22.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 11, 2024

Contact us: [email protected]

MVUA YAUA BIBI NA WAJUKUU

NA RAMADHAN HASSAN-MPWAPWA

WATU  wanne wamefariki dunia, watatu wakiwa wa familia moja katika Mtaa wa Majumbasita Kata ya Mpwapwa Mjini, wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma kwa kusombwa na maji, kutokana na mvua kubwa iliyonyesha jana wilayani hapa.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dk. Saidi Mawji alwataja waliofariki dunia kuwa ni Marita Mabula (60), Shukuru Mabula(15) Bernadetha Mabula (7) wote wa familia moja na Jesca Lubeleje (19)

Dk. Mawji alisema waliipokea miili hiyo  asubuhi ya jana ikapelekwa Hospitali ya Benjamini Mkapa na Jeshi la Polisi wilayani Mpwapwa.

“Asubuhi ya leo (jana) tumepokea miili ya watu wanne ambao kati ya hao watatu ni ndugu ambao ni bibi na wajukuu zake wawili,”alisema.

DIWANI ASIMULIA

Diwani wa Kata ya Mpwapwa Mjini, George Fuime (CCM) akisimulia tukio hilo alisema wakati linatokea jumla ya watu watano walikuwa katika nyumba hiyo.

Alisema watu watatu walifariki kwa kusombwa na maji huku wengine wawili wakijiokoa kwa mmoja kupanda juu ya mbuyu huku mwingine akikimbilia katika nyumba ya jirani.

Fuime alisema watu watatu waliofariki ni wa familia moja ambao ni bibi aliyekuwa na wajukuu zake wawili, huku mwili mwingine wakiuokota katika maeneo ya jirani na nyumba iliyosombwa na maji.

“Waliofariki ni bibi aliyekuwa na wajukuu zake wawili, hawa wengine wawili walijiokoa kwa mmoja kupanda katika mbuyu ambao upo jirani na nyumba hiyo huku mwingine akikimbia kwa majirani.

“Huyu wa nne aliyefariki mwili wake tuliuokota jirani na nyumba yake katika eneo hilo hilo,”alisema.

Alisema baba wa familia hiyo ni mfugaji hivyo wakati tukio hilo linatokea hakuwepo kwani alienda makambini nje ya Mpwapwa.

Diwani huyo alisema siku tatu kabla ya kunyesha kwa mvua hiyo walifanya maombi ya kumuomba mungu awapatie mvua.

“Haya nadhani ndio malipo ya maombi yetu ila kila kitu anapanga Mungu’’ alisema.

Fuime ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpwapwa alisema kutokana na tatizo hilo halmashauri imejitolea kutoa majeneza.

Alisema miili hiyo inatarajiwa kuzikwa leo (Jumatano) katika makaburi ya Ilolo Kati wilayani humo.

MAJIRANI WASIMILIA

Wakizungumza  na MTANZANIA majirani wa mtaa huo au maarufu kwa jina la Ilolo Kati  walisema watu hao wamefariki kutokana na kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha juzi kuanzia saa 5 usiku.

Mmoja wa majirani hao ambaye alijitambulisha kwa jina la Masha Ilunda alisema mvua hiyo ilidumu kwa zaidi ya saa tano.

Alisema familia iliyosombwa na maji ilikuwa ikiishi katika eneo ambalo linabonde hivyo mvua ilivyozidi maji yalikuwa yakikimbilia katika nyumba hiyo.

Naye Mwajuma Matonya alisema kilichowaokoa wao ni kutokana na kuchelewa kulala hivyo mvua ilivyozidi kuwa kubwa wakaamua kukimbia katika eneo hilo na kwenda katika nyumba ambazo zipo juu.

Naye Issa Shija alisema walishaambiwa wahame katika eneo hilo lakini wakakaidi agizo la Serikali na sasa yamewakuta lakini akaiomba Serikali iwasaidie ili waweze kutengeneza nyumba zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles