28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

AMNESTY YAITAJA TANZANIA KUMINYA DEMOKRASIA

 

 

NA MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Haki za Binadamu (Amnesty International), limeeleza kutoridhishwa na mwenendo wa uhuru wa habari, kuminywa kwa uhuru wa vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa na haki ya kukusanyika nchini.

Kupitia ripoti yake ya mwaka 2016/2017 iliyotolewa hivi karibuni, shirika hilo lilitolea mfano kuwa Juni mwaka jana, mikutano yote ya kisiasa ilipigwa marufuku na Rais Dk. John Magufuli hadi mwaka 2020.

Kwamba marufuku hiyo ilisababisha vyama vya upinzani kupitia mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuanzisha operesheni Ukuta na kupanga kufanya maandamano ili kupinga, lakini baadaye waliyahairisha.

Licha ya vyama vya upinzani kupinga, lakini baadaye Jeshi la Polisi lilipanua agizo hilo kwa kukataza hata mikutano ya ndani ya vyama vya siasa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wafuasi 35 wa vyama vya upinzani toka Zanzibar na Bara walikamatwa na kushtakiwa kwa makosa mbalimbali ikiwamo uchochezi.

Ripoti hiyo imedai kuwa mamlaka za Tanzania zilishindwa kushughulikia vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

Pia imeuelezea Uchaguzi Mkuu wa marudio Zanzibar uliofanyika Machi, mwaka jana kuwa uligubikwa na vitendo vya fujo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, karibu watu 200 walijeruhiwa, wanawake 12 kudhalilishwa kijinsia na mmoja kubakwa.

Ripoti hiyo inaendelea kusema kuwa zaidi ya wanachama 100 wa Chama cha Wanachi (CUF), walikamatwa baada ya kupinga uchaguzi wa marudio kutokana na kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi, uliodaiwa kuwa uligubikwa na kasoro nyingi na kulikuwa na madai ya matumizi makubwa ya nguvu kupita kiasi dhidi ya wafuasi wa CUF yaliyofanywa na polisi na watu waliovaa kininja.

Pamoja na kuwapo kwa malalamiko mengi dhidi ya polisi, lakini ripoti hiyo inadai kuwa hakuna aliyeshtakiwa.

Kuhusu vyombo vya habari, ripoti hiyo inadai kuwa vinne vilifungiwa huku waandishi wa habari wakikamatwa na kushtakiwa kwa makosa mbalimbali, yakiwamo yale yaliyo chini ya sheria ya makosa ya mtandao na magazeti.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa katika kipindi hicho, gazeti la Mawio lilifungiwa moja kwa moja, huku waandishi wake watatu wakifunguliwa mashtaka ya uchochezi kwa sababu ya kuripoti Uchaguzi wa Zanzibar na mgogoro wa kisiasa ulioibuka baada ya uchaguzi.

Kwamba pia gazeti la wiki la Mseto lilifungiwa kwa miaka mitatu kwa kile kilichodaiwa ni kukiukwa kwa sheria ya magazeti baada ya kuchapisha habari iliyoonyesha ofisa wa Serikali akijihusisha na rushwa.

Pia ripoti hiyo inasema kuwa vituo vya Radio 5 na Magic FM vilifungiwa kwa kudaiwa kutoa hewani habari za uchochezi na wanawake wawili na wanaume sita walishtakiwa chini ya sheria ya makosa ya mtandao kwa madai ya kutuma habari za uchaguzi na rais kwenye mtandao wa Facebook.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa Tanzania ilishindwa kutekeleza mapendekezo ya Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuondoa udhalilishaji dhidi ya wanawake ya mwaka juzi.

Pia inadai kuwa Tanzania ni moja ya nchi zenye ndoa nyingi za watoto duniani na asilimia 37 ya wasichana chini ya miaka 18 huwa tayari wameolewa.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles