Na Waandishi Wetu
RAIS mstaafu wa Marekani, Bill Clinton, amewasili nchi kimya kimya jana na kukutana na Rais Jakaya Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam.
Habari za uhakika ambazo MTANZANIA ilizipata, zinasema Clinton alifanya mazungumzo ya siri na mwenyeji wake, huku waandishi wa habari waliokuwapo wakiamuriwa kuondoka Ikulu.
Msafara wa Rais Clinton uliwasili Ikulu saa 7:45 mchana ukiwa na magari 10.
Jana asubuhi, Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilipiga simu kwenye vyombo mbalimbali vya habari ikihitaji wapigapicha wa magazeti na runinga kwa ajili ya tukio hilo.
Lakini katika hali ambayo haikutegemewa na wengi, licha ya vyombo hivyo kualikwa vilijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuzuliwa kupiga picha kwa maelekezo ya maofisa walioongozana na kiongozi huyo.
Mkurugenzi wa Mawasilino Ikulu, Salva Rweyemamu, alijaribu kuwaomba maofisa usalama walioambatana na kiongozi huyo ili wapigapicha waruhusiwe, lakini alikataliwa.
Mmoja wa maofisa hao alisikika akisema ziara ya Clinton ni binafsi.
Baada ya kuona kagonga mwamba, Rweyemamu aliwaomba msamaha waandishi wote kwa madai hakujua kama hali hiyo ingetokea.
“Ndugu zangu hatukujua kama wakubwa hawa walikuwa hawahitaji vyombo vya habari, kama tungejua mapema tusingewaita hapa, imeshatokea hatuna jinsi, nyie nendeni mkaendelee na majukumu mengine,” alisema.
Katika hatua nyingine, Clinton anatarajiwa kuwasili nchini Kenya leo.
Ziara ya Clinton nchini humo itahusisha utembeleaji wa miradi inayofadhiliwa na taasisi zake za Clinton Foundation na Clinton Global Initiative.
Kwa mujibu wa gazeti la Standard la Kenya, taarifa za maofisa wa nchi hiyo zinasema Rais Clinton ataambatana na binti yake Chelsea.
Pia watatembelea kituo cha elimu ya wanawake.
Mbali ya Clinton, Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani, John Kerry anatarajia kuwasili nchini humo wiki ijayo, kwa mujibu wa chanzo cha habari ndani ya Ikulu ya Marekani ambacho hakikuwa tayari kutajwa.
Kerry anatarajia kuzuru Kenya Mei 4, mwaka huu kwa ziara ya siku mbili ambapo pamoja na mambo mengine atakuwa na vikao vya majadiliano ya namna ya kukatisha mirija ya kifedha ya kundi la wanamgambo wa Somalia la Al-Shabaab.
Ziara ya Kerry, inakuja wiki kadhaa baada ya ujumbe kutoka Baraza la Seneta na Bunge la Marekani kuitembelea Kenya na kukutana na viongozi wa nchi hiyo akiwamo Rais Uhuru Kenyatta na viongozi wa upinzani Raila Odinga na Kalonzo Musyoka.
Timu ya watu watano kutoka Capitol Hill, tayari imezuru Kenya kwa siku tatu ili kutathimini hali ya usalama na vita dhidi ya ugaidi.
Wakati huo huo, magari mawili ya Limousines yatakayotumiwa na Rais Barack Obama wa Marekani wakati wa ziara yake nchini Kenya Julai, mwaka huu tayari yamewasili.
Magari hayo aina ya Cadillacs yanafanana mno, lakini lile linalombeba Obama kwa kawaida hujulikana kama ‘mnyama’.
Gari la Rais Obama liliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta wiki mbili zilizopita kabla halijapelekwa kwenye ubalozi wa Marekani nchini humo.
Hii itakuwa ziara ya kwanza ya Rais Obama nchini Kenya tangu ashike madaraka.
Akiwa Kenya, Rais Obama anatarajia kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa ujasiriamali uliopangwa kufanyika Nairobi.
Makachero wa vikosi vya siri vya kumlinda Rais Obama tayari wameitembelea Kenya.
Hata hivyo, haijaweza kufahamika iwapo mke wake Michelle Obama na binti zao wawili watajumuishwa kwenye safari hiyo.
Pia haijafahamika kama atatembelea nyumbani kwa bibi yake katika Kijiji cha Kegoro.