongozi wao kwa maslahi ya wanyonge wote.

“Nimechukua namba zao za simu ili niwasaidie kwa kuwa Serikali ni kubwa na inajali maslahi ya wanyonge na naamini hawa wanyonge ndiyo walionipigia kura, kwa hiyo tutatekeleza ilani ya CCM, lakini pia nawapongeza wote waliofanya usafi nchi nzima.

“Enzi za uhuru wetu tulipokuwa tunapata uhuru tuliambiwa ‘Uhuru na Kazi’ kwa hiyo inaende sawa na ‘Hapa Kazi Tu!’,” alisema Dk. Magufuli.

WAZIRI MKUU MAJALIWA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya, alisema idadi kubwa ya wananchi walijitokeza  na usafi umefanyika kwa asilimia 98.

Mkondya alisema katika eneo la Kariakoo Waziri Mkuu, Kasimu Majaliwa alishirikiana  na wananchi wa eneo hilo kufanya usafi.

“Pia Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadick aliungana na mkuu wa kituo cha Polisi Msimbazi pamoja na wafanyabiashara wa eneo hilo ambao walifanya usafi kwa kiwango kikubwa,”alisema.

SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA (NHC)

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Felix Maagi alisema wameshiriki kufanya usafi ili kuunga mkono wito wa Rais Magufuli alioutoa wa kufanya usafi katika maadhimisho ya sherehe za Uhuru.

Maagi alisema kazi hiyo kwa Dar es Salaam wameifanya katika maeneo ya Upanga katika nyumba zao wakishirikiana na wapangaji wa nyumba hizo.

“Kazi ya usafi tuliyoianzisha leo kwa nchi nzima itakuwa endelevu kwa wapangaji wetu kwa kuwaonyesha kwamba wanatakiwa kuendelea kufanya usafi katika maeneo yao,” alisema Maagi.

Wizara ya afya na Ustawi wa Jamii

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema itaandaa mpango maalumu wa kuendeleza zoezi la kufanya usafi nchini kama ilivyofanyika katika maadhimisho miaka 54 ya Uhuru wa Tanganyika.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Donald Mmbando alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa wizara hiyo waliofanya usafi kwenye hospitali ya kansa ya Ocean Road.

“Rais Dk. Magufuli ametusaidia kuongeza nguvu katika suala hili la usafi tunaandaa mpango maalum ili liwe endelevu na tutautaarifu umma lazima tupambane na uchafu kwani ni chanzo cha magonjwa mengi.

“Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 34 ya Watanzania pekee ndiyo wenye vyoo bora, nimewaagiza maofisa afya na waganga wakuu wa mikoa na wilaya kutoa elimu pia juu ya umuhimu wa kuwa na vyoo bora,” alisema na kuongeza kuwa wizara pia imeziagiza halmashauri zote nchini kutenga fungu la fedha katika bajeti ijayo kwa ajili ya kununua vifaa vya kuwekea taka na kuvisambaza.

 

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Ocean Roads Diwani Msemo alisema ni vyema usafi ukafanyika angalau mara moja kila mwezi.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani nchini (WHO) Rufalo Chatora, alipongeza hatua ya Rais Magufuli kuhimiza usafi kwani itasaidia kuweka mazingira safi na hatimaye wananchi kushiriki shughuli za kiuchumi jambo ambalo litaleta maendeleo.

CHUO CHA KODI

KAIMU Mkuu wa Chuo cha Kodi  (ITA) Edward Mwakimonga amesema zoezi la usafi linatakiwa kuwa endelevu ili kuepuka magonjwa ya mlipuko.

Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza kutekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli la kusherehekea sikukuu ya Uhuru wa Tanganyika kwa kufanya usafi wa mazingira Mwakimonga alisema tangu Tanzania ipate uhuru ilikuwa na kauli mbiu iliyokuwa ikisema Uhuru na Kazi hivyo kila mtanzania anatakiwa kuitekeleza.

Alisema usafi ni moja ya kazi ikiwa ni pamoja na tiba ya magonjwa ya milipuko, hivyo kila mtu anatakiwa kuwa balozi wa mwenzake ili zoezi ili liweze kuwa la mwendelezo.

“Nimefurahishwa sana na agizo hili la rais hivyo katika chuo chetu tutakaa kwa pamoja ili tupange utaratibu wa wanachuo kufanya usafi angalau kwa mwezi mara moja,” alisema Mwakimonga.

Naye Mhadhiri Mwandamizi wa ITA, Dk Jonas Senzige alisema kuwa zoezi hilo linatakiwa kuwa endelevu kama ilivyo kwa nchi kama Randa ambayo imejiwekea utaratibu wa kila mwisho wa mwezi kufanya usafi.

“Wenzetu wa Rwanda kila jumamosi ya mwisho wa mwezi kwao ni siku ya kufanya usafi hakuna mtu yeyote kuonekana anatembeatembea bila kufanya kazi hivyo na sisi tunatakiwa kuiga mfano huo,” alisema Dk Senzige.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi katika chuo hicho, Jeremiah Shushu alisema kuwa watanzania wanatakiwa kuacha kutegemea kauli kutoka juu na badala yake wanatakiwa kujituma wenyewe kufanya usafi ili kuepukana na magonjwa ya milipuko.

MAKAMANDA WA POLISI

Kamanda  wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Kamishna  Suleimani Kova  pamoja na wasaidizi wake walishiriki kufanya usafi katika eneo la Barax ambapo wananchi wa eneo hilo  nao walijitokeza kwa wingi  na kuungana kwa pamoja kutekeleza agizo la Rais Magufuli.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura alisema katika idara yake wameshiriki vizuri kufanya usafi ambapo walianza saa 11:00 kwa kufanya mazoezi ya kukimbia  kilomita 16 wakiwa askari 80 na wananchi 20.

Alisema walianza kufanya usafi  katika eneo la Bamaga hadi Mwenge sokoni  na walikamilisha saa 2:30 na walirudi kwa kukimbia  hadi Kituo cha Polisi Oysterbay na kuungana na askari wengine kufanya usafi na walihitimisha saa 5:00 asubuhi.

“Mji ulikuwa mchafu lakini tunawashukuru wananchi wamejitokeza kwa wingi kutekeleza agizo la rais na niseme kwamba suala la usafi ni la kila mmoja  si mpaka litolewe maelekezo kila mmoja anapaswa kuwajibika. Nawaomba wakurugenzi wa manispaa kuweka mikakati ya vifaa vya kuhifadhia uchafu katika  maeneo ya barabara na kutunga sheria itakayowezesha kuwachukulia hatua wanaotupa uchafu barabarani.

MANISPAA TEMEKE

Manispaa ya Temeke kwa kushirikiana na Kampuni ya simu Tanzania (TTCL) jana walifanya usafi katika soko kuu la Temeke Stereo ili kuunga mkono agizo la Rais Magufuli.

Akizungumza mara baada ya kufanya usafi huo katika soko la Temeke Stereo, Meneja Uhusiano wa Kampuni hiyo, Nicodemus Mushi alisema, usafi huo ni harakati za kuweka jiji safi na kumaliza tatizo la ugonjwa wa kipindu pindu.

Mushi alisema kampuni hiyo inajali wateja wake ambao wengi ni wananchi wa kawaida ambao pia ndio wateja wa masokoni hivyo kwa kuhudumia soko hilo kutasaidia kuweka wateja wake katika hali ya usafi na usalama pia.

“Hii ni njia moja wapo ya kuwaweka wateja wetu katika hali ya usafi na kuepukwa na ugonjwa hatari wa kipindu pindu unaosababishwa na uchafu wa mazingira TTCL tutakuwa na muendelezo wa kufanya usafi mara kwa mara,”alisema Mushi.

Wakati huo huo, Ofisa Masoko wa Manispaa ya Temeke, Tito Nombo aliipongeza kampuni hiyo kwa kutoa msaada wa vifaa mbalimbali vikiwemo matoroli ya kupepea uchafu, mafagio, reki kwa ajili ya usafi.

 

TUME YA UCHAGUZI

Tume  ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), nao  walijitokeza kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ikiwemo ofisi tatu za tume hiyo.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Ramadhan alisema wafanyakazi wa tume hiyo walifanya usafi Makao Makuu ya NEC, (Posta House), Ofisi za Uhasibu na kwenye ghala la kuhifadhia nyaraka mbalimbali za ambako kuna ofisi za mifumo ya kisasa ya kompyuta na Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Alisema usafi walioufanya ni endelevu na wanaiomba serikali isimamie utaratibu huo uwe wa kudumu.

MNYIKA AUNGA MKONO
Mbunge wa Kibamba,  John Mnyika (Chadema) ameunga mkono agizo la rais  kwa kufanya usafi katika Shule ya Msingi Mbezi na Upendo na kumtaka rais kutangaza siku maalumu kwa ajili ya kufanya usafi badala ya kusubiri maadhimisho ya uhuru.

Mnyika alisema kuwa usafi huo ulilengwa zaidi katika maeneo ya barabara na masoko lakini yeye ameamua kufanya usafi katika vyoo vya shule hizo za masingi  kwa kuwa ni moja ya mazingira hatarishi kwa mlipuko wa magonjwa kama kipindupindu na kuchafuka njia ya mkojo (UTI).
Mazingira ya vyoo vya wanafunzi ambavyo  mara nyingi vinazidiwa na idadi ya wanafunzi kuna maradhi mengi na hali ya usafi inakuwa ni changamoto kubwa sana kutokana na sababu mbalimbali. “Nimeshiriki kusafisha vyoo vya shule ya Msingi Mbezi na Upendo kama mfano kwa jamii kukumbuka kuwahakikishia watoto usalama wa mazingira sio kuwaachia walimu na wanafunzi wenyewe” alisema Mnyika.
Mbali na hilo, Mnyika  alisema rais asiishie hapo bali awabane wakandarasi ambao wanadhamana ya kufanya usafi ili kutumbua majipu ya walaji kupitia bajeti inayotolewa na halmashauri kwa ajili ya kufanyika usafi huo.

“Usafi unaendana na upatikanaji wa maji baada ya siku hii ambayo ilitengwa kwa ajili ya kufanyika usafi,  Chadema  tutakuja na kampeni ya kudai maji kwani usafi kama huu wa vyoo vya mashuleni na kwingineko unahitaji maji mengi na kiuhalisia maji hayo huwa ni shida kupatikana katika mazingira kama haya,” alisema Mnyika.

MITAANI MAGARI YA TAKA YAPUNGUA

Jijini Dar es Salaam, wananchi wamejitokeza kwa wingi kufanya usafi, huku kukiwa na upungufu wa magari ya kuzoa taka.

Katika baadhi ya maeneo magari ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yalionekana yakibeba takataka, kama hatua ya kukabiliana na changamoto ya uhaba wa magari ya kubebea taka.

MTANZANIA ilitembelea maeneo mbalimbali ya jiji hilo na kujionea moshi uliokuwa ukizagaa kutokana na uchomaji wa taka katika maeneo mengi ya jiji hilo.

Katika Mtaa wa Osterbay barabara ya Ghuba, Manispaa ya Kinondoni moshi uliotokana na kuchomwa kwa taka ngumu pamoja na nyasi mbichi ulikuwa mwingi kiasi cha magari kupita kwa shida kutokana na moshi mkubwa uliotanda.

Eneo la Msasani Macho pia lilikuwa na moshi mzito ambao ulitanda huku takataka zikiwa zimekusanywa bila kuzolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles