25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

MTIBWA, AZAM WANAVYOWAUMBUA WAKUBWA

NA MAREGES NYAMAKA

ZIMECHEZWA mechi nne hadi sasa msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara na tayari timu kongwe; Simba na Yanga, hazionekani katika nafasi mbili za juu katika msimamo wa ligi.

Simba ipo nafasi ya nne ikiwa imejikusanyia pointi nane sawa na Yanga ambao wanatofautiana kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Mtibwa Sugar ambao wikiendi iliyopita walipoteza asilimia 100 ya ushindi baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Ruvu Shooting, bado wapo kileleni mwa ligi hiyo na pointi 10.

Wakata miwa hao kutoka Turiani, Morogoro wamewazidi Azam FC iliyo nafasi ya pili na pointi 10 pia kwa wingi wa mabao ya kufunga.

Nafasi ya tatu inashikiliwa na timu iliyopanda daraja na inajivunia idadi kubwa ya wadhamini, Singida United, yenye pointi tisa baada ya michezo minne.

Azam FC na Mtibwa Sugar wote wameshinda michezo mitatu na kutoka sare moja kiasi cha kuonekana tishio kwa Yanga na Simba wenye mashabiki lukuki.

Mtibwa Sugar ambao wananolewa na kocha mzawa, Zuberi Katwila, wameonyesha utofauti ambao unaweza kusema wameziumbua timu zilizotumia usajili mkubwa ikiwamo Simba inayojigamba kutumia zaidi ya bilioni moja.

Ikumbukwe Mtibwa Sugar haijafanya usajili wa kutisha au wa wachezaji wenye majina makubwa kama ilivyo utamaduni wao misimu yote licha ya kuondokewa na wachezaji wao tegemeo kama vile, Salim Mbonde, Said Mohamed na Ally Shomari, ambao wote walitua Simba, lakini imeendelea kucheza soka la kuvutia na kupata matokeo bora.

Licha ya wadau wa soka kuendelea kuichukulia kama ni ya kawaida yao kuongoza ligi kwa muda, lakini hawa hawa ndio waliofanya vibaya msimu uliopita wakiwa na kocha wao huyo huyo ambapo takribani mechi saba walitoka sare.

Kwa upande wa Azam FC chini ya kocha wao, Aristica Cioaba raia wa Romania, ambaye muda wote wa mchezo anasimama kutoa maelekezo kwa wachezaji huku akionyesha ukali, haikupewa nafasi na wadau wengi ya kuanza vyema ligi.

Hatua hiyo ilitokana na kuondokewa na wachezaji wake tegemeo akiwemo nahodha John Bocco, kipa Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni (wote Simba) na Gadiel Michael aliyetua Yanga wakiwa kama chaguo la kwanza, lakini imekuwa tofauti kabisa.

Takwimu zinaonyesha Wanalambalamba hawa ni timu pekee ambayo haijaruhusu wavu wao kuguswa ambapo langoni anasimama Mghana, Razak Abalora, aliyesajiliwa dakika za mwisho. Abalora tayari anaanza kuizoea ligi.

Safu ya ushambuliaji ya Azam FC inaongozwa na Mbaraka Yusuph aliyejiunga na timu hiyo akitokea Kagera Sugar na sasa ndiye aliyechukua mikoba ya Bocco ambapo tayari amefunga mabao mawili kati ya matatu waliyofunga katika michezo yote minne.

Viungo wamekuwa mhimili muhimu kwa timu hiyo kupata matokea kutokana na kocha huyo kuchezesha viungo watano kwa wakati mmoja ambao ni Himid Mao, Stephan Kingue, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo na Bruce Kangwa.

Huku Mtibwa Sugar wakionekana kuanza vizuri msimu huu, Kagera Sugar imekuwa na matokeo ya kusuasua na kuzua mshangao mkubwa kwa wadau wa soka kulingana na ubora waliomaliza nao msimu uliopita.

Wanankurunkumbi hao wanaonolewa na kocha bora wa msimu uliopita, Mecky Mexime, aliyekiongoza kikosi hicho kumaliza nafasi ya tatu hadi sasa hakijaonja ladha ya ushindi na wanaburuza mkia wakiwa na pointi moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles