28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Mutharika ashinda muhula wa pili urais

LILONGWE, MALAWI

RAIS Peter Mutharika amechaguliwa kwa muhula wa pili kuwa rais wa Malawi baada ya kupata ushindi katika uchaguzi wa wiki iliyopita uliogubikwa na madai ya udanganyifu.

Mutharika amepata ushindi mwembamba wa asilimia 38.6 ya kura akimpita mpinzani wake wa karibu, Lazarus Chakwera wa Chama cha Malawi Congress (MCP) aliyejipatia asilimia 35.4.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jane Ansah aliyetangaza matokeo hayo alisema; “ninapenda kutanguliza pongezi zangu kwa rais mteule na makamu wake.

“Umechaguliwa na watu wa Malawi kuiongoza nchi kuelekea mustakabali bora, umepewa jukumu la kuongoza ajenda ya maendeleo ya taifa hili kwa miaka mitano ijayo.”

Matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo uliofanyika wiki iliyopita, yalitangazwa baada ya kubishaniwa mahakamani ambapo Chakwera alipata zuio la muda la mahakama kutokana na madai ya udanganyifu.

Jaji wa Mahakama Kuu, Charles Mkandawire aliondoa zuio hilo na dakika chache tu baadae tume ikathibitisha ushindi wa Mutharika.

MCP iliitaka Tume ya Uchaguzi kuchunguza madai 147 yaliyowasilishwa kuhusu hitilafu zilizojitokeza wakati wa uchaguzi huo.

Mahakama baadae ilisema kwamba uchunguzi kuhusu madai hayo unaweza kuendelea baada ya matokeo kutangazwa.

Vyama vya upinzani vimelalamika kwamba idadi kubwa ya karatasi za kupigia kura zilikuwa zimechezewa kwa kutumia wino wa kufanyia masahihisho.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, Rodney Jose ametoa onyo kali dhidi ya waandamanaji wa upinzani ambao walijitokeza katika mji mkuu wa Lilongwe na mji wa kaskazini wa Mzuzu akisema ghasia hazitavumiliwa.

Waangalizi wa Umoja wa Ulaya walielezea kampeni za uchaguzi kuwa ‘ziliandaliwa vyema, zilishirikisha wote na zilikuwa za wazi na zenye ushindani’.

Mutharika aligombea kupitia Chama cha Democratic Progressive (DPP) ambacho kilianzishwa mwaka 2004 na kaka yake Rais wa zamani, marehemu Bingu wa Mutharika. 

Rais huyo alitoa ahadi za kupambana na ufisadi na kuboresha miundombinu, lakini muhula wake wa kwanza ofisini ameshindwa kukabiliana na ufisadi na wimbi la mauaji ya wenye ualbino.

Yeye mwenyewe amekabiliwa na madai ya ufisadi ambapo Novemba mwaka jana alilazimika kurejesha kiasi cha Dola za Marekani 200,000 alizochangiwa na kama mchango kutoka kwa mfanyabiashara anayekabiliwa na tuhuma za rushwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles