Na Mauli Muyenjwa, Dar es Salaam
MSAJILI wa Vyama vya Siasa, Francis Mutungi amesema licha ya uchaguzi wa mwaka huu kughubikwa na ushindani, muda muafaka ukifika rungu litawadondokea wanasiasa wanaokwenda kinyume na makubaliano waliyoyasaini.
Alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa mafunzo kwa mawakala wa usimamizi wa vyama vya siasa ya kuwaandaa katika uchaguzi mwaka wa mwaka huu.
“ Tuelewe kwamba kuna maisha baada ya uchaguzi, wanasiasa wafanye amani iwe kipaumbele na kila mtu ana wajibu kuufanya uchaguzi kuwa salama… chama kinapokosea kitaadhibiwa,” alisema Mutungi.
Alisema mawakala wapatao 1,300 kutoka katika vyama vya siasa watapatiwa mafunzo hayo katika siku zijazo na 30 walianza mafunzo hayo jana.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) ambalo ni wadhamini wa mafunzo hayo, Awa Dabo, alivishukuru vyama vya siasa akisema mawakala hao wakifundishwa watajiamini na matokeo ya uchaguzi yatakua ya kweli na ya haki.
“Mawakala kutoka katika vyama vya siasa wanatakiwa kujua sheria za uchaguzi na utaratibu. Wanahitaji kufundishwa waweze kushiriki vizuri katika mchakato huo lakini pia wanatakiwa kujua haki zao na wajibu katika utendaji na mamlaka yao,” alisema Dabo.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Peter Mziray alisema ikitokea kuvunjika amani na purukushani nchini, baraza la vyama vya siasa lazima lilaumiwe kwa vile linahusisha vyama vyote.
Akizungumza kwenye ufunguzi huo, Mwenyekiti wa Chama cha UMD, Kamana Masoud, alisema uchaguzi wa mwaka huu ni mgumu kuliko wa miaka yote iliyopita na kuna wasiwasi mawakala kuweza kununuliwa na kuchakachua kura.