26.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 28, 2023

Contact us: [email protected]

NANDY: Anakuja kimwendokasi express

Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’
Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’

NA KYALAA SEHEYE,

NI msichana mrembo, mdogo mwenye makeke awapo jukwaani. Ukimsikiliza sauti yake kwa makini, utagundua kuwa binti huyu amedhamiria kuingia kwenye muziki wa Bongo Fleva na kuwapa joto la nguvu mastaa wa kike wanaotesa kwenye game.

Huyu si mwingine bali ni Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’ (19) ambaye kwa kasi aliyoanza nayo ni kama amepiga hodi kimwendokasi express! Hana utani, anataka njia.

Chipukizi huyu ambaye kwa sasa anatesa na kibao chake ‘Nagusagusa’ ambacho ametoa sanjari na video yake inayosumbua kwenye vituo mbalimbali vya runinga na mitandao ya kijamii hasa Youtube amesema, anatamani kuwa na mafanikio makubwa kimataifa.

Tofauti na wasanii wengine wanaochipukia ambao wamekuwa na kawaida ya kuingia kwenye game kwa kuwashirikisha mastaa wanaotesa kwenye fani, Nandy yeye ameimba mwenyewe mwanzo mwisho.

Akizungumzia hilo, Nandy anasema ameamua kufanya hivyo ili kujitambulisha kivyake, huku akieleza hofu yake ya kufunikwa na msanii ambaye angemshirikisha.

“Nilitaka nitoke kivyangu, lakini si vibaya kufanya kolabo. Nilichohofia ni kwamba, unaweza kufunikwa na staa. Naona huwa inakuwa na maana kufanya ngoma yako ya utambulisho peke yako, watu wakikuelewa, sasa unaweza kufanya kolabo na msanii mwingine, hiyo ndiyo sababu kubwa iliyonifanya niamue kutomshirikisha msanii mkubwa kwanza,” anasema na kuongeza:

“Hata staili yangu ni ya tofauti… ndiyo maana nikaamua kuja na staili ya mavazi tofauti na wasanii wengine wa Bongo ambao wamekuwa wakivaa mavazi ya kuiga wasanii wa majuu.

“Kwangu mimi Uafrika una nafasi zaidi, najua nikiwa na mavazi yanayowakilisha Afrika na Tanzania, itakuwa rahisi kupenya katika majukwaa ya kimataifa. Ndivyo ninavyofanya na ninaamini kutakuwa na mafanikio, hata kama si sasa, lakini baadaye yatakuja.”

MY STYLE: Mwanamuziki gani wa kike anayekunyima usingizi?

NANDY: Hakuna kwakweli… na kwasababu nimekuja kikazi, naamini siku moja naweza kuwa msanii mkali kuliko wote wa kike nchini. Lakini wapo ninaokubali muziki wao.

MY STYLE: Kama binti, umepitia vikwazo gani katika game?

NANDY: Nimepitia vikwazo vingi sana, ila kubwa ni ushindani wa kikazi baina ya wasanii kwa wasanii na hilo naamini mimi nitafanikiwa kwa kuwa nina mwanzo mzuri.

MY STYLE: Nandy unaye mpenzi? Na kama huna unapenda mpenzi wako awe na sifa zipi?

NANDY: Sina mpenzi kwa sasa, ila nitakapoamua kuwa na mpenzi basi anatakiwa awe mcha Mungu kwelikweli, siyo wa maigizo. Pia awe mwenye kujiheshimu, huyo ndiye nitakayempa nafasi.

MY STYLE: Tukio gani ambalo lilikuumiza na hutalisahau maisha mwako?

NANDY: Niliumia sana pale nilipofanya wema kwa mtu niliyempenda na kuchukua kosa langu moja nililotenda kwake kama fimbo ya kunichapia.

MY STYLE: Kwa kawaida huwa unatumia manukato ya aina gani?

NANDY: Sipendi kuwa na harufu kali hadi ikamkera mwingine, napenda perfume iliyotulia, ndiyo maana nikachagua Nick Minaj.

MY STYLE: Vipi kwa upande wa magari, unatamani kumiliki gari aina gani?

NANDY: Kwakweli Lexus Harrier ndiyo gari ambalo linaniumiza kichwa, naamini ipo siku nitamiliki mkoko huo wa ndoto zangu.

MY STYLE: Je, unapenda kuvaa vito vya madini ya aina gani?

NANDY: Mimi na Gold hunitoi aisee. Nayapenda kwa sababu hata ukivaa nguo za asili, ukiweka vito vya madini hayo yanakubali na kuleta mvuto wa aina yake.

MY STYLE: Ukipewa ofa ya kutembelea mji wowote duniani, ungependa mji ganii?

NANDY: Haraka sana ningetaja Dubai, nahisi huko akili yangu ingepata burudani na ningepata mapumziko mazuri. Napenda vivutio vya mji huo.

MY STYLE: Asante sana Nandy kwa ushirikiano wako.

NANDY: Nashukuru pia dada yangu, karibu tena siku nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles