25 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 6, 2022

Contact us: [email protected]

Polisi wapya walilia mishahara miezi minne

IGP Ernest Mangu
IGP Ernest Mangu

Na TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM

WAKATI kasi ya uhakiki wa watumishi hewa ikiendelea, imebainika baadhi ya taasisi za Serikali ikiwamo Jeshi la Polisi halijawalipa mishahara askari wake wapya walioajiriwa Juni, 2016 kwa kipindi cha miezi minne sasa.

Habari za uhakika ambazo MTANZANIA imezipata Dar es Salaam jana na kuthibitishwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Mambo yaNdani ya Nchi, Christina Mwangosi, zinasema askari wapya hawajalipwa mishahara kutokana na maandalizi ya mfumo mpya wa malipo.

“Unajua kuna taratibu za malipo zinaendelea kufanyiwa kazi, hivi sasa majina yao yanaingizwa kwenye mfumo wa malipo kutokana na uhakiki unaondelea.

“Kuna baadhi yao hawajalipwa, lakini wizara inaendelea kuwaingiza katika mfumo huo, tunaamini watalipwa pindi taratibu zote zitakapokamilika,” alisema Christina.

Wakizungumza na gazeti hili, kwa sharti la kutotaja majina yao gazetini, askari hao walisema wamekuwa wakiishi maisha magumu kutokana Juni hadi sasa.

“Tangu tumehitimu mafunzo hatujawahi kulipwa mishahara yetu, tunaishi katika mazingira magumu.

“Hatuna fedha za kujikimu, kila mmoja wetu ana majukumu yake ambayo anapaswa kuyatimiza kupitia malipo ya mshahara…tunaomba tuangaliwe,”alisema mmoja wa  askari  huyo.

Lakini askari mmoja kutoka Idara ya Uhamiaji makao makuu, alisema baada ya kumaliza mafunzo waliajiriwa, lakini nao  hawajawahi kulipwa.

“Tulipotoka depo tulipewa likizo ya mwezi mmoja kusubiri kuingizwa katika mfumo wa malipo, tuliporudi tumeendelea kufanya kazi bila kulipwa mishahara jambo linalotufanya tuishi kwa shida,” alisema.

Alisema hawaelewi kwanini suala hilo linachukua muda mrefu kumalizika.

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani  ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira kuzungumzia suala hilo,  alisema baada ya askari hao  kumaliza mafunzo majina yao yalipelekwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa ajili ya kuingizwa kwenye mfumo wa malipo.

“Walivyotoka mafunzoni tuliwapokea na kupeleka majina yao Utumishi kama bado hawajaanza kulipwa nakuomba waulizeni Utumishi ndiyo wenye majibu sahihi,” alisema Meja jenerali Rwegasira.

Alipoulizwa Serikali kusitisha ajira mpya,  Meja Jenerali Rwegasira alisema ajira za askari huanza pale wanapoingia mafunzoni.

“Unajua ajira za jeshi, si sawa na za raia wa kawaida kwa kuwa wanapoanza mafunzo huingia moja kwa moja kazini, ndiyo sababu tumepeleka majina yao huko,”alisema.

Alisema baada ya Serikali kusitisha ajira mpya,hata wao wamelazimika kusimamisha udahili wa askari wapya katika vyuo vyao.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki alipoulizwa suala hilo, alimtaka mwandishi awasiliane na Katibu Mkuu Utumishi, Dk. Laurean Ndumbaro.

Juhudi za kumtafuta Dk. Ndumbaro, hazikufanikiwa kwa sababu yake ya kiganjani muda wote haikuwa hewani.

AGIZO

Juni 19, mwaka huu, Dk. Ndumbaro aliliambia gazeti hili kuwa Serikali imesitisha ajira zote kama njia ya kukabiliana na wimbi la watumishi hewa.

Alisema hakuna nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa Serikali na wakala zake pamoja na utoaji wa vibali wa likizo ya bila malipo.

Alisema lengo kubwa ni kupitia upya muundo wa Serikali na taasisi zake.

Alisema utekelezaji wa mkakati huo, utakwenda sambamba na kusitisha kwa muda utoaji wa vibali vya ajira zote mbadala pamoja na uidhinishaji wa ajira hizo zilizopo Sekreterieti ya Ajira katika utumishi wa umma na kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi.

“Ni kweli tumesitisha kwa muda ili kupitia mfumo wa Serikali na hata kuangalia ulipaji wa mishahara kama upo katika malipo stahiki.

“…na hili litakwenda sambamba na hata kusitishwa malipo ya mishahara yanayotokana na upandishwaji wa vyeo kwa watumishi. Tukimaliza kazi  hii ndipo tunaweza kuanza kutoa ajira za Serikali,” alisema Dk. Ndumbaro.

Alisema muundo mpya wa utumishi wa Serikali unakwenda sambamba na uhakiki wa malipo ya mishahara, hivyo ni lazima ijulikane ni nani anayelipwa kuliko ilivyo sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,605FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles