32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 1, 2024

Contact us: [email protected]

Mwenyekiti Wazazi CCM azindua Kamati za Maendeleo, akosoa wanaobeza safari za Rais nje

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhil Maganya amezindua kamati tano ndogondogo za utekelezaji huku akitoa maagizo kuhakikisha Jumuiya hiyo inapata maendeleo.

Kamati hizo ni Uchumi, Fedha na Mipango, Afya na Mazingira, Elimu na Malezi, Michezo, Utamaduni na Sanaa na Kanuni, Maadili na Sheria.

Akizungumza leo Februari 21,2024 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi huo, Mwenyekiti huyo amewapongeza waliochaguliwa katika kamati hizo huku akiwataka kupambana ili kuleta maendeleo ya Jumuiya hiyo.

Amesema Jumuiya ina changamoto nyingi hivyo ni wajibu kuhakikisha wanapambana kwa kutumia wataalamu mbalimbali.

“Tunakubaliana na majukumu mengi, hivyo tutengeneze kikosi kazi naamini tutapiga hatua katika maeneo haya matano.Tukishambulia kwa pamoja mambo yataenda vizuri,” amesema Mwenyekiti huyo.

Aidha, amesema Jumuiya ina miradi kadhaa ya ujenzi wa hospitali tatu ikiwemo hospitali ya kisasa maalumu mkoani Shinyanga.

“Ardhi imepatikana wiki ijayo michoro itakuwa tayari na tumekuwa na mazungumzo na taasisi mbalimbali,” amesema Mwenyekiti huyo.

Pia amesema wana mradi wa Hospitali ya wazazi maalumu ambayo itajengwa Kaskazini Pemba na mipango ya kupata ardhi ilikamilika na wapo katika utaratibu wa kutafuta wahisani.

Maganya amesema pia watajenga hospitali maaalum Iringa Vijijini na tayari ekari 105 zimepatiaka.

Ameitaja miradi mingine ni viwanda ikiwemo kiwanda kikubwa cha kuchakata mafuta wilayani Muheza na wana mpango wa uanzishwaji wa kiwanda cha nguo ambacho watashirikiana na watu mbalimbali ambapo amedai kitajengwa Bunda mkoani Mara.

“Pia tuna mpango mzuri wa kiwanda cha vifaa tiba, kwahiyo kazi inaendelea na tutakuwa na mashamba mbalimbali yakiwemo ya Mbegu tunaendelea kutafuta ardhi na kuna sehemu tumepata, tutajikita na kwenye ufugaji.

“Hiki ni Chama chetu sote tukiimarika kiuchumi kitaendelea kuwa imara, tumezindua hizi kamati na zina wenyeviti ni vizuri muweke mpango kazi namna ya kufanya kazi,”amesema Mwenyekiti huyo.

Aidha amesema Jumuiya hiyo itashirikiana na Kanali Iddi Kipingu kuendeleza shule zao.

Katika hatua nyingine, Maganya ameonya wale wanaobeza safari za Rais nje ya Nchi na ndani ya Nchi kwa kudai zimekuwa na tija na zimeendelea kuleta maendeleo.

“Kuna watu wanabeza hasa anaposafiri ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kutafuta misaada.Nchi hii siyo bchi iliyoendelea ila ni inaendelea ni kweli tuna uhuru lakini hauwezi kutufanya tukapiga hatua kwa haraka.

“Nitumie fursa hii kuwaomba kwamba wamwache mheshimiwa Rais aifungue Tanzania nirejeee misemi ya Kiswahili wanasema ‘mwenda bure si mkaaa bure hueda akaokota pia Mgaa gaa na upwa hali wali mkavu na usiporudi na umande utarudi na mwiba,”amesema Mwenyekiti huyo.

Amesema wao kama wasaidizi wa Rais wataendelea kumpa sapoti kuhakikisha anailetea nchi maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles