23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

Ni bajeti ya uchaguzi

NA FREDY AZZAH, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Fedha, Saada Mkuya, ametoa mwelekeo wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2015/16 ya Sh trilioni 22.4 na kusema kipaumbele chake kitakuwa ni uchaguzi mkuu, maji na nishati.
Kwa mujibu wa Mkuya, bajeti hiyo haina miradi mingi mipya kwa kuwa itajikita kumaliza miradi ambayo haikukamilishwa na bajeti iliyopita.
Mkuya alitoa mwelekeo wa bajeti hiyo jijini Dar es Salaam jana mbele ya wabunge wa Bunge la Muungano.
“Katika bajeti hii, shilingi trilioni 16.7 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 5.4 zitakuwa ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
“Bajeti hii ni ya kipekee kwani ni ya mwaka wa uchaguzi mkuu, ni ya mwaka wa mwisho kwa Serikali ya awamu ya nne, ni ya mwaka wa mwisho wa Mkukuta, ni ya mwaka wa mwisho wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano na pia ni ya mwaka wa malengo ya milenia kwa mwaka 2015.
“Bajeti itaweka kipaumbele katika kugharamia uchaguzi mkuu na kuweka msukumo maalumu kwenye miradi ya umeme vijijini, miradi ya maji vijijini na kuimarisha rasilimali watu,” alisema Mkuya.
Kwa upande wa fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, alisema Sh trilioni 6.6 zimetengwa kwa ajili ya mishahara, huku Sh trilioni 2.6 zikiwa ni za kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva.
Alisema fedha za miradi ya maendeleo ambayo ni sawa na asilimia 25.9 ya bajeti yote, Sh trilioni 4.3 ambazo ni sawa na asilimia 75 ya fedha hizo, zitatoka kwenye vyanzo vya ndani.
Sh trilioni 1.8 ambazo ni sawa na asilimia 8.4 zitakuwa ni fedha za wahisani ikilinganishwa na mwaka 2014/2015 ambapo fedha hizo zilikuwa ni asilimia 14.8.
“Pamoja na hayo, kwenye bajeti yote, jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 14.8, sawa na asilimia 57.8 na kodi itakuwa ni Sh trilioni 13.3 ambazo ni sawa na asilimia 90.1 ya mapato ya ndani. Yale mapato yasiyo ya kodi ya halmashauri yatakuwa ni shilingi bilioni 949.2.
“Hata hivyo, Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 5.7 kutoka vyanzo vyenye masharti ya kibiashara,” alisema.

DENI LA TAIFA
Kuhusu deni la taifa, Mkuya alisema hadi kufikia Machi mwaka huu limefikia dola za Marekani bilioni 19.5 ikilinganishwa na dola bilioni 18.7, Machi mwaka 2014.
“Ongezeko la deni la taifa lilitokana na mikopo mipya kutoka vyanzo vya masharti nafuu pamoja na malimbikizo ya riba ya deni la nje.
“Fedha za mikopo hiyo zilitumika kugharamia miradi ya maendeleo hususani katika sekta ya ujenzi, nishati, uchukuzi, elimu na maji. Hata hivyo, vyanzo vya kimataifa vinaonyesha deni letu la taifa bado ni himilivu,” alisema.

MSAADA WA WAHISANI 2014/15
Waziri Mkuya alisema kwa bajeti inayomaliza muda wake, wahisani waliahidi kuchangia dola za Marekani trilioni 2.9 ambazo ni sawa na asilimia 14.8 ya bajeti yote lakini hadi kufikia Machi 2015, fedha zilizokuwa zimetolewa na wahisani hao ni Dola za Marekani trilioni 1.5 ambazo ni sawa na asilimia 54 ya ahadi yao.

MFUMUKO WA BEI
Alipokuwa akizungumzia mfumuko wa bei, waziri huyo wa fedha alisema mwaka 2014 ulipungua na kufikia asilimia 6.1 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 7.9 mwaka 2013.
Mkuya alisema kushuka kwa mfumuko huo kulisababishwa na mambo mbalimbali ikiwamo kushuka kwa bei ya petroli katika soko la dunia na la ndani, upatikanaji wa mavuno ya chakula na utekelezaji mzuri wa sera ya bajeti.

KUPOROMOKA KWA SHILINGI
Mkuya alikiri kuwa thamani ya shilingi ya Tanzania iliyokuwa tulivu dhidi ya dola ya Marekani kwa miaka mitatu kuanzia 2012, imeshuka kwa kasi kuanzia robo ya mwaka 2014.
“Hata hivyo, kushuka huko kwa kiasi kikubwa kumetokana na kuimarika kwa dola ya Marekani dhidi ya sarafu nyingine.
“Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania, Juni 2014, dola moja ya Marekani ilikuwa ni sawa na shilingi 1,650.97 wakati Aprili 23 mwaka huu, dola hiyo ilifikia shilingi 1,814.99.
“Siyo tu thamani ya shilingi yetu iliyoshuka dhidi ya dola, bali hata thamani ya sarafu nyingine kubwa kama vile euro ya Ulaya, pauni ya Uingereza, yen ya Japan, randi ya Afrika Kusini na nyingine nyingi, zilishuka pia.
“Kasi ya thamani ya shilingi kuporomoka inatarajiwa kwisha siku za usoni kutokana na kupatikana kwa mikopo ya kibiashara yenye thamani ya dola za Marekani milioni 500.
“Pia kuanza kwa msimu wa mapato ya utalii kuanzia Mei mwaka huu na mauzo ya bidhaa za kilimo nje ya nchi, ni sababu nyingine zitakazochangia shilingi yetu kutengemaa,” alisema Mkuya.

DK. MARY NAGU
Akiwasilisha mpango wa maendeleo ya taifa wa mwaka 2015/16, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Dk. Mary Nagu, alisema ni wa miaka mitano kuanzia mwaka 2011/12 hadi 2015/16.
“Hivyo basi, miradi mingi ni ile inayoendelea kutekelezwa na iliyo kwenye mpango wa mwaka 2014/15. Mpango wa mwaka 2015/16 utaendelea kuandaa programu ya miradi ya kisekta yenye uhusiano wa moja kwa moja na mpango wa maendeleo wa miaka mitano na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
“Mambo muhimu yaliyoingizwa kwenye mpango huo kwa mwaka 2015/16 ni kukamilisha miradi inayotekelezwa chini ya Mpango wa Maendeleo Makubwa Sasa (BRN), kuendeleza rasilimali watu, kuhakikisha chakula cha kutosha nchini kinakuwapo, kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi,” alisema Dk. Nagu.
Pamoja na hayo, alisema miradi ya kilimo imetengewa Sh bilioni 131.6, viwanda na biashara vimetengewa Sh bilioni 62.5, ardhi nyumba na makazi zimetengwa Sh bilioni 7 na maji yametengewa Sh bilioni 362.2.
Alisema nishati na madini zimetengewa Sh bilioni 375.8, uchukuzi zimetengwa Sh bilioni 143.5 na Sh bilioni 2.6 zimetengwa kwa ajili ya sayansi, teknolojia na mawasiliano wakati Sh bilioni 673.5 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi.
“Pia jumla ya fedha zilizotengwa kwa miradi hiyo ambayo ni ya kimkakati ni shilingi trilioni 1.6,” alisema Dk. Nagu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles