Na Ibrahim Yassin, Busokelo
UONGOZI wa Shule ya Sekondari Mwatisi Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, umemfukuza mwanafunzi mmoja (jina tunalo) kwa madai ya ushirikina.
Mwanafunzi huyo anadaiwa kuhusika na kitendo cha baadhi ya wanafunzi shuleni hapo kukumbwa na matatizo ya kuanguka na mapepo kwa muda wa miezi miwili mfululizo.
Mwanafunzi huyo pia anahusishwa na mzuka wa ajabu uliotokea hivi karbuni, ambapo ulikuwa ukianua vyakula vya watu wakati wakianika nje, huku ukiwakumba wanafunzi wa kike waliokuwa wakikimbilia porini na kuzua taharuki kwa wakazi wa eneo hilo.
Hali hiyo ilisababisha uongozi wa shule hiyo kuitisha mkutano wa hadhara ulioshirikisha viongozi wa dini, machifu na watu wengine, lengo likiwa ni kufikia mwafaka wa sakata hilo.
Furaha Mwakalundwa, Mwinjilisti wa Kanisa la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Konde Jimbo la Mwakaleli, alisema kufukuzwa kwa mwanafunzi huyo hakuwezi kuleta tija kutokana na kwamba masuala ya ushirikina hayana uthibisho.
“Siku zote masuala ya ushirikina hayana uthibitisho, hivyo ni vyema hii kazi wangetuachia watumishi wa Mungu, ili tuendelee kuitatua kwa nguvu za Mungu. Kumwondoa mwanafunzi huyo hatuwezi kujua kama kweli ni mhusika au laa,” alisema Mwakalundwa.
Baadhi ya wanafunzi walisema kuondolewa kwa mwanafunzi mwenzao kumeleta faraja kutokana na hali hiyo kupungua kwa asilimia 90 ukilinganisha na awali.
“Alikua akiingia tu darasani au kila anapokutana na mwanafunzi yeyote walikuwa wakianguka na kupata kama kichaa na kuanguka na kusababisha wanafunzi na walimu kumchukia,” alisema mmoja wa wanafunzi katika shule hiyo.
Walimu na wanafunzi walikuwa wakimwogopa na kumkimbia kila anapoonekana ikiwamo kuogopa kumpatia adhabu wakihofia kukumbwa na sintofahamu hiyo.
Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, Japhet Boniface, licha ya kukiri kuwepo kwa adha hiyo, alisema kwa sasa hali iko shwari ukilinganisha na alipokuwepo mwanafunzi huyo.
“Vitendo kama hivyo vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara kitu ambacho kinatupa wakati mgumu kujua ukweli wa jambo hilo,” alisema.
Mkuu wa Shule hiyo, Eliza Halinga, alisema mwanafunzi huyo hajafukuzwa shule isipokua uongozi uliamua kumhamishia shule nyingine ili kunusuru hali yake kutokana na kila mwanafunzi kumchukia, hali iliyosababisha wanafunzi na walimu wengi kutofika shuleni kwa hofu.
“Tuliamua kumwita mzazi wake ili kuongea nae ili tuweze kumhamishia shule nyingine kwani kila mwanafunzi alikuwa akimchukia kutokana na kunguka kwao, pia licha ya kunguka kwao lakini kila akikutana na wanafunzi wenzake walikuwa wakianza kuanguka na kujipigapiga,” alisema Halinga.