30.2 C
Dar es Salaam
Friday, May 3, 2024

Contact us: [email protected]

MWANA MFALME KUIJENGA  KIUCHUMI SAUDI ARABIA MPYA

Na Balinagwe Mwambungu


UNAWEZA ukasema kwamba Saudi Arabia inajengwa upya, baada ya Mwana wa Mfalme Abdullah Salman, kuanika mpango kabambe wa Visheni 2030 ambao utaufumua mfumo wote wa utawala wa kifalme ikiwa ni pamoja na uchumi wanchi hiyo ambao unategemea rasilimalimoja tu—mafuta. Hii imetokana na ukweli kwamba tangu mwaka 2014, bei ya mafuta imekuwa ikishuka, kitu ambacho kinasababisha kuyumba kwa mapato ya serikali. Asilima 90 ya mapato ya serikali hutokana na mafuta na asilimia 80 ni mapato kutokana na mauzo ya nje.

Prince Mohammed bin Salman, ametangaza mabadiliko makubwa ambayo wachambuzi wa mambo wanasema yatafuta ‘ukuukuu’ wa ufalme na kuifanya Saudia kuwa miongoni mwa nchi za kisasa duniani.

Prince Mohammed amepania kuifanya Saudia  iendane na matarajio ya usasa wa vijana wa nchi hiyo ili ifanane na nchi zingine duniani. Vijana wanataka nchi yao iachane na mambo ya kizamani na kuijenga Saudia mpya—ya kisasa na yenye uwazi zaidi.

Inaelezwa kwamba Prince Mohammed (32), anakusudia kuifanya Saudia iachane na msimamo mkali wa kihafidhina na irejee kwenye msimamo wa kati (moderate) wa dini ya Kiislamu. Mohammed na kundi lake la vijana wanaamini kwamba kwa mtizamo huo mpya, utafungua milango kwa wawekezaji wa kigeni.

“Tunarudi vile tulivyokuwa zamani—nchi inayofuata  Uislamu wa kati ambao ulikuwa wazi kwa dini zote na kwa mataifa yote,” Prince Mohammed alisema wakati akihutubia mkutano wa wawekezaji ulilofanyika mji mkuu Riadh hivi karibuni.

“Hatutatumia miaka 30 ijayo ya maisha yetu kujishughulisha na mawazo ya kidhalimu. Tunayaacha mara moja. Tutauzika msimamo mkali hivi karibuni,” alisema.

Wachunguzi wa mambo wanatafsiri hotuba ya Mwana wa Mfalme wa Saudia kama mpasho dhahiri kwa viongozi wa kidini wahafidhina, ambao kwa miongo mingi wamekuwa na ushawishi mkubwa kwenye sera za nchi hiyo.

“Tunataka kuishi maisha ya kawaida. Maisha ambayo kwayo dini yetu inataka uvumilivu na upole wa  mila na desturi zetu,” alisema Prince Mohammed.

“Asilimia sabini ya Wasaudi ni vijana chini ya umri wa miaka 30, na kwa kweli hatutakaa kwa miaka 30 ijayo tukijishughulisha na mawazo yanayohimiza maangamizo. Tutayavunja mara moja,’’ alisema Mfalme huyo mtarajiwa.

 

“Tunarejea kwenye asili yetu—ya kuwa nchi yenye Uislamu wa kati, Uislamu ambao unatambua uwepo wa  dini nyingine na mila na desturi za aina zote duniani,” alisema.

Ingawa mashirika ya kimataifa na makundi ya haki za binadamu yamekuwa yakiikosoa vikali Saudia, Prince Mohammed ameendelea kuleta mabadiliko tangu alipoteuliwa kushika madaraka mwezi Juni, mwaka huu.

Saudia ilikuwa hairuhusu mambo yanafanyika nchi zingine duniani—unywaji wa pombe, na vilabu vya usiku. Wanawake kwenda shule na kuendesha magari. Wanawake lazima wavae hijabu, walikuwa hawaruhusiwi kuhudhuria shajara bila kufuatana na mwanaume.

Aidha baadhi ya wawekezaji wa kigeni walikuwa wanakwazwa na masharti ya serikali—kwamba mkandarasi wa kigeni ni lazima agawe asilimia ya thamani ya kazi anayopewa kwa makampuni ya ndani. Mkandarasi lazima aajiri idadi kubwa ya Wasaudi, masharti magumu ya visa ya kuruhusu kufanyakazi Saudia na kwa ujumla ubaguzi wa jinsia katika biashara na mambo ya kijamii.

Lakini hivi karibuni, viongozi wanashindana kulegeza msimamo, kumekuwa na mabadiliko katika baadhi ya sekta. Majumba ya sinema na dansi ambayo yalikuwa yamepigwa marufuku, yananza kufunguliwa. Msimamo huu mpya ni sehemu ya mabadiliko ya sera ya kihafidhina ya nchi  hiyo. Wachunguzi wa mambo wanatabiriwa kwamba mabadiliko hayo, huenda yakaitikisa nchi na kuchangia mabadiliko na mtizamo wa kitamaduni wa nchi hiyo.

Inaaminika kwamba Mohammed ndiye aliyemshauri Mfalme Abdullah Salman  kufuta katazo la miaka mingi la kutowaruhusu wanawake kuendesha magari mwezi uliopita.

Hivi karibuni, Mfuko wa Uwekezaji wa Saudi (Public Investment Fund), ulio chini ya Prince Mohammed, ulitangaza kuanzishwa kwa ukanda huru wa kiuchumi (free economic zone) Kaskazini-Magharibi ya ufukwe wa Bahari ya Shamu. Imeelezwa kuwa ukanda huo maalumu, kutajengwa jiji jipya na kubwa (megacity) kwa ya Dola za Kimarekani bilioni 500. Jiji hilo  litaendeshwa kwa sheria tofauti na sheria za sasa za Saudia. Mradi huo utachechemua uchumi wan chi hiyona kutoa ajira nyingi kwa vijana na wageni kwa kuwa na maono mapya.

Lakini pamoja na mambo haya mazuri, inaripotiwa kwamba utawala wa Saudia umeongeza ukandamizaji wa haki za binadanu na kuwasulubu wanaharakati.  Mwezi uliopita, ilitangazwa kwamba zaidi ya wanaharakati 20, pamoja na wahubiri  maarufu wa dini wawili, walikamatwa na kuwekwa ndani bila kuwafungulia mashitaka yoyote.

Abdul Aziz (27), mmoja wa washauri wa sera wa Prince Mohammed, anaunga mkono kuwa anatekeleza yale yanayowezekana katika ufalme mgumu ‘rigid’ wa Saudia. Anampongeza kwa kuzungumza moja kwa moja na wananchi kwa njia ya televisheni na kutilia mkazo mambo ambayo yanaonesha kizazi kipya kana kwamba kilitelekeza uhalali wake wa kuleta maendeleo.

“Inaonesha kwamba mabadiliko ya kisiasa na kijamii nchini Saudi Arabia sio mapya, bali Saudi Arabia inarejea kwenye mizizi yake ya zamani—ya Uislamu wa kati wa jamii yenye uvumilivu na kustahiana,” anasema Abdul Aziz.

Prince Mohammed, maarufu kama MBS, anasema atahakikisha kuwa nchi yake inayasahau mambo ya 1979, akimaanisha kuzuka kwa Uislam wa kisiasa baada ya kuuliwa kwa Mfalme Faisal mwaka 1975.

Katika miaka ya 1970 kulifanyika mabadiliko mengi nchini humo, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa vituo vya televisheni na shule za wasichana.

Lakini familia ya Al-Sheikh, ambayo ndio mhimili na mdhibiti wa mambo ya kidini na kijamii katika familia ya nyumba ya Al-Saud, inakazia sera za kihafidhina.

Mkutano wa siku tatu wa wawekezaji ambao ulijadili mambo ya kiuchumi, ulihudhuriwa na wajumbe 2,500, pamoja na wawekezaji wa kigeni 2,000.

Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo kutoka Marekani, alisema kwamba alivutiwa na visheni ya Prince Mohammed.

“Hotuba yake inapeleka ujumbe mzito sio tu kwa Wasaudia, bali pia kwa dunia nzima kwamba ufalme umepania kufanya mabadiliko,” alisema mjumbe huyo.

 

*Imendikwa  na msaada wa mitandao

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles