27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

NDUGAI AONGOZA WAOMBOLEZAJI MAZISHI YA DK. MACHA

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa (kushoto), akisalimiana na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, wakati wa mazishi ya Mbunge wa Viti Maalumu wa Chama hicho, Dk. Elly Macha, yaliyofanyika kwenye makaburi ya familia katika kijiji cha Kirua Vunjo mkoani Kilimanjaro. Katikati ni Spika wa Bunge, Job Ndugai.

 

Na Safina Sarwatt – Kilimanjaro

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, jana aliwaongoza maelfu ya Watanzania katika mazishi ya mbunge wa viti maalumu, Dk. Elly Macha (Chadema) aliyefariki dunia nchini Uingereza, Machi 31, mwaka huu.
Mazishi hayo yaliyofanyika  kwenye  makaburi ya familia katika Kijiji cha Kirua  Vunjo, Wilaya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, yalihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Wengine waliohudhuria ni pamoja na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki na waliowahi kuwa mawaziri wakuu, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye ambao sasa ni makada wa Chadema.

Akitoa salamu za rambirambi, Spika Ndugai, alisema Dk. Macha alikuwa miongoni mwa waliokuwa wakitetea sana haki za watu wenye ulemavu, hivyo Bunge limempoteza mtu muhimu sana katika kutetea masilahi ya taifa kwa ujumla.

Naibu Spika, Dk. Tulia, alisema Dk. Macha alikuwa mfano wa kuigwa kutokana na umahiri wake na kwamba alikuwa mwenye upendo na watu wote bila kujali kabila wala dini.

Kwa upande wake, Kairuki alisema kuwa Dk. Macha alikuwa mpenda maendeleo na mzalendo kwa nchi yake.

“Dk. Macha alikuwa ni mtu wa pekee aliyependa kuendeleza tamaduni za Kiafrika, alikuwa mpenda amani, mara zote alikuwa mzalendo kwa nchi yake,” alisema Kairuki.

Naye Mbowe alisema kuwa Dk. Macha alikuwa hazina kubwa katika chama chao na kwamba wamepata pigo kubwa kwa kuondokewa na mbunge huyo.

Mbowe alisema kwamba Chadema kwa ujumla wamepoteza mtu wa muhimu na kwamba mchango wake utaendelea kukumbukwa daima.

Akiongoza ibada ya mazishi kwa niaba ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),  msaidizi wa mkuu huyo wa KKKT, Elingaya Saria, alisema kuwa ameridhishwa na umoja wa viongozi wa Serikali kwa jinsi walivyofanikisha kupumzisha mwili wa marehemu Dk. Macha.

“Mimi kwa niaba ya mkuu wa KKKT, nimefurahishwa sana na umoja wenu, kwani umoja ni nguvu katika taifa, hivyo mzidi kuendeleza umoja huo katika kujenga taifa hili,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles