25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanafunzi aliyejikita katika uimbaji kukemea unyanyasaji

Jamal Said
Jamal Said

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

WATU wenye ulemavu wamekuwa wakikabiliwa na vitendo vya kubaguliwa mara kwa mara katika maisha yao, ambapo wengi wao wamekuwa wakitengwa na kukataliwa kutokana na ulemavu wao.

Inaelezwa kuwa takribani asilimia kumi ya idadi ya watu wote duniani ni walemavu. Idadi kubwa ya walemavu wamekuwa wakijikimu maisha yao kwa kuombaomba hasa barani Afrika.

Hata hivyo, baadhi ya walemavu  wamekuwa wakifungiwa majumbani na familia zao, wakichukuliwa kuwa watazitia aibu familia zao.

Katika mataifa mengine huona ulemavu kuwa ni laana kutoka kwa mizimu ya mababu zao.

Ingawa ipo mikataba iliyoundwa ya kuwalinda, lakini bado  wameendelea kukumbana na vizuizi katika jamii wakitengwa  katika maisha ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.

Matukio ya unyanyasaji dhidi ya watu wenye ulemavu ni suala ambalo watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakilivalia njuga na kulipigia kelele kila kukicha.

Kwa mfano; hivi majuzi tumesikia habari ya kufichwa kwa mtoto mmoja mlemavu ndani ya nyumba huko mkoani Morogoro.

Jamal Said ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kinondoni anasema huwa anaumizwa mno na watu wanaowanyanyasa wenye ulemavu.

“Unajua hawakupenda au kumuandikia Mwenyezi Mungu wawe walemavu na hata siku moja hakuna mtu yeyote anayejua lini atakuwa mlemavu hivyo naweza kusema kila mmoja ni mlemavu mtarajiwa, kwa kweli huwa najisikia uchungu nikiona mtu anamnyanyasa na kumnyanyapaa mlemavu.”

Ndivyo alivyoanza kunieleza mwanafunzi huyo ambaye amejaliwa kipaji cha kuimba na kucheza.

“Napenda masomo ya Kiswahili, Hisabati, Kiingereza na Sayansi, natumia kipaji changu kila ninapopata nafasi ya kupanda jukwaani kuelimisha jamii iache kufanya unyanyapaa dhidi ya walemavu,” anasema.

Anaongeza: “Ni jambo linaloniumiza,  kwanini watu wengine hawana huruma, kwa sababu walemavu nao ni binadamu kama wao na wanahitaji upendo kama wengine,” anasema

Anasema si jambo jema kuwatenga, kuwatukana, kuwanyanyasa badala yake wanastahili kupendwa kwa dhati na kuheshimiwa kama wanadamu wengine.

“ Baadhi ya wazazi wenye watoto walemavu wamekuwa wakiwaficha ndani eti wanakwepa aibu hii si sahihi…  wawapeleke shule ili nao wapate kuelimika kama watoto wengine,” anasema.

Anasema amepanga kuja kuwa balozi wa walemavu na kutumia kipaji chake hicho kuelimisha jamii.

“Lakini kwa sasa nawekeza nguvu zangu katika kusoma kwa bidii ili niweze kufaulu vema masomo yangu lakini nitakapomaliza napenda niwe balozi wa walemavu.

“Kupitia nyimbo zangu nitahakikisha naelimisha jamii iache tabia hii ya unyanyapaa dhidi ya watu wenye ulemavu kwa kuwa ni jambo ambalo naamini halimpendezi hata Mwenyezi Mungu aliyetuumba sisi wote,” anasema.

Kwa kawaida wanadamu huwa tunapenda kujifunza jambo kutoka kwa watu waliofanikiwa kimaisha. Ndiyo maana huwa tunachagua marafiki wazuri na kujifunza kwao jinsi walivyoweza kufanikiwa katika mambo mbalimbali.

Said anasema anavutiwa na kipaji cha muimbaji Hamonize na kwamba amekuwa akijifunza mengi kutoka kwake yakimsaidia kukuza kipaji chake.

“Napenda niwe hodari katika uimbaji na kucheza muziki, fedha nitakazokuwa napata nitaenda pia kuwasaidia wasiojiweza hasa walemavu na wazee ambao ni tunu ya Taifa letu na wamefanya kazi kubwa ya kuijenga nchi hii,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles