31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

‘NISHATI YA UMEME CHANGAMOTO KUKUZA UCHUMI WA VIWANDA’    

                          

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

URAHISI wa kuingia kwenye sekta za soko zenye matarajio mazuri ya kukua na changamoto zinazokumba kampuni katika shughuli zao ni miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa wakati wa kutia saini mkataba wa maelewano (MoU) kati ya TPSF na Taasisi ya Utafiti na Ushauri wa Kimataifa ya Oxford Business Group (OBG) Julai, mwaka huu.

Godfrey Simbeye, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, aliyesaini mkataba (MoU) kwa niaba ya taasisi hiyo, alisema upatikanaji wa nishati/umeme kwa bei nafuu na wa kutegemewa bado ni changamoto kubwa kabisa kwa malengo ya nchi ya kujenga uchumi wa viwanda.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo wa TPSF alieleza kuwa, kutokana na uwekezaji unaofanywa na utawala wa Rais Dk. John Magufuli kwenye miradi mikuu ya miundombinu, hali inategemewa kuboreka kwa kiasi kikubwa katika miaka ijayo. Alitolea mfano mradi wa megawati 2,100 ya Stigler’s Gorge.

Mbali na hayo, Simbeye alizungumzia changamoto zinazokumbana na kampuni katika upatikanaji wa mikopo ya riba nafuu kutoka taasisi za kifedha na wawekezaji binafsi, hususani katika hatua za mwanzo na za kati.

“Changamoto hizi mbili zitaendelea kuinyima Tanzania nafasi ya kuendesha miradi mikubwa ya viwanda na kuwafanya wawekezaji binafsi wazawa kusita kushiriki katika miradi hii,” alisema.

Baada ya kutia saini, Mkurugenzi wa Kitaifa wa OBG, Ivana Carapic, alisema taasisi hiyo itaangalia masuala haya pamoja na mengine katika chapisho lake lijalo, The Report: Tanzania 2017.

Alisema uchumi wa Tanzania kubadilika kuwa wa viwanda itakuwa ni eneo kuu la chapisho hilo pamoja na jitihada za Serikali kupunguza mfumo wa uchumi usio rasmi na changamoto iliyopo ya kufidia upungufu kwenye bajeti bila kubana zaidi biashara.

“Cha kuzingatiwa, Tanzania ina idadi kubwa ya miradi ya miundombinu inayotarajiwa kutekelezwa ambayo ina uwezo wa kubadilisha mwelekeo wa nchi,” alisema.

“Zaidi ya hayo, jitihada za kitaifa zinazowalenga wenye kipato cha kati zinategemewa kuzaa fursa nyingi za uwekezaji, ninategemea kufanya kazi pamoja na TPSF katika kuelezea masuala ambayo kampuni zingependa yashughulikiwe na maeneo ya uchumi ambayo yako tayari kwa ukuaji wakati tunapoanza chapisho letu la kipekee.”

Kwa mujibu wa mkataba wa MoU, TPSF itachangia kwenye ripoti ya kwanza ya OBG juu ya fursa za uwekezaji Tanzania na shughuli za kiuchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles