23 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

Polisi watakiwa kupima madereva afya ya macho

Dotto Mwaibale-Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, ameshauri Jeshi la Polisi kupitia kitengo chake cha Usalama Barabarani kuanzisha dawati maalumu la upimaji wa afya ya macho ili kupunguza ajali zitokanazo na uoni hafifu.

Dk. Nchimbi aliyasema hayo mwishoni mwa wiki mkoani hapa wakati wa upimaji macho unaoendeshwa na Shirika lisilo la kiserikali la Sightsavers, linalokwenda sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Usalama Barabarani.

“Kati ya dawati ambalo mnatakiwa kuwa nalo kwa sasa ni hili la afya ya macho, niwasihi shirikianeni na wataalamu wa macho, nendeni mkafanye kampeni ya afya ya macho, mkisema jamii itawaelewa na ajali zinazotokana na tatizo hili la uoni hafifu zitapungua.

“Tunapoadhimisha Wiki ya Usalama Barabarani tusisahau kuwa afya ya macho ni kati ya kipengele na mhimili muhimu katika suala zima la usalama barabarani hapa nchini.

“Endapo kila mtumiaji wa barabara atapatiwa huduma stahiki ya afya ya macho, ni dhahiri atakuwa mwangalifu, makini na hatimaye kuweza kupiga hesabu zinazotakiwa awapo barabarani,” alisema Dk. Nchimbi.

Alisema iwapo mtumiaji wa barabara anakabiliwa na tatizo la macho, badala ya kuona gari moja anajikuta anaona mawili.

“Wakati mwingine mtu yupo pembeni ya barabara, lakini badala ya kusubiri anaamua kukatisha barabara akiamini chombo cha moto kilicho kulia kwake au kushoto bado kipo mbali,” alisema Dk. Nchimbi.

Alisema yote hayo ni matokeo ya matatizo ya afya ya macho ambayo kwa pamoja Jeshi la Polisi na jamii wakiamua tatizo hilo litamalizika.

Dk. Nchimbi alisema suala la usalama barabarani halimaanishi wale wanaoendesha vyombo vya moto pekee, bali ni kwa watumiaji wote wa barabara, wakiwemo watembea kwa miguu, hivyo kuhimiza kila mtu anapaswa kuchukua tahadhari wakati wote.

“Mtumiaji wa barabara unapokuwa barabarani hakikisha kwanza macho yako yapo sawasawa, pia unapaswa kuwa wewe mwenyewe ni dereva unayejiendesha.

“Lakini muendeshe pia na mwenzako aliye kushoto kwako, kulia kwako na nyuma yako, hii iwe kwa wote ikiwemo waendesha bodaboda, baiskeli, bajaji, wafugaji na vyombo vingine vya moto ili tuweze kumaliza kabisa ajali hizi zinazoweza kuepukika,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,800FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles