25.8 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

OMOG AIAGIZIA STAND MVUA YA MABAO

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

BAADA ya kupiga kambi ya wiki moja jijini Mwanza, Simba, imepanga kuifuata Stand United  mkoani Shinyanga leo, huku kocha wa timu hiyo, Joseph Omog, akiwataka wachezaji wake hasa wa safu ya ushambuliaji kutambua kuwa kila mmoja ana wajibu wa kufunga mabao kadiri inavyowezekana.

Simba itakuwa mgeni wa Stand United katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara litakalopigwa kesho kutwa  kwenye Uwanja wa Kambarage.

Kikosi cha Simba kilisalia Mwanza baada ya mchezo wake dhidi ya Mbao FC uliofanyika wiki moja iliyopita kwenye Uwanja wa Kirumba na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Sare hiyo haikuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo, hivyo watataka kuona ikiifanyizia Stand United na kuzoa pointi tatu ili kuzidi kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu.

Wekundu hao wa Msimbazi wanashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa wamejikusanyia pointi nane, sawa na timu za Singida United na Yanga, lakini zikitofautiana kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, aliliambia MTANZANIA jana kuwa amekipika kikosi chake kiasi cha kutosha kwa ajili ya kuivaa Stand United na kuvuna pointi tatu ili kujiweka vizuri katika msimamo wa ligi.

“Tumepanga kwenda Shinyanga kesho (leo), baada ya kufanya maandalizi ya nguvu, nafahamu mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa hivyo lazima tuwe makini.

“Tumeimarika kiasi cha kutosha, nilikuwa nashughulika  zaidi na ufungaji nahitaji kila mchezaji afunge, nataka nione hili likifanyika Jumapili tutakapocheza na Stand United,” alisema.

Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles