MANILA, PHILIPPINES
RAIS Rodrigo Duterte, amesema ataamuru kuuawa kwa mtoto wake wa kiume iwapo tuhuma za kuuza mihadarati dhidi ya mwanasiasa huyo kijana zitakuwa kweli na polisi watakaomuua watalindwa.
Mwanae huyo, Paolo Duterte (42), alionekana mbele ya Kamati ya Seneta akikana tuhuma zilizotolewa na mbunge wa upinzani, kwamba yu mwanachama wa kundi la China linalohusika na dawa za kulevya aina ya crystal methamphetamine kutoka nchini humo.
Rais Duterte hakurejea tuhuma hizo, lakini alisisitiza kauli aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi kuwa hakuna watoto wake wanaohusika na dawa za kulevya, lakini watakabiliwa na adhabu kali iwapo watabainika.
“Nilisema awali kwamba iwapo nina watoto wanaoshiriki katika dawa hizi, wauawe ili watu wakose cha kusema,” alisema Duterte katika hotuba yake juzi usiku mbele ya wafanyakazi wa Serikali Ikulu mjini hapa.
Aliongeza: “Hivyo nakuambia Pulong (jina la utani la Paolo). Amri yangu ni kukuua iwapo utakamatwa. Na nitawalinda polisi watakaokuua, iwapo ni kweli unashiriki uchafu huu.”
Duterte, alishinda uchaguzi wa urais kwa ahadi ya kupambana na mihadarati, kitu ambacho amekitimiza kwa kuendesha operesheni katili iliyoua watu zaidi ya 3,800 tangu aingie madarakani katikati ya mwaka jana.
Alisema kuwa atafurahia akiua watu milioni tatu wanaojihusisha na mihadarati.