23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

MUUJIZA WA LISU

Na AGATHA CHARLES -DAR ES SALAAM

BAADA ya siku 15 tangu watu ambao vyombo vya dola havijawabaini hadi sasa wamshambulie kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe,  aliyekuwa amemsindikiza katika matibabu nchini Kenya amerejea na kueleza mambo mengine mapya.

Mbowe aliyezungumza na vyombo vya habari jana katika mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Chadema yaliyopo Kinondoni, Dar es Salaam alieleza kwa namna nyingine kabisa kuhusu mwenendo wa tukio lililotaka kuchukua maisha ya Lissu pia na maendeleo ya afya yake kwa sasa.

Hali ya Lissu

Kuhusu mwenendo wa afya ya Lissu kwa sasa, Mbowe alianza kwa kusema:

“Lissu anawasalimu sana, na hii ni kauli thabiti kabisa, niliachana naye Nairobi jana (juzi) mchana, na nikamwambia nitazungumza na Watanzania. Akaniomba niwapelekee salamu zake kwamba Mungu anaendelea kumpigania.”

Mishipa ya Fahamu

Mbowe alisema madaktari wanaomtibu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya, walishangaa licha ya Lissu kushambuliwa kwa risasi kadhaa katika mwili wake lakini alitoka pasipo kuharibika mishipa ya fahamu.

Ingawa hakutaja idadi ya risasi zilizompata Lissu katika shambulio hilo lililotokea Septemba 7, mwaka huu mjini Dodoma alikokuwa akihudhuria vikao vya Bunge, Mbowe alisema madaktari wameliona jambo hilo kama ni muujiza.

“Madaktari wanasema ni miujiza kwa mashambulio yale mtu akatoka salama bila nerves (mishipa ya fahamu) zake kuwa zimekatwakatwa na risasi, hakuna nerve yake hata moja imeguswa na risasi.

“Kuna maeneo mengine risasi imepita juu na nyingine ikapita chini ya nerve ikabaki katikati inaning’inia. Yote ni mipango ya Mungu,” alisema Mbowe.

Kukata Kauli

Mbowe alitumia pia nafasi hiyo kuweka sawa kile ambacho kimepata kusemwa au kuandikwa awali kuhusu Lissu kukata kauli.

Kwa maneno yake mwenyewe Mbowe alisema:“Lissu hakukata kauli hadi anaingia theater (chumba cha upasuaji) pamoja na majeraha yote, ambacho wananchi nataka waelewe kuna tofauti ya kukata kauli na kupewa dawa za usingizi kutokana na wingi wa majeraha, hiyo ndiyo hali iliyomtokea Lissu,”

Katika hilo Mbowe alisema fahamu na akili za Lissu ziko timamu kwa asilimia 100.

“Ninawahakikishia Watanzania mashine yetu itarudi barabarani ikiwa sahihi na timamu,” alisema Mbowe.

Jopo la madaktari tisa

Mbowe alisema Lissu anatibiwa na jopo la madaktari tisa na manesi kadhaa tangu alipofikishwa katika Hospitali ya Nairobi kwa matibabu.

Mbowe alilitaja kundi hilo kuwa linaongozwa na Daktari Mkuu, Vincent Moki Mutisu, Dk. Khan, Dk. Khaisha, Dk. Mongela, Dk. Kisyoka ambaye ni daktari wa moyo, na timu ya madaktari wengine watatu waAnxiety ambao ni Dk. Kibeti, Dk. Aruga na Dk. Gasii na kuna Dk. Nangole wa  upasuaji pandikizi (plastic surgery).

Alisema taarifa ya madaktari ambayo tayari wamepewa ni siri lakini hali ya Lissu imeimarika na kwamba hofu ya kupoteza uhai dhidi ya shambulio hilo haipo tena.

Wakati akizungumzia hilo, awali Mbowe aliwashukuru madaktari wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwamba kama wasingefanya wajibu wao wa msingi, Lissu asingeweza kusafirishwa na kufika Nairobi akiwa hai.

“Kazi kubwa iliyofanywa na madaktari wa Dodoma tusiwapuuze kabisa, ndiyo iliyotuwezesha sisi kumfikisha Nairobi bado akiwa hai. Ilikuwa ni miujiza kila mmoja alishangaa, madaktari walishangaa, kuwa huyu mtu kwa shambulio hili, kwa majereha haya bado anapumua lakini mipango ya Mungu ni mikubwa kuliko ya wahalifu na tunashukuru kwa waliyoyafanya madaktari, kum- stabilize, na sie tukapambana usiku kwenda Nairobi, wengine wakishika damu, maji na kumfikisha. Tunamshukuru Mungu” alisema Mbowe.

Asilimia 95 ya damu ngeni

Kuhusu kiasi cha damu aliyoongezewa, Mbowe alisema asilimia 95 imetoka kwa watu mbalimbali, Dodoma, Nairobi na kwingine.

Kuchangia damu kila Jumapili

Mbowe alisema kila siku ya Jumapili kundi la Watanzania na Wakenya wamekuwa wakijitokeza kutoa damu kwa ajili ya Lissu nchini Kenya.

Alisema kutoa damu ni kielelezo cha kulinda uhai wa mtu kwa sababu isingetolewa Lissu asingekuwa hai.

Wakati Mbowe akieleza hayo kwa upande wa Kenya kwa Tanzania alionekana kusikitishwa na vyombo vya dola kwa kuzuia maombi kwa Lissu huku watu takriban 18 waliotaka kuchangia damu kwa upande wa Wilaya ya Temeke wakiishia kulala polisi siku mbili wakidaiwa kupanga uhalifu.

Hospitali sita nje

Akizungumzia kuhusu jitihada za watu mbalimbali kutaka Lissu atibiwe nje ya nchi, akiwamo Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyarandu, Mbowe alisema kulikuwa na maombi kutoka katika nchi sita tofauti kutaka kumtibu mwanasiasa huyo.

“Kuna kundi lilitaka apelekwe Afrika Kusini, lingine India, Watanzania wanaoishi Belgium waka-offer, mleteni huyu mtu tutaangalia namna ya kumsaidia, kundi lingine likawa linashughulika kumpeleka Ujerumani, lingine Uingereza na Marekani,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema pamoja na nia njema ya makundi hayo lakini kikao kikubwa cha tathimini ya hali ya mgonjwa kilichofanyika siku tatu zilizopita kikimshirikisha yeye mwenyewe, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji na familia ya Lissu akiwamo mke, kaka na dada yake, ilielezwa na timu ya madaktari kuwa bado mgonjwa hahitaji kusumbuliwa.

Alisema madaktari hao waliwahakikishia kuwa wana vifaa, uwezo na utaalamu wa kukamilisha awamu ya pili ya matibabu ya Lissu akiwa nchini Kenya.

Akifafanua hilo, Mbowe alisema awamu ya kwanza iliyofanywa Hospitali ya Dodoma ilikuwa ni kumuimarisha ili aweze kufikishwa hospitali rasmi.

Awamu ya pili ilikuwa ni ya kuokoa maisha ya Lissu, kutibu na kufanya upasuaji wa maeneo husika na kuhakikisha kuwa anarudi katika hali ya utimamu wa kutoka hospitali itakayofanyika hapo hapo Nairobi.

Mbowe alisema awamu ya tatu ambayo itachukua muda mrefu itahusisha mazoezi na namna ya kumrudisha katika hali ya kawaida kwa namna alivyoumizwa.

“Wakati huo ukifika ndio tutafikiria huyu mtu aende wapi, Marekani, Uingereza, Ujerumani, aje nyumbani, itategemea mazingira ya wakati huo, itakuwa ni jambo linalomrudisha katika utaratibu wake wa kimaisha, baada ya kupitia majeraha makubwa,” alisema Mbowe.

Ugeni wasitishwa

Mbowe pia alisema katika kikao hicho cha tathimini kuhusu hali ya Lissu kilihitimishwa kwa kusitisha wageni kutoka ndani na nje ya nchi kuendelea kumtembelea.

Alisema uamuzi huo ulichukuliwa ili kumpa muda wa kupumzika katika chumba maalumu cha uangalizi (ICU).

Alisema Lissu yuko kwenye ulinzi mkali wa saa 24 na usalama wa ndani na nje ya hospitali hiyo umeimarishwa.

Msemaji pekee wa Lissu

Mbowe alisema kumekuwapo kauli nyingi kuhusu hali ya Lissu na kwamba jambo hilo si suala la kuuzia magazeti au kutafuta umashuhuri mitandaoni.

“Jambo hili limesababisha usumbufu mkubwa si tu kwa familia ya Lissu lakini hata wanachama wetu na hatimaye hata wale madaktari wanaomtibia katika Hospitali ya Nairobi, wameleta malalamiko rasmi wanalalamika vyombo vya habari vya Tanzania, vingi vimekuwa vikipotosha kwa makusudi taarifa mbalimbali kuhusu hali ya Lissu,” alisema Mbowe.

Alisema aidha wapo watu waliofika hospitali na kufanikiwa kumwona Lissu au kutomwona lakini wanatoka na kuongeza chumvi au kueleza taarifa ambayo si sahihi.

“Nawaomba Waandishi wa Habari, viongozi wenzangu tuungane katika hili kwamba taarifa za ndani za hali ya mgonjwa zitolewe na wale walio na mamlaka karibu yake sana lakini taarifa Lissu leo amekaa, leo amekula ugali,hizi ni habari za uongo ambazo zinaleta usumbufu mkubwa kwa Watanzania.

“Nisisitize tu taarifa rasmi za chama zitatolewa na mimi mwenyewe aidha nikiwa Dar es Salaam ama nikiwa Nairobi,” alisema Mbowe.

Gharama za matibabu jumla Sh milioni 167

Kuhusu gharama zilizotumika kumtibu Lissu hadi kufikia jana asubuhi zilikuwa ni Sh 7,400,000 za Kenyaambazo ni sawa na Sh 162,800,000 za Tanzania hii ni mbali na zile za ndege na madaktari.

MICHANGO ILIYOPATIKANA

Mbowe pia aliweka hadharani taarifa ya michango iliyokusanywa kutoka kwa watu mbalimbali ambayo jumla kuu imefikia Sh 214,508, 686.

Kwa mujibu wa Mbowe, mchanganuo wa michango hiyo ni kama ifuatavyo;

Wabunge wa Chadema kila mmoja alitoa Sh 1,000,000 na kufanya jumla walizotoa kufikia Sh 48,468,000 na bado inaendelea kukusanywa.

Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko, ambaye alichaguliwa kukusanya michango kupitia simu yake, zilipatikana Sh 24,200,000 huku Shmilioni 52 zikichangwa na wananchi kupitia benki ya CRDB.

Katika mchango mwingine kila mbunge wakiwamo wale wa Chadema walichangia tena Sh milioni 43 na kufanya jumla kuwa Sh milioni 167.

Alisema michango mingine ya Watanzania wanaoishi Marekani kupitia kampeni ya mtandaoni iliyopewa jina la Go fund me iliyofanyiwa kampeni zaidi na Mange Kimambi na Wema Sepetu ilikusanya Dola 20,387.39 za Marekani baada ya kukata makato ya ada zilizoingia hospitali moja kwa moja.

Alisema makundi mengine kama Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS ) ilitoa Dola 9,005za Marekani zilizokwenda moja kwa moja hospitali.

Mbowe alisema Sh milioni 43 zilizochangwa na wabunge wote hazijapokelewa kwenye akaunti ya matibabu ya Lissu ambayo Spika wa Bunge, Job Ndugai, alipatiwa.

Hata hivyo, baadaye Bunge lilitolea ufafanuzi suala hilo kupitia kitengo chake cha Habari, Elimu kwa Umma na Mawasiliano likisema kuwa fedha hizo zilizochangwa na wabunge Sh milioni 43 kwa ajili ya kusaidia matibabu ya Lissu zilikuwa tayari zimetumwa katika akaunti ya Hospitali ya Nairobi anakopatiwa matibabu.

AMSHANGAA WAZIRI WA AFYA

Mbowe pia alirejea kile kilichopata kuzungumzwa mwanzo na kutolewa ufafanuzi kuhusu utaratibu wa Bunge kutaka kumtibu Lissu ambao wao waliukataa.

Mbowe alishangaa Lissu kuwekewa utaratibu wa kuchaguliwa hospitali ya Muhimbili kisha nchini India wakati baadhi ya wabunge wamekuwa wakitibiwa katika maeneo tofauti duniani.

Pamoja na hilo Mbowe pia alieleza kushangazwa na kauli iliyotolewa juzi na Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Ummy Mwalimu,kuiomba familia kupeleka maombi juu ya matibabu ya Lissu na kwamba ipo tayari kugharamia nchi yoyote duniani.

“Serikali haiwezi kukwepa fedheha na aibu katika hili, hatuwezi kupiga magoti,” alisema Mbowe.

TUKIO, Chadema kuhusishwa

Mbowe kwa mara nyingine alielezea namna tukio hilo lililovyoibua maswali mengi ikiwamo wao wenyewe kuhusishwa.

Katika hilo alisema kuna mkakati unatengenezwa wa kusema Chadema wamehusika kwa sababu ya kugombania vyeo.

Mbowe alisema huo ni upumbavu kwa sababu wao hawana utamaduni wa kugombea vyeo na kwamba ni mtu mjinga anaweza kufikiria kitu kama hicho.

Mashirika ya kuchunguza

Katika hilo alisema wanaomba vyombo vya nje vije kuchunguza tukio hilo ikiwamo kuwachunguza wao wenyewe, ili ukweli ufahamike.

Alisema kwa sasa hawana imani na vyombo vya uchunguzi vya hapa nchini.

Alisema hapingani na kauli ya Jaji Mkuu,Profesa Ibrahim Juma kuwa vyombo vya ndani havijashindwa kufanya uchunguzi lakini mtuhumiwa namba moja ni vyombo vya ulinzi na usalama.

“Suspect namba moja kwenye shambulio la Lissu ni vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi, hilo nalisema bila kumumunya maneno. Viashiria vyote vya tukio lile tangu linatokea, kauli za viongozi, kusita kwa viongozi na baadaye kauli za kujiosha na mazuio yasiyo na mantiki, mtu yeyote mwenye akili timamu atasema suspect ni vyombo vya ulinzi na usalama, sasa ni nani, simjui mimi. Lakini ni vigumu sana kusema ni tukio la kijambazi,” alisema Mbowe.

Alisema hadi wao kudai vyombo huru vya uchunguzi vilitokana na madhira ya muda mrefu ambayo vyombo vya ndani vya ulinzi na usalama havina msaada katika hilo.

Katika hilo, Mbowe alikumbushia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, ambaye alidai waliomshambulia wanajulikana na hakuna aliyefikishwa mahakamani.

Zaidi alikumbushia kupotea kwa msaidizi wake, Ben Saanane na kwamba alimuuliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Serikali kuruhusu uchunguzi huru kutoka Scotland Yard lakini alikataa.

“Na hata sasa tumezungumza na vyombo vya uchunguzi vya Marekani, Uingereza, Ujerumani viko tayari kuja kutoa msaada, wakasema tupeni maombi kutoka Serikali ya Tanzania… ruhusuni, kama mnajiamini hawa watu waje kufanya uchunguzi, msibaki tu mnasema ni Chadema wenyewe kwa wenyewe, ruhusuni watu wenye utaalamu wao waweke vielelezo hapa,” alisema Mbowe.

Katika hilo alimtaka Jaji Mkuu kutoingilia suala la uchunguzi na kwamba yeye abaki na mambo ya mahakama.

“Wawalete watu wa Scotland Yard, FBI, Israel, Ujerumani wako tayari kuchunguza wanaogopa nini? Kama hawana mawasiliano tutawapa na watakuwa chini yao,” alisema Mbowe.

Magari yalizingira gari la Lissu

Katika hatua nyingine, Mbowe alieleza namna watu waliomshambulia Lissu walivyojipanga na kusema kuwa lilikuwa kundi la watu wengi.

“Hawa watu hakuwa mmoja au wawili lilikuwa ni kundi la watu, Nissan ilikuwa na wawili, magari yalifunga kulia na kushoto. Masaa mawili ndio polisi wanafika eneo la tukio,”alisema Mbowe.

KUHUSU DEREVA

“Dereva yuko Nairobi anaendelea kufanyiwa counseling, madaktari wa akili wakiridhia yuko sasa timamu atarejea. Hatumfichi. Katika mazingira ya kiusalama na tukio, kuuwawa isingekuwa kazi ngumu.

“Wale watu waliopiga risasi hawakutegemea mtu angetoka hai. Dereva amekuwa na Lissutangu anagombania ubunge wa kwanza, ni mlinzi wake, ndugu yake, dereva wake wanaishi naye nyumba moja, muda ukifika atasema,” alisema Mbowe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles