25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

NSUNZA: ILALA TUMETENDA HAKI KATIKA KUPANDISHA MADARAJA WALIMU

Na Adili Mhina, Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Kamati ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Wilaya ya Ilala, Janeth Nsunza amesema Kamati yake imetenda haki katika kupandisha vyeo/madaraja walimu ambapo jumla ya walimu 2367 wa Wilaya hiyo wamepandishwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Wilaya ya Ilala, Janeth Nsunza akieleza jambo kwenye Kikao cha Kamati hiyo kilichokaa hivi karibuni kwa lengo la kuwapandisha vyeo walimu.

Nsunza ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa kuhitimisha kikao cha Kamati hiyo kilichokaa kwa siku mbili kwa lengo la kupandisha madaraja walimu kama ilivyoelekezwa na Serikali.

“Kamati yangu ina wajumbe makini, tumefanya kazi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa na kila mtu ametendewa kama sheria inavyotaka. Haikuwa kazi nyepesi hata kidogo lakini na tunamshukuru Mungu kila kitu kimekwenda vizuri, nina imani kuwa hakuna mwalimu wa Ilala atakayekuwa na malalamiko ya madaraja,” alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na kauli aliyoitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan juu ya kupandisha vyeo watumishi wa umma, walimu wamekuwa na imani na matarajio kuwa kutakuwa na mabadiliko ya maslahi katika ajira zao, hivyo Kamati yake ina wajibu wa kufanya vizuri ili kukidhi matarajio hayo.

“Tangu tulivyoanza kazi tumeendelea kuperuzi na kuhakikisha kila daraja haachwi mtu, pale tulipogundua tuna jalada la mtu lakini kwenye orodha limerukwa au majina yao yanashida tumekwenda mbali zaidi kutafuta vielelezo ili kupata taarifa sahihi,” alisema.

Nsunza amewatoa hofu walimu wa Wilaya hiyo na kusema kuwa waendelee kufanya kazi kwa moyo na wawe na imani kuwa Kamati yake imetekeleza kikamilifu agizo la Rais Samia Suluhu Hassan na katika kipindi kifupi kijacho watapokea barua zao za kupanda madaraja.

Akifafanua idadi ya walimu waliopandishwa madaraja, Kaimu Katibu wa TSC wilayani hapo, Subira Mwakibete, alisema kuwa  katika Jumla ya Walimu 2,367 wa shule za msingi na sekondari waliopandishwa madaraja, walimu 1,362 ni wa shule za msingi na 1,005 ni wa sekondari.

Alisema baada ya Kamati kufanya uamuzi wake, kazi inayoendelea ni kuandaa barua za walimu pamoja na kuwasilisha nyaraka mbalimbali za waliopandishwa vyeo kwa mamlaka zingine ili ziendelee na hatua zinazotakiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC Makao Makuu, Christina Hape ambaye alikutana na Kamati hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya zoezi la kupandisha vyeo walimu, alisema kuwa ni muhimu pande zote zinazohusika katika madaraja ya walimu zifanye kazi kwa ushirikiano zaidi.

Hape alitaja baadhi ya taasisi zinazohusika moja kwa moja kwenye zoezi hilo kuwa ni TSC, Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango.

“Suala la promotion (upandishaji vyeo) kwa walimu si la TSC peke yake, sisi tunalianzisha tu na kutoa barua kwa mwalimu kuwa tumekupandisha. Lakini michakato mingine ya maslahi yao inaanzia kwa mwajiri, iende UTUMISHI hadi Wizara ya Fedha ambao ndio wenye fedha za kulipa mishahara,” alisema Hape.

Aliongeza kuwa; “Uhusiano wetu unatakiwa uwe wa karibu zaidi, tufanye kazi kwa pamoja kwa kuelewana ili mwalimu aweze kuishi vizuri. Pale ambapo itatokea changamoto, ni vyema mawasiliano yafanyike haraka na wote tushirikiane kuitatua, lengo nikufanya mwalimu asiwe na manung’uniko,” alisema.

Katika kusisitiza hilo, Hape amemtaka Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC wilayani hapo kuhakikisha ofisi yake inaongeza kasi katika kukamilisha taratibu zilizosalia ili kutoa fursa kwa mamlaka zingine kuendelea na hatua zao.

“Lazima ujipange vizuri kuhakikisha mambo yanakwenda harakaharaka. Unajua sasa hivi kila mtu anapambana watumishi wake waingizwe kwenye mfumo ili approvers (waidhinishaji) kule utumishi warekebishe mishahara yao kwa wakati. Lazima na wewe uhakikishe kazi yako inakamilika haraka ili wilaya yako isije ikabaki nyuma,” alisisitiza.

Katika mwendelezo wa ziara hiyo, Mkurugenzi Hape alitembelea pia Wilaya za Temeke na Kigamboni ambapo aliridhishwa na utekelezaji wa zoezi hilo. Alisema kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ndio wenye idadi kubwa ya walimu, hivyo aliamua kufanya ziara hiyo ili kuona namna zoezi linavyokwenda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles