29.7 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

MWANDISHI WA HABARI AOKOTWA AKIWA HAJITAMBUI

Na MANENO SELANYIKA-DAR ES SALAAM


MWANDISHI  Mwandamizi wa gazeti la The Guardian, Finnigan Simbeye, ameokotwa eneo la Bunju wilayani Kinondoni akiwa hajitambui.

Baadhi ya mashuhuda ambao walizungumza na MTANZANIA, walisema mwandishi huyo alikutwa kwenye kichaka akiwa ametupwa na watu wasiojulikana.

Kutokana na tukio hilo, baadhi ya wasamaria wema waliamua kumsachi na kumkuta na kitambulisho na walianza kupiga simu katika baadhi ya vyumba vya habari ili kueleza kuokotwa kwa mwandishi huyo.

Mmoja wa mashuhuda hao aliyejitambulisha kwa jina moja la  Adam, alisema walimuokota mwanahabari huyo akiwa hajitambui.

“Ilikuwa kama saa 11 alfajiri  tulipokuwa tunapita kwenda kwenye shughuli zetu, nikiwa na mwenzangu tukaona mtu amelala kwenye mtaro ndipo tuliposogea na kumwita, lakini alikuwa haitiki na tukaanza kuomba msaada kwa wenzetu hapa katika eneo la Bunju Sheli.

“Baada ya kuja baadhi ya wenzetu, wakapiga simu polisi kuwafahamisha lakini kadiri ya muda ulivyokuwa unakwenda ndipo tukaamua kuanza kupiga simu katika vyombo vya habari.

“Hata hivyo, ilipofika saa mbili polisi walifika wakiwa na gari na kuondoka naye. Kifupi tunahisi watu waliomfanyia unyama walihisi ameshakufa ndipo wakaamua kumtupa hapa kwetu. Lakini kumbe alikuwa mzima,” alisema shuhuda huyo.

Baada ya kuchukuliwa Simbeye na polisi hao, alipelekwa Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

Akizungumza jana na MTANZANIA, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Muliro Jumanne, alisema baada ya taarifa hizo za askari kufika eneo la tukio, uchunguzi wa awali umebaini hakukutwa na jeraha lolote mwilini.

“Jana majira ya saa 11:00 alfajiri tulipokea taarifa kwamba kuna mtu ameonekana huko Bunju pembeni ya barabara amelala akiwa hajitambui, askari walimkagua wakafanikiwa kupata vitambulisho ambapo vinaonesha ni mfanyakazi wa gazeti la Kiingereza la The Guardian,” alisema Kamanda.

Alisema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa Finnigan alikuwa amelewa, ambapo waliamua kumpeleka katika Hospitali ya Mwananyamala.

Muliro alisema Jeshi hilo linafanya uchunguzi na kwamba wakithibitisha alikuwa amekunywa kupita kiasi, tutampeleka mahakamani kwa sababu amesababisha taharuki katika jamii.

“Haya ni matukio ya kawaida ya mwisho wa wiki, sisi tumezoea ila tunataka kufahamu atakapozinduka atueleze alikuwa anakunywa na nani na wapi, ikibainika tutamchukulia hatua za kisheria.

“Inadaiwa alionekana juzi maeneo tofauti tofauti akiwa hajimudu, ambapo baadhi ya watu aliokuwa nao usiku huo baada ya kusikia taarifa zake hawashangai,” alisema.

Aliongeza kuwa kwa kuwa tukio hili limeleta taharuki katika jamii, bado Jeshi hilo linaendelea kukusanya ushahidi, endapo akibainika sheria itachukua mkondo wake.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dk. Festo Dugange, alithibitisha kumpokea mgonjwa huyo na kueleza kwamba alikuja akiwa hajitambui.

Alisema walimpatia huduma ya kwanza kisha baadaye walimhamishia katika wodi ya wanaume, ambapo amelazwa huku akisubiria vipimo zaidi.

“Ni kweli kuna mgonjwa alifikishwa hospitalini hapo ambaye ni mwanahabari wa The Gurdian, aliletwa akiwa hajitambui (serious condition), ambapo alipelekwa chumba cha dharura na baadaye kuhamishiwa wodini akingojea vipimo vingine, lakini hadi sasa anaendelea na matibabu,” alisema Dk. Dugange.

Akizungumza hospitalini hapo, mke wa Finnigan, Rose Mirondo, alisema mumewe aliondoka nyumbani tangu juzi asubuhi ambapo alimuaga anakwenda kazini.

Alisema mumewe hana tabia ya kuchelewa kurudi nyumbani, lakini siku za wikiendi ni kawaida yake kurejea nyumbani usiku majira kati ya saa 5 hadi saa 6 usiku ila juzi alishangaa kutoonekana hadi jana alipopata taarifa kwamba ameokotwa.

“Aliondoka na gari asubuhi kama kawaida yake kuelekea kwenye majukumu yake ya kila siku, ila juzi nilipata wasiwasi maana hakurejea nyumbani na kwamba hapakuwa na mawasiliano yoyote.

“Ilipofika jana asubuhi ndipo kuna mtu alinipigia simu akaniambia kuwa  Finnigan ameonekana huko Bunju eneo la Lake Oil, ndipo nikafika eneo hilo lakini sikufanikiwa kumkuta, nilielezwa na wenyeji kwamba amepelekwa Hospitali ya Mwananyamala,” alisema Rose.

Alisema baada ya kuwasili hospitalini hapo, alifanikiwa kumwona mumewe na kwamba alimtambua lakini hakuweza kuzungumza chochote kilichomsibu.

“Sitaweza kuzungumza zaidi, nimewaachia madaktari waendelee kufanya kazi yao lakini namshukuru Mwenyezi Mungu afya yake inatia moyo kwa sababu amenifahamu na ali ‘smile’ alivyoniona,” alisema Rose.

Baadhi ya askari waliokuwa wamevalia nguo za kiraia walifika hospitalini hapo, walionekana kutaka kuzungumza na Finngan akiwa wodini ila wauguzi waliokuwa zamu waliwaambia hawaruhusiwi kwa sababu muda wa kuona wagonjwa uliisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles