23.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 22, 2023

Contact us: [email protected]

Nchi za SADC kubadilishana wafungwa

NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

MKUTANO wa 39 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), umeridhia kwa kauli moja kubadilishana wafungwa kuwezesha kutumikia vifungo wakiwa katika nchi zao.

Makubaliano hayo, ni miongoni mwa itifaki zilizosainiwa jana wakati wa kuhitimisha mkutano huo ulioanza juzi ambao pamoja na mambo mengine, ulimpitisha Rais Dk. John Magufuli kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo.

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Rais Magufuli alisema pia wamekubaliana kushughulikia suala la amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na uanzishwaji wa chombo cha kukabiliana na majanga kama ya mafuriko, ukame, njaa, vimbunga, magonjwa ya mlipuko na mengine.

 “Nchi nne mwaka huu zinatarajia kufanya uchaguzi ambazo ni Botswana, Msumbiji, Namibia na Mauritius, tunategemea chaguzi zitafanyika kwenye mazingira ya amani na utulivu na kuzingatia vigezo vya jumuiya yetu,” alisema Rais Magufuli.

Katika suala la uchumi, Rais Magufuli alisema wamekubaliana nchi wanachama ziendelee kuboresha sera za uchumi na fedha ili kuboresha mazingira ya ukuaji uchumi katika ukanda huo.

Alisema pia wamekubaliana nchi wanachama kusimamia upatikanaji wa mapato katika jumuiya hiyo sambamba na kubana mtumizi ili fedha zielekezwe katika miradi ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, bajeti ya jumuiya hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 ni Dola za Marekani milioni 74 na kati ya hizo washirika wa maendeleo watachagia Dola milioni 31 na nchi wanachama Dola milioni 43.

“Sekretarieti itumie vizuri fedha zinazotolewa kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo badala ya kutumika kwenye semina na warsha kwa sababu nchi wanachama zinatoa michango kutoka kwenye kodi zinazokusanywa kwa wananchi wake ambao wengi ni masikini,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kama sekretarieti itabana matumizi inaweza kujenga shule, vituo vya afya au kufanya usanifu wa miradi ya miundombinu itakayoleta matokeo chanya.

“Tutafurahi kama sekretarieti itakaribisha viongozi kufungua kituo cha afya ilichojenga na kituo kimoja kinatibu watu 10,000 kwa mwaka, hivyo tutaokoa maisha ya wananchi wengi wa SADC,” alisema.

Alisema mkutano huo, umekuwa na mafanikio kwani wajumbe walijadiliana kwa utulivu, upendo na maelewano na kufikia maamuzi makubwa.

“Mara chache kulikuwa na kutofautina kwenye baadhi ya hoja, tulijadiliana kwa utulivu mkubwa na kufikia mafanikio,” alisema.

BURUNDI, ZIMBABWE

Rais Magufuli, alisema walijadili pia ombi la Burundi la kutaka kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo, lakini ilibainika bado kuna maeneo ambayo hayajakamilika, hivyo sekretarieti imeelekezwa kuieleza ili masuala hayo yafanyiwe kazi.

Kuhusu suala la Zimbabwe, alisema wataendelea kuzisihi jumuiya za kimataifa ili nchi hiyo iweze kuondolewa vikwazo vya kiuchumi.

“Tuendelee kufanya mawasiliano na jumuiya za kimataifa kuwezesha kuondolewa vikwazo, tupo pamoja na Zimbabwe na hatutaiacha,” alisema Rais Magufuli.

NYERERE ALIVYOENZIWA

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alitangaza uamuzi wa wakuu wa nchi na Serikali wa SADC kuwa lugha Kiswahili inakuwa lugha rasmi ya nne ya jumuiya hiyo kuanzia  jana.

Alisema uamuzi huo ni heshima kubwa kwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye alitumia lugha ya Kiswahi katika harakati za ukombozi wa mataifa mbalimbali ya Afrika, hususani kwa wapigania uhuru ambao walijifunza na kutumia lugha hiyo katika mapambano dhidi ya wakoloni.

Alisema kitendo cha wajumbe kukubali lugha ya Kiswahili kuwa rasmi katika jumuiya hiyo, kimeonyesha dhahiri namna walivyomuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye alijitoa kusaidia harakati za ukombozi katika nchi mbalimbali za Kusini mwa Afrika.

Amemwelezea  Mwalimu Nyerere, kuwa alikuwa mtu mwenye huruma na upendo mkubwa sio tu kwa nchi yake ya Tanzania, bali Afrika nzima kutokana na kujitoa kwake kwa hali na mali katika kusaidia mapambano ya ukombozi tena kwa gharama zilizobebwa na Watanzania.

“Suala la kutoa huwa ni gumu sana, wapo wanaojitolea figo kusaidia wagonjwa na wapo wanaosaidia kuokoa wengine, na Baba wa Taifa aliamua kutoa upendo wake kusaidia wengine.

“Nyerere alijitoa kuhakikisha mataifa mengine yanakombolewa hata kwa kutaka nchi yake ipate shida na katika shughuli zote hizo walikuwa wanatumia Kiswahili, tunafurahi sana tumefuta machozi ya Mwalimu Nyerere,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Tanzania itakuwa tayari kuunga mkono jitihada za kueneza Kiswahili katika jumuiya hiyo kwa kutoa walimu na nyenzo za kufundishia.

 ITIFAKI NYINGINE ZILIZOSAINIWA

Mpango wa kuwahamisha wafungwa utaendana na mfumo wa kimataifa hivyo ni lazima uendane na muundo wa kisheria ulioko katika nchi husika.

Itifaki nyingine zilizosainiwa jana ni zile zilizohusu viwanda na masuala ya uhalifu katika ukanda huo.

“Itifaki kuhusu viwanda inalenga kukuza maendeleo na kuongeza ushindani kwenye viwanda kuwezesha SADC kuendeleza viwanda endelevu na jumuishi,” alisema mwanasheria wa SADC.

Mbali ya itifaki hizo zilizosainiwa na nchi ya Zimbabwe ambazo ni makubaliano ya marekebisho ya itifaki iliyopitishwa mwaka 2009 na makubaliano ya marekebisho ya mkataba uliopitishwa 2009 ambao sasa utaiwezesha sekretarieti hiyo kuwa na manaibu makatibu watendaji wawili badala ya mmoja kama ilivyokuwa awali.

Itifaki nyingine iliyosainiwa na Msumbiji ni ile iliyohusu ulinzi wa aina mpya ya mimea katika ukanda huo ambayo inalenga kuhifadhi na kutunza aina mbalimbali za mimea.

Awali itifaki hiyo ilipitishwa mwaka 2017, lakini ilikuwa haijaanza kutumika kwa sababu ya kutokamilika kwa masuala kadhaa ya kisheria.

Mbali ya itifaki hizo, pia zilisainiwa programu tatu za jumuiya hiyo zinazolenga kuhamasisha utekelezaji wa kaulimbiu ya mkutano huo inayosema; ‘Mazingira Mazuri ya Maendeleo ya Pamoja na Endelevu ya Viwanda, Kuongezeka kwa Biashara ya Kanda na Uzalishaji wa Fursa za Ajira’.

Programu hizo ambazo zitasimamiwa na SADC kwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya (EU) zilitiwa saini kupitia kwa Katibu Mtendaji wa SADC, Dk. Stergomena Tax na Balozi wa EU kwa Botswana na SADC, Jan Sadek.

Programu hizo, zinahusu Uwezeshaji wa Kuboresha Uwekezaji na Mazingira ya Biashara (SIBE), Uwezeshaji kwa Viwanda na Sekta za Uzalishaji (SIP) na Programu ya Uwezeshaji (TFP).

Programu hizo zinatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano na zitagharimu Euro milioni 47.

MAKAMU MWENYEKITI

Makamu Mwenyekiti wa SADC, Rais wa Msumbiji, Philipe Nyusi, alisema anaamini Rais Magufuli ataiongoza vema jumuiya hiyo kutokana na uwezo mkubwa alionao.

 “Umeapishwa jana (juzi), lakini umezaliwa kama mtoto mkali wa kukimbia, usiwe na wasiwasi sisi tutakufuata.

“Rais Magufuli alivyosikia tumepatwa na majanga alinipigia simu akataka ataarifiwe hali iliyopo na nini afanye kusadia wananchi wa Msumbiji.

“Tunakushuru sana kwa upendo wako na heshima kubwa na mapokezi tuliyoyapata, nawakaribisha wajumbe wote katika mkutano wa 40 utakaofanyika Maputo,” alisema Rais Nyusi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,020FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles