30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, August 9, 2022

Mwanafunzi aua mwenzake kwa kumchoma kisu

Walter Mguluchuma-Katavi

 JESHI la Polisi   Mkoa wa  Katavi, linamshikilia mwanafunzi wa  kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari ya  Kabungu  mwenye umri wa miaka 15 kwa tuhuma za kumuua   mwanafunzi mwenzake wa  kidato cha tatu mwenye umri wa miaka 17 kwa kumchoma kisu kifuani.

Inaelezwa chanzo cha mauaji hayo, ni ugomvi katia ya wanafunzi hao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 5 usiku Kijiji cha Kagwila wilayani Tanganyika.

Alisema wanafunzi hao  walikuwa wakiishi  chumba kimoja kutokana na nyumbani kwao kuwa mbali na shule.

Alisema pamoja na mtuhumiwa kusoma kidato cha tofauti na  marehemu na kuishi chumba kimoja, katika masuala ya chakula kila mmoja alikuwa anajitegemea kwa  kila kitu.

“Siku ya  tukio, marehemu  alidai alikuwa amenunua mafuta ya kula aina ya Korie mchana ya Sh 300 kwa ajili  ya kupikia  chakula  chake cha usiku.

“Alipotaka kupika hakuyaona mafuta hayo alipokuwa ameyahifadhi ndani ya chumba chao kitendo kilichosababisha kuibuka mzozo,”alisema.

Alisema  marehemu alipomuuliza  mwenzake kama ametumia mafuta hayo alikana na kwamba hajawahi kuyaona.

Kamanda Nyanda, alisema mzozo ulianza hapo kwa muda mrefu, huku mtuhumiwa akimtuhumu mwenzake kuwa amemwibia na ghafla wakaanza kupigana na mtuhumiwa alizidiwa nguvu na marehemu.

“Mtuhumiwa baada ya kuona amezidiwa nguvu na mwenzake, alichukua kisu na kumchoma nacho kifuani upande wa kushoto, marehemu alipiga yowe akiomba msaada, majirani walifika eneo hilo la tukio. “Walipofungua mlango kwa nguvu walikuta  marehemu akigalagala sakafuni  huku damu ikiwa imetapakaa,”alisema Kamanda Nyanda .

Alisema majirani walipojaribu kumkimbiza hospitalini kwa matibabu waligundua  amekata roho .

“ Mwili wa marehemu umehifadhiwa  Hospitali Teule ya Rufaa Mkoa wa Katavi mjini Mpanda na baada ya kufanyiwa uchunguzi tutawakabidhi ndugu kwa ajili ya mazishi,”alisema.

Hili ni tukio la pili la kutokea kwa  vifo vya wanafunzi kwa kipindi cha wiki moja, ambapo hivi karibuni mwanafunzi wa  kiume aliyekuwa anasoma darasa la  saba Shule ya Msingi Ifukutwa  Wilaya ya Tanganyika alijinyonga hadi kufa kutokana na ugumu wa maisha kwa madai wazazi wake walishindwa kumpatia mahitaji ya msingi na kulazimika kufanya vibarua ili ajikimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,291FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles