27.5 C
Dar es Salaam
Friday, July 1, 2022

New Habari yapata pigo

Na AVELINE KITOMARY  -DAR ES SALAAM 

KAMPUNI ya New Habari (2006) Ltd, inayozalisha magazeti ya Mtanzania, Rai, Bingwa na Dimba imepata pigo baada ya jana kuondokewa na mshauri wa kampuni katika masuala ya utawala na biashara, Benjamin Ackland Mhina.

Mhina ambaye alikuwa akitibiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alifariki dunia jana asubuhi baada ya kupata malaria kali ghafla.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, mtoto wa marehemu,  Ackland Mhina, alisema baba yake alipelekwa hospitali siku ya Jumapili baada ya kuugua ghafla na alikuwa akiendelea kutibiwa hadi mauti yalipomkuta. 

Kwa mujibu wa Ackland, baba yake alikuwa anasumbuliwa na shinikizo la damu kwa muda mrefu na baadae alipata malaria kali ambayo ndiyo ilimsababishia kupelekwa hospitali. 

“Alikuwa anasumbuliwa na ‘blood pressure’ (shinikizo la juu la damu) kwa muda mrefu, lakini akapata malaria kali ambayo  hakujua kwa muda mrefu kama anayo na hivyo iliathiri figo na kichwa. 

“Tulimpeleka Muhimbili siku ya Jumapili saa mbili usiku baada ya kuzidiwa sana, na alikaa hospitali siku tano tu hadi leo (jana) Alhamisi akafariki alfajiri,” alisema Ackland.

WASIFU WA MAREHEMU 

Benjamin Mhina ambaye ni miongoni mwa wafanyakazi wachache waliofanya kazi muda mrefu Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, na kabla ya hapo ikiitwa Habari Corporation, alizaliwa Juni 6, 1955 Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.

Alipata elimu ya msingi Shule ya Msingi Bunge, Dar es Salaam na elimu ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi sita  Shule ya Mzizima pia ya Dar es Salaam.

Baada ya kuhitimu elimu ya sekondari, mwaka 1974 hadi 1975 alifanikiwa kupata stashahada ya sayansi ya siasa, uchumi, filosofi na saikolojia Chuo cha Comsomol Institute kilichopo Moscow nchini Urusi. 

Mwaka 1975 hadi 1981 alifanikiwa kusoma shahada ya uzamili ya filosofi Chuo Kikuu cha Lumumba kilichopo Moscow nchini Urusi.

Baada ya kumaliza masomo mwaka 1983 hadi 1988 alifanya kazi kama Katibu Msaidizi Idara ya Uhusiano wa Mambo ya Nje, ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mwaka 1989 alifanya kazi kama Mkurugenzi katika Kituo cha Utamaduni cha Urusi kilichopo Dar es Salaam.

Juni 1997 hadi Machi 1998 alifanya kazi kama Meneja Utawala katika Kampuni ya Habari Corporation Ltd na mwaka 1998 hadi 2000  alihudumu kama Kaimu Meneja Mkuu katika kampuni hiyo.

Mwaka 2000 hadi 2003 alikabidhiwa rasmi nafasi ya Meneja Mkuu katika Kampuni ya Habari Corporation.

Mwaka 2006 hadi 2015 alikuwa Mkurugenzi wa Mauzo na Usambazaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd na baada ya kustaafu kazi Juni 2015, alikuwa mshauri wa kampuni hiyo katika masuala ya utawala na biashara,  kazi aliyoifanya hadi mauti yalipomkuta Mei 21.

Marehemu ameacha mke na watoto wawili.

Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina la Mungu wa Yakobo lihimidiwe, Amin.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,419FollowersFollow
544,000SubscribersSubscribe

Latest Articles