29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Mradi wa usambazaji gesi majumbani Sinza kukamilika ndani ya miezi sita

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC limesema mradi wa usambazaji wa gesi asilia majumbani katika nyumba 506 ndani ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, umeanza kwa kasi na utakamilika baada ya miezi sita.

Hayo yamebainisha mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk. James Mataragio, mara baada ya kufanya ziara ya kujionea utekelezaji wa maagizo ya waziri wa Nishati,(Dk. Medard Kalemani) aliyemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo ambayo ni Kampuni ya BQ kukamilisha mradi huo ndani  ya muda mfupi  na si mwaka  mmoja kama ulivopangwa.

Dk.Mataragio amesema, baadhi ya changamoto ambazo zingechelewesha mradi huo zimeshapatiwa ufumbuzi na kufafanua kuwa mradi huo ungetumia mwaka mmoja kutokana na uagizaji wa vifaa nje ya nchi kutumia muda wa takribani miezi sita mpaka kufika nchini.

“Kikubwa ambacho kilikuwa kinauchelewesha mradi huu ilikuwa ni uagizaji wa vifaa vya kuunganishia gesi na vya kupunguza presha, sasa tumepata vifaa hapa nchini kupitia kampuni ya Plascom ambayo imeamua kusambaza mabomba hayo.

“Jambo lingine ni upatikanaji wa PRS ambazo Mkandarasi ameamua kuzilipia moja kwa moja kiwandani na zitafika hapa nchini baada ya miezi miwili, tayari mitaro imeanza kuchimbwa kwa ajili ya kutandaza mabomba ya gesi, kazi hii itatumia miezi miwili hivyo tunategemea kufikia mwezi Agosti, Mwaka huu mradi huu utakuwa umekamilika na utakuwa maeneo mawili, Sinza  na eneo la Barabara ya Kilwa Barracks,” amesema Dk. Mataragio.

Dk.Mataragio ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutawezesha nyumba zaidi ya 500 zitanufaika na matumizi ya nishati hiyo ya gesi asilia.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya BQ, Mhandisi John Buza, amesema changamoto kubwa waliyokumbana nayo katika utekelezaji wa mradi huo ni wafanyabiashara nchini kuwauzia vifaa vinavyohitajika katika utekelezaji wa mradi huo kwa  gharama kubwa tofauti na zinavyouzwa nje ya nchi.

“Tuliwaeleza ukweli na kuwaambia tutaagiza vifaa hivyo nje kwasababu nje ni rahisi kuliko hapa nchini na tulifikia muafaka wakashusha bei hivyo tunawaomba hawa wasambazaji wa vifaa vya gesi asilia wasitumie nia bora ya serikali kuwahudumia wananchi kama fursa kwao kupandisha bei ya vifaa vinavyohitajika,”amesema Mhandisi Buza.

Aidha, Dk.Mataragio ameonya wafanyabiashara kuacha mchezo mchafu wa kuongeza bei ya vifaa vya kuunganishia gesi kwani nia ya serikali kukutana nao na kuwahakikishia soko la uhakika haikuwa kibali kwao kuanza kuuza kwa gharama za juu.

“Serikali ina nia njema ya kuwawezesha wazalishaji wazawa, sasa wasitumie mwanya huo kuongeza bei ya bidhaa mfano bomba wameongeza bei, ukibainika hilo ni kosa sawa na uhujumu uchumi, amesema Dk. Mataragio.

Awali wakati wa uzinduzi wa mradi huo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo alisema asilimia 75 mpaka 80 ya nishati ya kupikia majumbani hususan  katika wilayani humo ni mkaa, na asilimia nyingine iliyobaki ni gesi ya mitungi na umeme.

“Gesi ya mtungi gharama yake ni Sh 48,000 mpaka Sh 50,000  na  gunia moja la mkaa ni Sh 70,000 mpaka Sh 80,000  na katika familia yenye watu watano gunia moja la mkaa kwa mwezi halitoshi.

“Pia katika matumizi ya gesi  ya mtungi mmoja hautoshi kwa familia ya watu wanne, lazima kuwe na nishati nyingine mmbadala hususani mkaa,”amesema Chongolo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles