29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

‘Mwanajeshi’ ateswa kama Ulimboka

mgobaNA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM
KIONGOZI wa vijana waliopata mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), waliokuwa wakiishinikiza Serikali kuwapatia ajira, George Mgoba, amelazwa katika Hospitali ya Amana, jijini Dar es Salaam, baada ya kutekwa nyara na kisha kuteswa na watu wasiojulikana.
Mgoba ni miongoni mwa vijana waliowawakilisha wenzao zaidi ya 300 kukutana na viongozi wa juu wa Serikali hivi karibuni, akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kuzungumzia kilio chao na kupinga upendeleo wa ajira ndani ya Jeshi.

Tukio hilo ambalo kwa kiasi kikubwa linafanana na kile alichofanyiwa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka au Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda, lilimfika Mgoba Jumatatu wiki hii saa 11:00 jioni.
Mgoba, ambaye analindwa na vijana wenzake waliomaliza mafunzo ya JKT katika wodi namba saba aliyolazwa, anadai kufanyiwa vitendo vya kinyama ikiwa pamoja na kuchomwa sindano ambayo haijulikani aina ya dawa iliyokuwa nayo.

MTANZANIA Jumamosi lilifika katika Hospitali ya Amana ambako pamoja na mambo mengine, lilifanikiwa kuzungumza na Msemaji wa vijana hao, Omary Bakari, ambaye alisema alipokea simu saa nne siku ya Jumatatu hiyo hiyo ikimtaarifu kuwa Mwenyekiti wao, Mgoba, amelazwa katika Hospitali ya Tumbi, iliyoko Kibaha, mkoani Pwani.
Alisema simu hiyo aliyopigiwa na mtu aliyejitambulisha kama askari polisi pia ilimtaarifu kuwa mwenzao huyo alikuwa mahututi.
Baada ya kupata taarifa hizo, Bakari alisema alichukua jukumu la kutoa taarifa kwa baadhi ya vijana wenzao ambao walikutana katika Hospitali ya Tumbi usiku huo huo.
Alisema akiwa Tumbi alipata nafasi ya kuzungumza na mgonjwa ili kufahamu kilichompata hadi kufikia hatua hiyo.
Bakari alisema mgonjwa, huku akizungumza kwa shida, alieleza kilichomkuta ambapo alidai kuwa siku hiyo ya Jumatatu saa 11:00 jioni, akiwa nyumbani kwake maeneo ya Mabibo Loyola, alipigiwa simu na watu waliojitambulisha kuwa ni vijana wenzake wa JKT.
Alisema vijana hao walimtaka waonane eneo la Mabibo Mwisho ili wazungumze kuhusu mipango ya maandamano ya kudai ajira yaliyokuwa yamepangwa kufanyika tena keshokutwa, baada ya yale ya awali ya kuelekea Ikulu kumuona Rais Jakaya Kikwete kugonga mwamba.
“Nusu saa baada ya kupigiwa simu alifika eneo walilopanga na kukutana na watu hao ambao walikuwa ni wanawake wawili na mwanaume mmoja, waliokuwa na gari aina ya Noah,” alisema.
Akinukuu maelezo ya mgonjwa, Bakari alisema baada ya kusalimiana kwa kupeana mikono na wanawake hao, mmoja wao alimwambia ajitoe kitu katika sikio na mara baada ya kufanya kitendo hicho alihisi mwili kupata ganzi na hivyo kupoteza fahamu papo hapo.
Alisema baada ya kuhakikisha amezimia inavyoonekana watu hao walimfunga kamba mikononi na miguuni na kisha kitambaa usoni na kwenda naye kusikojulikana.
“Baada ya muda mchache kupita Mgoba alipata fahamu na kujikuta akiwa amefungwa kamba pamoja na kitambaa usoni na hakujua anakopelekwa, ila alisema wakati huo alihisi wanaingia kwenye bonde ambako walimshusha,” alisema.
Alisema walipomshusha walianza kwa kumpiga, huku wakimtaka ataje ni nani aliyemtuma kuandamana kati ya Ukawa au Lowassa?
“Aliposhindwa kusema aliyemtuma ndipo walipombana sehemu za siri, vidole na mbavu na kisha kumpiga mateke na baada ya kumuona ameishiwa nguvu wakamvua nguo na kumlazimisha afanye tendo la ndoa na mmoja wa wanawake hao,” alisema.
Alisema walipoona ameshindwa kufanya tendo hilo wakamnyoa nywele na kisha kuanza kutafuta mshipa uliopo pembeni ya paji la uso, lakini walishindwa kuupata na hivyo kuamua kumchoma sindano mkononi.
“Walihakikisha hana nguvu, ndipo walisikika wakisema wamemaliza kazi, hivyo wakamchukua na kumtupa msitu wa Mailimoja wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.
“Akiwa msituni alijisikia kupata fahamu, ambapo alianza kutambaa kuelekea barabarani ambako msamaria mwema mmoja alimuona na kisha kumpeleka Kituo cha Polisi cha Mailimoja, Kibaha,” alisema.
Alisema Polisi wa Kibaha ndio waliochukua jukumu la kumpeleka katika Hospitali ya Tumbi saa nne usiku, kabla ya kufanya uamuzi mwingine wa kuwasiliana na ndugu pamoja na jamaa zake.
Kwa mujibu wa Bakari, polisi hao baada ya kufanya mazungumzo na ndugu wa Mgoba kwa minajili ya kumhamisha hospitali ili apatiwe matibabu zaidi, badala yake walimpeleka katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central) kilichopo jijini Dar es Salaam.
“Cha kushangaza huko Central walimuweka rumande na baadaye walimtaka atoe maelezo pasipo kujali hali aliyokuwa nayo,” alisema.
Alisema baadaye polisi huo walimruhusu Mgoba kuondoka na kumpatia Sh 2,000, ingawa wakati huo alikuwa akijisikia vibaya.
Inaelezwa kuwa baada ya kuruhusiwa hakufika mbali, alidondoka na alizinduka akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia magari ya polisi (defender) matatu na basi moja la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yakiwa yameegeshwa katika viunga vya hospitali hiyo.
Kitendo hicho kililalamikiwa na vijana hao kupitia kwa Katibu wake, Linus Steven, ambaye alisema kinatia shaka na kuonesha ubabe wakati awali walionekana kukwepa kumhudumia mwenzao.
Alilishutumu Jeshi la Polisi kutaka kutumia tukio hilo kama la kihalifu au kuna jambo la kuvunja amani.
MTANZANIA Jumamosi lilizungumza na mke wa Mgoba ambaye hata hivyo alikataa kutaja jina lake, ambapo alithibitisha kuwa siku ya tukio alikuwa pamoja na mume wake nyumbani na kwamba ilipofika saa 11:00 alimuaga anakwenda kwa rafiki zake.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, kuzungumzia tukio hilo, alikiri askari wake kumpokea Mgoba na kisha kumpeleka katika Hospitali ya Tumbi baada ya kumuona kuwa yupo katika hali mbaya.
Kamanda Matei alisema alipofikishwa katika hospitali ya Tumbi madaktari walithibitisha kuwa hana matatizo yoyote, na hivyo kuruhusiwa.
“Polisi wangu walimsaidia kutafuta ndugu zake na miongoni mwa waliofika ni mmoja aliyejitambulisha kama askari polisi na mwingine Usalama wa Taifa, aliyejitambulisha polisi alidai kuwa ni shemeji wa Mgoba, lakini yule aliyedai usalama wa Taifa alisema ni ndugu yake kwa hiyo sisi tuliishia hapo, hayo mengine siyafahamu, waulizwe polisi wa Dar es Salaam,” alisema Kamanda Matei.
Kwa upande wake, Kamada wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema ofisi yake ipo katika hatua za awali za upelelezi, ingawa kuna taarifa za kukanganya kuhusu kijana huyo.
Pamoja na hilo, Kova aliahidi kutoa taarifa kamili kuanzia leo baada ya kukamilisha upelelezi.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Meshack Shimwela, alisema hawezi kuzungumzia taarifa zozote za Mgoba mpaka hapo atakapopata taarifa kutoka kwa yeye mwenyewe au ndugu zake.
Daktari mmoja wa hospitali ya Amana aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina alisema mgonjwa huyo anaweza kuhamishiwa katika Hospitali ya Muhimbili kwa kuwa hospitali hiyo haina baadhi ya vipimo ambavyo vinaweza kubaini kitu kilichotokea kwenye damu yake baada ya kulalamika maumivu sehemu za siri na kudaiwa kuchomwa sindano.
Kwa mujibu wa daktari huyo, Polisi walitaka kuchukua jukumu la kumhamishia Muhimbili baada kumaliza dripu, lakini kumekuwa na mvutano mkubwa kati yao na ndugu zake.
Mpaka kufikia jana jioni, daktari huyo alisema kuwa hali ya mgonjwa huyo ilikuwa inaimarika, huku pia wakiwa wanasubiri kumpeleka Hospitali ya Muhimbili.
Tukio la kutekwa kwa kijana huyo limejenga hisia kwamba huenda kuna mpango unaandaliwa wa kummaliza nguvu kwa staili ile ile kama iliyotumika kwa Dk. Ulimboka.
Dk Ulimboka ambaye alikuwa akiongoza wenzake kudai haki za madaktari, alitekwa na kufanyiwa vitendo vya kinyama Juni 27, 2012, wakati Kibanda alifanyiwa vitendo vinavyofanana na hivyo Machi 5, 2013.
Mgoba ndiye kiongozi wa vijana zaidi ya 3,000 ambao wanaishinikiza serikali kuwapatia ajira wale wote waliopatiwa mafunzo JKT.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles