23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

MRADI KILIMO-BIASHARA SBL WAONGEZA UZALISHAJI KWA ASILIMIA 70

Na Mwandishi Wetu


KAMA ilivyo kwa nchi nyingi za Kiafrika, Tanzania ni moja kati ya nchi inayotegemea kwa kiasi kikubwa kilimo katika uchumi wake. Sekta ya kilimo inakadiriwa kuajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania, wengi wao wakiishi maeneo ya vijijini ambako ndiko asilimia karibu 80 ya Watanzania walipo.

Pamoja na kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa taifa, wakulima wamekuwa wakilalamika ukosefu wa masoko ya uhakika kwa mazao yao pale wanapovuna na kutaka kuyauza.  Ukosefu wa masoko ya uhakika umekuwa ukiwakatisha tamaa wakulima wengi.

Wakati Tanzania inaelekea kwenye uchumi wa viwanda, kilimo kinaendelea kuwa moja ya nguzo muhimu ya kuifanya nchi ifikie lengo hilo. Kilimo ni chanzo kikubwa cha malighafi kwa viwanda vingi hapa nchini.

Takribani miaka mitano iliyopita, Kiwanda cha Bia cha Serengeti (SBL) kilikuja na mkakati maalumu wa kuwasaidia wakulima kuzalisha zaidi mazao ambayo hutumika kama malighafi katika uzalishaji wake wa bia ikiwamo shayiri, mtama, ulezi na mahindi. SBL ni wazalishaji wa bia za Serengeti Lager, Serengeti Lite, Pilsner, Kibo Gold, Kick, Uhuru na Senator Lager.

Mradi huo unaojulikana kama Kilimo-Biashara, unatekelezwa katika mikoa ya Arusha, Manyara, Mbeya, Kilimanjaro, Singida, Morogoro, Shinyanga na  Dodoma.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa SBL, John Wanyancha, mradi wa Kilimo-Biashara umetoa jibu  kwa tatizo la ukosefu wa masoko kwa wakulima wa ndani ambao kipindi kirefu wamekuwa wakilia kutokana na ukosefu wa soko la uhakika la bidhaa zao.

“Hii ni fursa pekee ambayo Watanzania wanahitaji kuitumia na hasa ikizingatiwa kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha soko la ndani. Serengeti inaamini kuwa Watanzania wana uwezo wa kuzalisha malighafi bora na tukazitumia pia kupata bidhaa bora,” anafafanua Wanyancha.

Kwa mujibu wa Wanyancha, mradi huo umekuwa na mafanikio mazuri, hali ambayo anasema kuwa imechangiwa na uhalisia wake, kwa maana ya kutowapa usumbufu wakulima juu ya mchakato  wake.

Chini ya mradi huo, Kampuni ya Bia ya Serengeti inatoa mbegu zenye ubora bure kwa wakulima na pia kuwaunganisha na taasisi mbalimbali za kifedha ili kupata mtaji utakaohitajika kwa kilimo cha mashamba makubwa. Halikadhalika kuwawezesha kupata mbolea pamoja na pembejeo nyingine za kilimo.

“Ili kuhakikisha kuwa wakulima wanafaidika, SBL imekuwa ikinunua mazao yote kutoka kwa wakulima hao na hivyo kuwawezesha kurejesha walichokopa lakini pia kuboresha hali zao kimaisha,” anaelezea Wanyancha.

Pamoja na mafanikio hayo, SBL inaona bado kuna umuhimu wa kuendelea kutoa fursa kwa wakulima wa ndani kupitia programu yake hiyo, ili kulipa fadhila kwa Watanzania ambao kwa sehemu kubwa ndio wateja wa bidhaa zake zote. Mpango uliopo kwa sasa ni kuendelea kuwahamasisha Watanzania kujiunga na mradi huo kwa manufaa zaidi.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi huo wa Kilimo-Biashara, Shafii Mndeme, anasema mafanikio yaliyopatikana ni makubwa na kuongeza kuwa wakulima wengi zaidi wanaendelea kunufaika na mradi.

Akizungumza na gazeti hili, Shafii  anasema mpango huo umefanikisha upatikanaji wa soko la uhakika kwa mazao ya wakulima na kuongeza kuwa kabla ya mradi kuanza, wakulima walikuwa hawana uhakika na soko la mazao yao.

Akitolea mfano wa mafanikio kwa msimu wa mwaka huu, anasema, kupitia mpango huo uzalishaji wa mazao umeongezeka kutoka tani 10,000 katika msimu wa mwaka jana hadi tani 17,000 katika msimu wa mwaka huu.

“Kutokana na uwepo wa soko la uhakika kwa mazao yao, wakulima sasa wanazalisha kwa wingi jambo ambalo linathibitishwa na ongezeko la tani 7,000 katika msimu wa mwaka huu ukilinganisha na msimu wa mwaka uliopita,” anasema.

Alisema ongezeko hilo la uzalishaji limekwenda sambamba na ongezeko la kipato kwa wakulima na kuongeza kuwa wakulima wengi sasa wananufaika na kilimo biashara ambacho kinawapatia kipato kizuri kinachowawezesha kuboresha maisha yao .

Shafii anasema uwepo wa soko la uhakika umeongeza hamasa kwa wakulima kulima kwa wingi zaidi na pia wakulima wengine ambao walikuwa hawajaingia ndani ya mradi wamekuwa na ari ya kuingia baada ya kuona manufaa ambayo wenzao waliopo ndani ya mradi wamekuwa wakiyapata.

Meneja huyo aliongeza kuwa SBL inadhamiria kuwafikia wakulima wengi zaidi kupitia utoaji wake wa mbegu pamoja na huduma za ugani ili kuwezesha kampuni kupata malighafi nyingi zaidi kutoka ndani ya nchi.

Tunaendelea kuuboresha na kuupanua mpango wetu huu wa kuwasaidia wakulima wetu wa ndani. Mwanzoni wakati tunaanza mradi, tulikuwa na idadi maalumu ya wakulima ambao tulilenga kuwafikia lakini kwa sasa tumeamua kupanua wigo kwa kuongeza idadi ya wakulima ambao tutawafikia,” alieleza.

Shafii alisema uzalisahaji wa bia kwa Kampuni ya SBL unategemea malighafi za ndani na kwa hiyo kampuni hiyo itaendelea kuwekeza kwa wakulima wa ndani kwa kuwawezesha kuzalisha zaidi

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles