23.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

Mtoto aliyelazwa siku 490 aruhusiwa

 AVELINE KITOMARY– DAR ES SALAAM

HATIMAYE Daudi Mikidadi (17), ameruhusiwa jana kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH), baada ya kukaa hospitalini siku 490 sawa na mwaka mmoja na miezi mitano.

Katika siku hizo, alitumia siku 127 akiwa chumba cha uangalizi maalumu (ICU).

Daudi ambaye alikuwa anasumbuliwa na tatizo la upumuaji, alifikishwa hospitalini hapo Aprili 20, mwaka jana, akiwa na umri wa miaka 16 akitokea kituo cha kulelea watoto yatima cha Kurasini Children’s Home, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuruhusiwa, Daudi aliishukuru hospitali hiyo kwa huduma nzuri waliyompatia.

“Nawashukuru Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa mchango wao waliojitoa kwa mashine ya oxygen, wameweza kunitunza kwa miaka yote ,niliishi hospitalini kama nyumbani.

“Nimepata huduma nzuri, manesi wamenilea vizuri nilikuja sikuwa hivi, sasa hivi naweza kupumua nashukuru Mungu awabariki wote,”alisema.

Alitoa wito kwa Watanzania wenye moyo wa kusaidi waweze kufanya hivyo kutokana na uhitaji alionao.

“Kama kuna mtu atajisikia kufanya kitu kwa ajili yangu, inawezekana maana hii oxygeni inaweza kuisha, nitahitaji nyingine kama kuna Mtanzania yoyote anaweza kunisaidia anaweza kufanya hivyo,”alisema.

 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma MNH Aminiel Aligaesha alisema kuwa Daudia ataendelea kutumia mashine maalumu ya kumsaidia kupumua (oxygen concentrator). 

“Mikidadi ni kijana yatima kutoka Kituo cha Kurasini Children’s Home ambaye alilazwa Hospitalini hapa Aprili 20, mwaka jana akiwa anaumwa sana na kushindwa kupumua vizuri hivyo kuwekwa kwenye mashine ya kumsaidia kupumua.

“Uchunguzi ulifanyika na kugundua kuwa mapafu yote mawili yameharibika kutokana na kuugua ugonjwa mmoja wapo wa mapafu (ugonjwa umehifadhiwa), atahitaji usaidizi wa mashine ya kupumulia kwa maisha yake yote au kupandikizwa mapafu yote mawili. 

“Watalamu wameridhika hali aliyonayo sasa, anaweza kurudi kwenye kituo chake,hospitali ikishirikiana na kituo hicho wameandaa chumba maalumu chenye umeme na mahitaji mengine muhimu kwa ajili yake,”alisema.

Alisema hospitali imegharimia matibabu yake yote, imempa msaada wa mashine ya kumsaidia kupumua (oxygen concentrator).

“Madaktari walioko kwenye mafunzo kwa njia ya vitendo (intern doctors), wamechanga na kumnunulia mtungi wa oksijeni tiba, kuna msamaria mwema mwingine amempa msaada wa mashine ndogo ya kupumulia (portable oxygen machine).

 “Sehemu ya vifaa hivi vitamsaidia wakati akiwa nje ya chumba chake, umeme ukikatika au akiwa na safari yeyote na wakati anakuja kuhudhuria kliniki mbalimbali au kufanyiwa vipimo mara kwa mara kama mazoezi tiba,”alisema.

Alisema hospitali inatoa wito kwa wasamaria wema kutembelea kituo anachoishi Mikidadi ili kuendelea kumsaidia kwa mahitaji mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles