25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 9, 2024

Contact us: [email protected]

NAKULILIA  TANZANIA YANGU…TUMEFIKAJE HAPA?

 

SINA kumbukumbu yoyote ya historia ya nchi hii inayoonyesha kwamba kumewahi kutokea tukio la kushangaza kama lile lililotokea Alhamisi iliyopita mjini Dodoma, kwa mwanasiasa maarufu nchini Tanzania, Tundu Lissu, kushambuliwa kwa kupigwa risasi.

Ni kweli kwamba yamewahi kutokea mashambulizi hapo nyuma, lakini hayakuwa ya dhahiri namna hii kwa mtu maarufu, anayejulikana kuwa na kesi nyingi zaidi dhidi ya Jamhuri, kushambuliwa kwa risasi mchana kweupe kwa lengo la kuuawa.

Yamewahi kutokea mashambulizi kama yale ya Saed Kubenea na Ndimara Tegambwage, Dk. Steven Ulimboka, Absalom Kibanda, kupotea kwa kada wa Chadema, Ben Saanane, na hata kutekwa kwa msanii Roma Mkatoliki.

Watu hao walishambuliwa kwa kupigwa, wengine walipoteza fahamu na kuokotwa wakiwa hawajitambui, wengine walimwagiwa tindikali na kupigwa panga, wengine waling’olewa jino na kucha na kuumizwa vibaya, wengine wamepotea hadi leo hatujui walipo na wengine wanaogopa kabisa kusema kilichowakumba walipotekwa.

Lakini kumiminiwa risasi mchana kweupe?  Hii ni mpya. Mwenzenu mambo kama hayo nimezoea kuyaona kwenye ‘movie’, na ikimaanisha kwamba si kweli kuwa mambo hayo yanatakiwa kutokea.  Kwamba mtu anaweza kuwa maarufu kwa mema au kwa mabaya, halafu unaona gari moja likimfuatilia au magari kadhaa…wenyewe wanaiita ‘trailing’, halafu baadaye wakimpata wanammiminia risasi na kuhakikisha kwamba wanafanikiwa kummaliza kabisa.  Hayo mambo huwa hayatokei kweli jamani, ni maigizo tu.

Cha kushangaza, hayo maigizo yamegeuzwa kuwa kitu cha kweli.  Tena sio kwingine duniani, ila hapa hapa kwetu Tanzania.  Tanzania hii hii tunayojidai kuiimba kwamba ni nchi yenye amani na uzuri wa kutosha.  Tanzania hii hii tunayodai kwamba eti tunapendana sana na undugu wetu unaunganishwa na kiswahili chetu.  Tanzania hii hii tunayodai kwamba baba yetu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alituwekea misingi ya umoja na mshikamano.  Tanzania hii hii!!!

Naandika nikiwa na uchungu mwingi sana.  Uchungu nilionao hauwezi kuelezeka kwa maneno mepesi.  Uchungu nilionao unanifanya nione hata aibu, aibu kubwa ya kusimama mbele ya mataifa mengine na kudai kwamba natoka Tanzania.  Inauma jamani; tumefikaje hapa?

Tumefikaje hatua ya kubadili yale tunayosoma kwenye vitabu vya hadithi na kuyafanya kuwa kweli?  Tumefikaje hatua ya kuangalia ‘movie’ za aina ya ‘Mission Impossible’, ‘The Avengers’, ‘James Bond’, ‘The A-Team’ na nyinginezo na kuzibadili katika maisha ya kweli?  Hivi kwani hatujui kuwa yale ni maigizo tu na hayatakiwi kugeuzwa kuwa kweli?  Bado nina mshtuko!

Aliyeshambuliwa, Tundu Lissu, ndiye mwanasiasa maarufu kuliko wote hapa nchini kwa miezi kadhaa sasa.  Licha ya kuwa Mbunge wa Singida Mashariki kupitia chama pinzani cha Chadema, Lissu ni zaidi ya mbunge na zaidi ya mpinzani.

Ni mpinzani anayejua hasa kazi yake ya kupinga, kiasi cha kusababisha awe na kesi kadhaa dhidi ya Jamhuri na kiasi cha wengine kufika hatua ya kumuita “asiye mzalendo” kwa sababu tu ya kuibua na kusema hadharani ambayo wengine hawakutaka ayaseme.

Lakini huyu Lissu pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, cheo alichokipata baada ya kampeni mbaya dhidi yake kupigwa na hata aliyewahi kuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe kutishia kukifuta chama hicho endapo kingemchagua Lissu.

Alishikiliwa hata na Polisi wakati uchaguzi wa cheo hicho unakaribia, lakini alifanikiwa kuachiwa na kukimbilia Arusha kuuwahi uchaguzi ambao aliushinda kwa kishindo kikubwa, hasa kutokana na Serikali yenyewe kumfanya maarufu bila kujua.

Baada ya shambulio dhidi yake lililotokea Alhamisi iliyopita, kila mtu amekuwa na maswali yasiyo na majibu. Sisi wananchi tunataka kujua kwanini yametokea yaliyotokea na ni nani mhusika.  Kutokana na historia ya Lissu mwenyewe, watu wengi wanayahusisha moja kwa moja na masuala ya kisiasa, wengine na masuala ya kisheria, wengine pengine na mambo binafsi.

Binafsi, sitaki kabisa kuamini kwamba Tanzania imefikia hatua ya kuwanyamazisha wanasiasa kwa njia hiyo.  Sitaki kabisa kuamini.  Nataka kuendelea kuamini kwamba wapinzani wataendelea kuzuiwa kufanya kazi za siasa katika majimbo yasiyo ya kwao, kwamba wataambiwa wachape kazi na kuleta maendeleo huku wakisubiri wakati wa uchaguzi, kwamba wataendelea kuachwa wazungumzie bungeni na kwingineko.  Lakini kunyamazishwa kwa njia ya risasi?  Hapana!  Nakataa!

Lakini mimi si wananchi wote.  Kama mimi nakataa kwamba hilo shambulio si la kisiasa, ni lazima vyombo husika vihakikishe vinawahakikishia wananchi kwamba si tukio la siasa.  Njia pekee ya kuzima maneno hayo ni kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba wahusika wanapatikana, wanajulikana na sababu za shambulio lao zinajulikana pia.  Huu si wakati wa kurejea zile sentensi tulizozoea za “watu wasiojulikana…” sentensi hizo tumeshazisikia sana kwa kesi za akina Kibanda, Dk. Ulimboka na wengineo na sasa zimetuchosha.

Nguvu ile ile ambayo huwa inatumika na Jeshi la Polisi kukamata wahalifu wanaoshambulia vituo vya Polisi na kuua askari, kisha wahalifu na silaha zao kukamatwa ndani ya siku moja au mbili, ndio nguvu tunayotaka kuiona ikitumika kuwakamata wahalifu waliomshambulia Tundu Lissu.  Nguvu hiyo isipotumika na wahalifu halisi wasipopatikana, hakika nawaambia, Serikali itachafuliwa sana na tukio hilo.

Tumechoka na sentensi za “watu wasiojulikana…” ifike mahala wahalifu hawa wanaoichafua nchi yetu kwa kushindwa kutumia nguvu ya hoja na badala yake kugeukia risasi, wanyamazishwe kabisa.

 

Tukubali ama tukatae, Tanzania inamuhitaji Tundu Lissu.  Hakuna nchi ambayo inataka kila kitu kiwe kinasifiwa tu na kunyamaziwa tu.  Nchi kama hiyo ‘inaboa’.  Kila nchi inamhitaji “chizi” mmoja ambaye ana uthubutu wa kuyasema yale ambayo wengine wanashindwa kuyasema, yale ambayo wengine wanatamani kuyasema lakini hawana uthubutu wa kutosha, yale ambayo wengi wetu tunatamani kuyasikia.  Sisi Mungu ametupa “chizi” wetu ambaye ni Tundu Lissu, kwanini lakini mnataka kutuchukulia?  Tunamhitaji, mwacheni.

Lakini licha ya kwamba tunamhitaji sana Tundu Lissu, tunahitaji pia wale wanaoichafua nchi yetu wapatikane.  Kama ni mtu mmoja aliyejipa mamlaka ya kufanya upuuzi huu, ama ni watu wengi, hatuwezi kukubali nchi yetu iendelee kuchafuka kwa sababu yake.  Kwani yeye ni nani?  Huyo “mtu asiyejulikana” ni mkubwa kuliko Tanzania yetu?  Kweli hajulikani?  Kweli?

Haiwezekani kamwe wahusika waendelee kuwa “watu wasiojulikana” kwa miaka nenda-rudi.  Nakataa!  Wanachokifanya si kuwakomoa wale tu wanaowashambulia, bali hao ndio wanaokosa uzalendo wa kweli kwani wanatuchafulia Tanzania yetu…hivi wanalitambua hili?  Tuache kugeuza ‘movie’ kuwa maisha halisi jamani.  Tumefikaje hapa?

Mwisho.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles